NAMI NITAWAJALIA MAISHA MAREFU
Mungu anawaahidi wateule wake wamchao, wenye kumtumikia kwa moyo wa ukamilifu na wenye kutenda haki ya kuwa atawajalia maisha marefu. Hesabu ya siku zao ataitimiza kwani anazijua siku za wakamilifu. Imetupasa kumwogopa Mungu na kumpenda,kumheshimu na kumtumikia na kumtii kwa moyo wote Mithali 10:27 “Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; bali miaka yao wasio haki itapunguzwa.” BWANA anasema mtu mwenye haki hakika ataishi. Midomo ya mwenye haki hulisha watu wengi; bali wapumbafu hufa kwa kuwa hawana ufahamu. Mtumishi wa Mungu Nehemia kwa kujua ukweli huo anasema, “Unikumbukie,Ee Mungu wangu, kwa mema yote niliyowafanyia watu hawa(Nehemiah 5:19). Heri mtu yule amkumbukaye mnyonge BWANA atamwokoa siku ya taabu. BWANA atamlinda na kumhifadhi hai. Mungu anaweza kukujalia maisha marefu kama utaenenda kwa ukamilifu na kuomba kama mfalme Hezekia ambaye Mungu alimwambia atakufa. Isaya 38:2-5 “Basi Hezekia akajigeuza akaelekeza uso wake ukutani akamwomba BWANA, akasema, Ee, BWANA kumbuka haya, nakusihi,kwamba nimekwenda mbele zako katika kwelii na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana. Ikiwa neno la Mungu likamjia Isaya,kusema,Enenda ukamwambie Hezekia BWANA Mungu wa Daudi baba yako asema hivi,Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama nitaziongeza siku zako kiasi cha miaka kumi na tano.” Hata wewe na mimi tukienenda sawa saw ana mapenzi ya Mungu atatuongezea siku za kuishi hapa duniani.
Amri ya nne ina ahadi ya kupata maisha marefu nayo yasema, Waheshimu baba yako na mama yako,siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na BWANA Mungu wako. Imetupasa tusiwakasirishe,wazazi wetu ila uwaheshimu, tuwatumikie, tuwatii na tuwapende kwa moyo . Mithali 1:8 Mwanangu, yasikilize mafundisho ya baba yako, wala usiiache sheria ya mama yako,kwa maana hayo yatakuwa kilemba cha neema kichwani pako na mikufu shingoni mwako.” Mithali 30:17 “Jicho la mtu amdhihakiye; babaye, na kudharau kumtii mamaye; kunguru wa bondeni wataling’oa, na vifaranga wa tai watalilaa.”
Imetupasa tuzingatie maonyo haya kwa kuwa kushindwa kuyafuata ni dhambi mbele za Mungu na mshahara wa dhambi ni mauti Afuataye maovu hufuata mauti yake mwenyewe bali haki huokoa na mauti ukiacha dhambi zako kwa kutenda haki, ukaacha maovu yako kwa kuhurumia maskini utazidishiwa siku zako za kuishi hapa duniani tena utaishi kwa raha. Wapendwa tusiombe tu maisha marefu hapa duniani bali tuombe karama ya Mungu ambayo ni uzima wa milele katika Yesu Kristo Bwana wetu. Pamoja na kuomba maisha marefu tumwombe Mungu tuwe uzao mteule wenye baraka tele sawa sawa na ahadi zake kwa wateule wake; na sawa sawa na Neno lake Utukufu na eweza una yeye hata milele na milele Amina.