• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

WOSIA: MSIGOMBANE NJIAN

Siku ya mazishi ya Mwl. Marko Shaidi tukiwa kweye ibada Vudee Mhe. Baba Askofu (mstaafu) wa Dayosisi ya Pare Stephano Msangi alitusimamisha watoto wote wa marehemu akatuambia; Msigombane Njiani. Maneno hayo yalisemwa na mtumishi wa Mungu Yusufu katika kitabu cha Mwanzo 45:21-24 wakati akiagana na ndugu zake, “Akaagana na ndugu zake, wakaenda zao, akawaambia msigombane njiani.” Yapo mambo mengi ambayo yanaweza kugombanisha ndugu kama vile; chuki, ubinafsi, kiburi, hasira, mamlaka, upendeleo na maovu mengine mengi. Yusufu alijua kwamba ndugu zake wangeweza kugombana kutokani na mali nyingi alizowapa. Yusufu aliwapa ndugu zake vitu vingi ikiwa ni pamoja na magari, nguo za kubadili, nafaka mikate na chakula cha njiani. Wangeweza pia kugombana kwa sababu Yusufu alimpendelea mdogo wake aitwaye Benjamani. Yusufu alimpa Benjamini fedha mia tatu na mavazi matano ya kubadili. Neno hili lilikuwa (relevant) sahihi kwetu kwa sababu na sisi wazazi wetu wametuachia mali mbalimbali kama vile nyumba, mashamba, ng’ombe na fedha. Katika safari yetu ya miaka kumi (10) kutoka tulipoagana na wazazi wetu tungeweza kugombana njiani kwa sababu moja au nyingine. Tunamshukuru Mungu kwa kuwa hatukugombana njiani. Tunamwomba Mungu atujalie neema ya umoja na upendo katika Yesu Kristo Bwana wetu.

Tunamwomba Mungu atusaidie tusigombane hata na wenzetu tunaokaanao. Bali tuwapende na kuwafanyia mema na kweli watu wote. Tuimbe wimbo Na 128 Fungu la 3, " Umande mzuri wa mbinguni, geuza mioyo yetu, tujae pendo lako. Tupendana na wenzetu, tuwafanyie mema tu na kweli watu wote. Kwetu uwe upendano ; Kugombana na kuwe mbali, tuwe na amani daima. " Na sisi wazazi wenu tunawausia watoto wetu na wajukuu zetu msigombane njiani bali upendo wa ndugu udumu. Upendo ni amri kuu aliyotuachia Bwana wetu Yesu Kristo. Yohana 13:34 " Amri mpya nawapa, Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo. " Tusigombane kwa kuwa sisi ni ndugu katika Kristo Yesu Bwana wetu. Safari yetu ya mbinguni inahitaji umoja, upendo, amani na furaha.

 

WOSIA: TUPENDANE NA TUWE NA UMOJA

Wazazi wetu Mwl. Marko Shaidi na mkewe Merina Marko siku moja walituita watoto wao na kutupa mausia mbalimbali. Msingi wa mausia hayo ulikuwa upendo na umoja wa kindugu. Walitushukuru kwa jinsi ambavyo tuliwatunza na wakasema wazi kuwa hawana la kutulaumu. Wakatuombea baraka za Mungu. Watu wengi hawapati nafasi kama hiyo ya kuwa na mazungumzo ya amani na furaha kabla ya wazazi wao kutwaliwa. Tunamshukuru  Mungu kwa kutupa nafasi hiyo kama alivyompa Israeli yaani Yakobo kabla ya kulala. Mwanzo 49:1 “Yakobo akawaita wanawe, akasema, kusanyikeni, ili niwaambie, yatakeyowapata siku za mwisho.” Wazazi wetu walituusia kulingana na neno la Mungu; Zaburi 133:1 “ Tazama, jinsi ilivyo vyema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” Waebrania 13:1, 16 “Upendano wa ndugu na udumu. Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana, maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.” Tukiwa na upendo sisi kwa sisi watu wote watatambua ya kuwa sisi ni wanafunzi wa Bwana wetu Yesu Kristo.Yeye ampendaye ndugu yake, akaa katika nuru wala ndani yake hamna kikwazo. Bali yeye amchukiaye ndugu yake yu katika giza, tena anakwenda katika giza, wala hajui aendako, kwa sababu giza imempofusha macho (1 Yohana 2:10-11). Mausia haya ya wazazi wetu tunatakiwa tuyasikie na kuyazingatia. Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye; bali mwenye dharau hasikilizi maonyo. Tunamwomba Mungu atujalie neema ya kuwafundisha watoto wetu neno la Mungu kwa maana litakuwa kilemba cha neema vichwani mwao na mikufu shingoni mwao. Haleluya, Yesu Kristo ni yule yule jana, leo na hata milele.

Share This