TULINDE NA KUIMARISHA IMANI YETU KATIKA YESU KRISTO BWANA WETU
Imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo. Imani inahitaji kulindwa ndio maana mtume Paulo katika 2 Timotheo 4: 7 anasema “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda.” Imani inahitaji kuimarishwa kupitia maombi. Luka 22:32. “lakini nimekuombea wewe ili imani yako isitindike nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako.” Zipo njia nyingi za kulinda na kuimarisha imani ya mkristo. Katika makala hii nina mambo matatu ambayo tukiyafanya na kuyazingatia kama ukoo wa Shaidi yatasaidia kulinda na kuimarisha imani yetu kwa BWANA wetu Yesu Kristo. Mambo hayo matatu inawezakana kabisa kuwa mababu na wazazi wetu walishafanya maombi kwa uelewa wao wa wakati wao, na sisi tutafanya maombi kwa uelewa na wakati wetu kulingana na ufahamu wetu wa neno la Mungu. Inawezakana pia kuna watu binafsi walishafanya maombi yao kuhusu mambo haya lakini sasa tunayafanya kwa pamoja kama ukoo wa Shaidi. Maombi yetu yatahusu mambo matatu kama ifuatavyo: -
· Tukatae na kufuta maneno yote mabaya yaliyosemwa wakati wa mababu zetu na mababa zetu na yanayosemwa sasa juu ya uzao wetu. Maneno mengine ambayo yamesemwa na watesi wetu lakini mengine tumejitamkia na kujinenea sisi wenyewe na ndugu zetu. Maneno kama hayo huweza kutudhoofisha kiroho. Tuombe hekima ya Mungu juu ya watesi wetu; Luka 21:15. “kwa sababu mimi nitawapa kinywa cha hekima ambayo watese wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.” Tujitamkie maneno ya baraka yanayopatikana katika Neno la Mungu.
· Tukatae na kujitenga na madhabahu za miungu na ibada za sanamu na mambo ya kishirikina.Tukatae ibada zozote zile zilizofanywa na mababu zetu “Vyachome Vyaviombo” na tukatae maagano yote yaliyoingiwa katika ibada hizo. Tusije tukajihusisha wala tukahusishwa wala kutajwa katika ibada za miungu. Kutoka 20: 3-4 “usiwe na miungu mingine ila mimi usijifanyie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni wala kilicho duniani wala kilicho majini chini ya dunia.” Tumuombe Mungu aturehemu kama alivyotuahidi katika neno lake. Luka 20:6 “nami nawarehemu maelfu wanipendao na kuzishika amri zangu.” Imani yetu iwe kwa BWANA wetu Yesu Kristo, kwa kuwa pasipo imani haiwezakani kumpendeza Mungu.
· Tuinue na kusimamisha madhabahu ya Mungu aliye hai Jehova mioyoni mwetu. Tumtukuze na kumsifu Mungu kwa wema na fadhili zake kwetu. Tukumbuke kuwa miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu na katika kila hekalu kuna madhabahu, Wakorintho 6:19 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu mliyopewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe.” Sasa basi mtukuzeni Mungu katika miili yenu. Tunainua na kusimamisha madhabahu hii ili tumwabudu Mungu katika roho na kweli.
· SADAKA YA UKOO WA SHAIDI
1. Sadaka ya ukoo wa Shaidi hutolewa kila baada ya miaka miwili katika madhabahu ya KKKT Chome au KKKT Vudee. Tunamshukuru Mungu kwa kutubariki na kuzidisha uzao wetu. Kwa sababu hiyo nyumba tulizo nazo hazitoshi kuweza kulala na kushiriki tendo la sadaka ya ukoo kwa furaha na amani. Kwa ajili hiyo kumekuwa na manung’uniko na malalamiko mengi kama ifuatavyo:
2. Manung’uniko au malalamiko kuhusu ndugu wengine wa Chome ambao hawashiriki Vudee wakati wa kutoa sadaka ya ukoo. Vivyo hivyo na wa Vudee ambao hawashiriki Chome.
3. Manung’uniko na malalamiko kuhusu ndugu wengine kusumbuka sana kwa kukosa sehemu za kulala Vudee na Chome .
4. Kuondoa manung’uniko na malalamiko hayo ninapendekeza kuwa ili tusije kugombana hapo baadae sadaka ya ukoo wa Shaidi itolewe kwa wakati mmoja Vudee na Chome
5. Manun’guniko yanayotokana na njia tunayotumia katika kutoa sadaka ya ukoo wa Shaidi. Njia ya kwanza ambayo ndiyo iliyozoeleka ni ile ya kuchanga sadaka na kuweka katika kikapu kimoja na kisha kiongozi wa ukoo kupeleka sadaka hizo madhabahuni mwa Bwana. Njia ya pili ni ile ya kila mtu kupeleka sadaka yake yeye mwenyewe madhabahuni . Wengine wanawalalamikia wale wanatoa kwa njia hii ya pili wakiamini kuwa wamevunja makubaliano ya kutoa kwa kutumia njia ya kwanza. Sadaka inayompendeza Mungu ni ile iliyotolewa kwa siri. Mathayo 6:4 ‘’ Sadaka yako iwe kwa siri, na Baba yako aonaye sirini atakujazi.’’ Wala utoapo sadaka usipige panda mbele yako. Ni wajibu wetu kuangalia katika njia hizi mbili ni ipi inayoendana na Neno la Mungu. Tusiogope kujisahihisha tunapopata maono mapya, ili tutoe sadaka zetu kwa njia inayompendeza Mungu tunayemtolea.
Tarehe au majira ya kutoa sadaka ya ukoo, neno la kusimamia sadaka ya ukoo, wimbo, pamoja na mambo ya kuombea (prayer items) vitolewe na kutangazwa na kiongozi wa ukoo wa Shaidi. Utaratibu huu utasaidia kuondoa manung’uniko na malalamiko mbalimbali yaliyopo.
6. Itasaidia watoto wetu, wajukuu na vitukuu wa Shaidi kushiriki kwa wingi zaidi katika sadaka ya ukoo.
7. Itasidia kujenga imani imara katika Yesu Kristo Bwana wetu.
Tukumbuke kuwa hatuwezi kutoa sadaka inayompendeza Mungu ikiwa tunanung’unika na kulalamika mioyoni mwetu. Wafilipi 2:14 “Yatendeni mambo yote pasipo manung’uniko wala mashindano ili mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama.”
vMaamuzi kama haya ya hekima na busara yalifanywa na baba yetu wa Imani Abraham na nduguye Lutu. Mungu aliwabariki kiasi kwamba nchi ile haikuwatosha tena hata wachunga wanyama wao wakagombana. Abraham akamwambia Lutu achague upande atakaotaka kwenda ili wasigombane kwa kuwa wao ni ndugu (Mwanzo 13: 1-18). Na sisi wa ukoo wa Shaidi ni ndugu hivyo ni vyema kila mtu achague kutolea sadaka ya ukoo Vudee au Chome. Mungu atusaidie tusije tukagombana njiani. Umoja na Amani na upendo udumu kati yetu. Jina la BWANA lihimiliwe
Hayo yote yatawezekanaje?
· Yatawezekana kwa kuomba toba na rehema.
Matendo ya Mitume 3:19 “Tubuni basi mrejee, ili dhambi zenu zifutwe,zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana.”
Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda hata utusamehe makosa yetu yote na kutuhuisha pamoja na Kristo yaani tumeokolewa kwa neema (Waefeso 2:4).
· Yatawezekana kwa kuinua jina lenye nguvu, uweza na mamlaka; Jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Tukiomba kwa jina hili lipitalo majina yote, yote yatawezekana. Matendo ya Mitume 4:12” Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana Hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu lipasalo sisi kuokolewa kwalo.”
· Yatawezekana kwa damu inayonena mema kinyume cha mabaya yote, damu ya Bwana wetu Yesu Kristo. Waebrania 12:24 “Na Yesu mjumbe wa agano jipya na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.” Ufunuo 12:24 “Nao wakamshinda (Ibilisi/Shetani) kwa damu ya Mwana Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao,ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.”
· Yatawezekana kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo,lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Roho wa Mungu njoo kwetu utuongoze. Neema na iwe nasi, na rehema na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu.
Hayo yote yatawezekana kwa kuwa hakuna neno lililo gumu la kumshinda Bwana wala lisilowezekana kwa Mungu. Yeremia 32:27 “Mimi ndimi Bwana Mungu wa wote wenye mwili. Je, kuna jambo lolote lililo gumu asiloliweza.”
Mungu atusaidie katika tafakari hii ili yote yafanyike kwa utukufu wa jina lake. Jina la BWANA lihimidiwe.