SIFA KUU ZA SADAKA INAYOMPENDEZA MUNGU
Utoaji wa sadaka au dhabihu ni agizo la Mungu mwenyewe . Mungu alimwagiza Abraham amtolee sadaka ya mwana wake mpendwa Isaka. Mwanzo 22:2 “Akasema umchukue mwanao mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria , ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmoja wapo nitakaokwambia. “Katika kitabu kile cha Kutoka 25:1 “Bwana akanena na Musa akamwambia, waambie wana wa Israeli kwamba wanitwalie sadaka , kila mtu ambaye moyo wake wampa kupenda mtatwaa kwake sadaka yangu”. Neno la Mungu linatufundisha kuwa Mungu ni mtoaji wa sadaka pale alipomtoa mwanae pekee ampendaye afe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu na wokovu wetu. Bwana wetu Yesu Kristo naye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu Baba yetu. Waefeso 5:2 “Mkaenende katika upendo , kama Kristo naye alivyowapenda ninyi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu , kuwa harufu ya manukato”. Baada ya kuangalia maneno hayo ya utangulizi tutafakari na kuona ni sadaka ya namna gani yenye kibali inayompendeza na kugusa moyo wake.Tutagawanya somo hili katika sehemu kuu tatu; sifa zinazotokana na aina ya moyo unaotoa sadaka , pili aina ya sadaka inayotolewa na tatu mazingira sahihi ya kutolea sadaka .Moyo unaoweza kutoa sadaka inayompendeza Mungu unatakiwa uwe na upendo,mnyofu , wenye furaha , haki imani wenye kusamehe na uliovunjika na kupondeka .Utoaji wa Mungu na wa Bwana wetu Yesu Kristo alitokana na upendo.Yohana 3:16 “ Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu , hata akamtoa mwanawe pekee ili kila mtu amwaminiye asipotee bali awe na uzima wa milele.” Kama tulivyoonyeshwa hapo juu kwenye Waefeso 5:2 tunaona na kuamini kuwa Yesu Kristo alitupenda akaitoa nafsi yake kwa ajili yetu . Kwa hiyo ili sadaka yako impendeze Mungu unatakiwa umpende Mungu kwanza , kwa moyo wako wote, akili yako yote na nguvu zako na umpende jirani yako kama nafsi yako. Ukimpenda Mungu utatii sauti yake .1 Samwel 15:22 “ Naye Samweli akasema , Je? Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu sawa sawa na kuitii sauti ya BWANA? Angalia , kutii ni bora kuliko dhabihu, na kusikia kuliko mafuta ya beberu”. Mungu huzipima roho na Mungu huzitakabali sadaka za wenye haki, fadhili na rehema .Kutenda haki na hukumu humpendeza Mungu kuliko kutoa sadaka .Maana Mungu anataka fadhili na rehema si sadaka, na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa.Waebrania 10:8 “ Hapo juu asemapo , dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka , wala kupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema , tazama nimekuja niyafanye mapenzi yako”. Neno la Mungu linasema kuwa nao ulimwengu unapita pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele. Warumi 12:2 “ Wala msifuatishe namna ya dunia hii, bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema ya kumpendeza na ukamilifu”. Kinyume cha kufanya mapenzi ya Mungu ni kutenda dhambi. Mithali 15:8 “Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA, bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha kwake” Tukileta sadaka zetu mbele za Mungu tunatakiwa kutubu dhambi zetu tukimsihi Mungu atuwie radhi sisi wenye dhambi .Tuje mbele zake na roho zilizovunjika, moyo uliovunjika na kumpondeka. Tutoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo. Sadaka yenye kibali, inayomgusa Mungu na inayompendeza ni ili yenye msamaha ,Mathayo 5:23-24 “ Basi ukileta sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu uende zako upatane kwanza na ndugu yako, kisha rudi utoe sadaka yako”. Zaidi ya hayo yote tujivike upendo , maana ndio kifungo cha ukamilifu .Kumbuka sadaka ni tendo la hiari la kumtolea Mungu wako huhitaji kushurutishwa wala kulazimishwa. 2 Wakoritho 9 :7 “ Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake si kwa huzuni wala si kwa lazima, maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu” . Mheshimu BWANA kwa mali yako yote kwa maana ana wingi wa siku katika mkono wake wa kuume , utajiri na heshima katika mkono wake wa kushoto. Katika sehemu hii ya kwanza tumeangalia zaidi moyo unatakiwa wakati wa kutoa sadaka .Katika sehemu hii ya pili tutaangalia sifa ya aina ya sadaka inayotolewa ambayo inamgusa Mungu na kumpendeza, hatimaye huipa kibali mbele ya macho yake.Watoaji wa mwanzo wa sadaka ni watoto wawili wa Adamu ambao ni Kaini na Habili. Habili alikuwa mchunga kondoo na Kaini alikuwa mkulima ardhi. Mwanzo 4:3-5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA.Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama.BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake bali Kaini hakumtakabali , wala sadaka yake”. Mungu aliikubali sadaka ya Habili kwa kuwa alitenda vyema kwa kutoa vitu vilivyo bora, vilivyonona na wazaliwa wa kwanza .Kumbuka kuwa BWANA anasema wazaliwa wa kwanza wa wanyama na wa binadamu ni wake.Mungu anataka tumtolee vitu vyenye dhamani na wala sio mabaki au baadhi ya mali iliyozidi. Wakati Daudi alipotaka kiwanja kwa ajili ya kumjengea BWANA madhabahu kutoka kwa mtu aitwaye Arauna alikataa kupewa kiwanja hicho bure. 2 Samwel 24:24, “Lakini mfalme akamwambia Arauna, la sivyo, lakini kweli nitavinunua kwako kwa thamani yake, wala sitamtolea BWANA ,Mungu wangu sadaka ya kuteketezwa nisizozigharamia. Hivyo Daudi akanunua hicho kiwanja cha kupuria na wale ng’ombe kwa shekeli hamsini za fedha. Naye Daudi akamjengea BWANA madhabahu huko akatoa sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani. Basi BWANA aliiridhia nchi na tauni ikazuiliwa katika Israel.Katika kitabu kile cha Matendo ya Mitume 5:4 Anania na Safira sadaka yao ilikataliwa kwa kuwa hawakutoa thamani halisi ya kiwanja walichouza wakazuia kwa siri sehemu ya thamani yake. Petro akamwambia kilipokuwa kwako hakikuwa mali yako? Na kilipokuwa kimekwisha kuuzwa thamani yake haikuwa katika uwezo wako? Ilikuwaje hata ukaweka neno hili moyoni mwako? hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu. Anania aliposikia maneno haya akaaanguka akafa”. Ndugu zangu tujihadhari sana tusije hata siku moja kumtolea Bwana kwa udanganyifu Mungu hapendezwi na sadaka ziliyopatikana kwa udhalimu na kilema na kilicho kigonjwa. Katika Malaki 1:13 BWANA wa majeshi asema hivi, Nanyi mmeleta kitu kilichopatikana kwa udhalimu na kilema na kilicho kigonjwa; ndivyo mnavyoleta sadaka. Je, niikubali hii mikononi mwenu? Bwana anasema na alaaniwe mtu mwenye kudanganya amtoleaye Bwana kitu kilicho na kilema wakati yeye ni mfalme mkuu BWANA wa majeshi na jina lake la tisha katika Mataifa. Tukumbuke kuwa thamani inapimwa kulingana na vitu ulivyonavyo. Mfano. mzuri hapa ni ule wa mjane mmoja masikini aliyetoa senti mbili akatia sadaka yake katika sanduku la hazina na wale matajiri ambao nao walitoa sadaka zao. Bwana Yesu katika Luka 21:3-4 “akasema hakika nawaambia huyu mjane maskini ametoa zaidi kuliko wote maana hao wote walitia sadakani katika mali iliyowazidi bali huyu katika umaskini wake ametoa vyote alivyokuwa navyo”. Tunajifunza pia kutoka kwa watu na Makedonia kuwa tunatakiwa kutoa sadaka kwa uwezo wetu na hata zaidi ya uwezo wetu. 2Wakorintho 8:1-3”. Tena ndugu zetu twawaarifu habari ya neema ya Mungu waliyopewa makanisa ya Makedonia; maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao. Maana nawashuhudia kwamba kwa uwezo wao na zaidi ya uwezo wao kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao. Vitu vyote hivyo walivitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Tukumbuke kuwa kipimo tutakacho pima wakati wa kutoa sadaka ndicho hicho hicho na Mungu atakachotupimia. Kila mtu naatoe Mungu alivyombariki, aliye pewa vingi na atoe vingi. Luka 12:48. “Na yule asiyejua naye amefanya yasitailiyo mapigo atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakiwa vingi, naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi”. Tukumbuke pia ya kuwa apandaye haba atavuna haba. 2Wakorintho 9:6 “Lakini nasema neno hili apandaye haba atavuna haba, apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu”. Pamoja na kutoa mali zetu Mungu anataka tutoe kwanza, nafsi zetu kwa Bwana kwa mapenzi ya Mungu.Tuitoe miili na roho zetu kwa Bwana kwa kuwa hiyo ni sadaka inayompendeza. Warumi 12:1”. Basi, ndugu zangu nawasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhahabu iliyo hai , takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana”. Tunatakiwa tutoe maisha yetu kwa Mungu na kumruhusu Bwana Yesu atawale maisha yetu yote , tuwe mali yake , wala dhambi isitawale ndani ya miili yetu. Tutoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo .Ili uweze kutoa dhabihu za roho ni lazima uwe na imani kwa Mungu wako.Waraka wa Waebrania 11:6 “ Lakini pasipo na imani haiwezekani kumpendeza kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa dhawabu wale wamtafutao”. Wakati unapotoa sadaka yako umwombe Roho Mtakatifu akupe neno la kusimamia sadaka yako na akufundishe na kukuongoza jinsi ya kumtolea BWANA, Mungu wako. Katika sehemu hii ya tatu tutaangalia mazingira sahihi ya kumtolea BWANA sadaka zetu. Sadaka inatakiwa itolewe katika mazingira ya siri .Mathayo 6:1-4 “ Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu kusudi mtazamwe na wao kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni.Basi wewe utoapo sadaka, usipige panda mbele yako kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani, ili watukuzwe na watu .Amini, nawaambieni , wamekwisha kupata dhawabu yao .Bali wewe utoapo sadaka , hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume , sadaka yako iwe kwa siri , na baba yako aonaye sirini atakujazi Mungu humshusha yeye ajikwezaye au mwenye majivuno lakini humkweza yule ajishushaye na kunyenyekea mbele ya uso wake 1 Petro 5:6 “ Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari , ili awakweze kwa wakati wake”. Tusiwe kama mafarisayo ambao matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu kwa kuwa kufanya hivyo wamekwisha kupata thawabu yao .Bali wewe utoapo sadaka yako usionekane na watu ila na baba yako aliye sirini , na baba yako aonaye sirini atakujazi au atakupa. Sadaka inatakiwa kutolewa katika hali ya utulivu na uchaji kwa kuwa sadaka ni sehemu ya ibada. Kuna sadaka ambazo Mungu anakuagiza uzitolee mahali maalumu ambapo Mungu amepachagua .Roho Mtakatifu atusaidie tuweze kusikiliza sauti ya Mungu .Tusitoe sadaka zetu kwenye madhabahu ya miungu isipokuwa kwa Mungu wetu mahali ambako jina lake lipo .Mungu alimpomtaka Abrahamu amtolee sadaka alimwonyesha sehemu aliyoichagua katika nchi ya Moria juu ya milima. Tuhitimishe somo hili kwa kusisitiza kuwa tuwe na shauku katika mioyo yetu ya kumtolea Mungu kwa hiari yetu wenyewe.Tutoe vitu vyetu vya thamani vitiwe katika hazina ya nyumba ya BWANA kwa furaha na kwa utukufu wa Mungu kwa kuwa, hazina yako iliyopo ndipo utakapokuwapo na moyo wako 1 Mambo ya Nyakati 29:11-14 “ Ee BWANA , ukuu ni wako , na uweza na utukufu na kushinda na enzi , maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako, Ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote , na mkononi mwako mna uweza na nguvu , tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea”. Mungu alibariki Neno lake.