• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

KUMILIKI MLANGO WA ADUI KWA MAOMBI

Tukiomba kulingana na Neno la Mungu sawa sawa na mapenzi yake tunapata nguvu ya kumiliki mlango wa adui na kuufunga. Kuomba kunatusaidia tusiingie majaribuni au kuufunga mlango wa majaribu. Mathayo 26:40 (a) “Kesheni,mwombe,msije mkaingia majaribuni.” Yakobo 4:3 (b) “Mwafanya vitu na kupigana,wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi.” Maombi yanauwezo wa kuzuia jambo la kishetani ambalo lilipangwa likupate, lakini kwa maombi yako ya kulizuilia hakika jambo hilo halitakupata. Kwa kuwa Neno la Mungu linatupa mamlaka hayo. Mathayo 18:18 “Amin,nawaambieni,yoyote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni;na yoyote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni.” Nguvu na mamlaka hiyo utaipata kwa kumwamini na kumpokea Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yako. Kumbuka kuwa ukiokoka unakuwa uzao wa Ibrahimu na uzao wa Yesu Kristo Wagalatia 3:29 “Na kama ninyi ni wa Kristo,basi mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawa sawa na ahadi.”  Ahadi mmoja wapo ya uzao wa Ibrahimu ni kumiliki mlango wa adui. Hivyo sifa moja kuu ya uzao wa Yesu Kristo ni uwezo wa kumiliki mlango wa adui. Nje ya uzao huo huwezi kwa namna yoyote ile kufunga mlango wa shetani wala kumkwepa na hila zake. Tunawezeshwa na Yesu Krsto Bwana wetu kumiliki mlango wa adui (shetani) kwa njia ya Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anaingia ndani yetu kisha anatuongoza katika kweli yote ambayo ni Neno la Mungu Katika vita ya kuufunga mlango wa adui Neno la Mungu linatutaka tuvae silaha zote za Mungu kuweza kuzipinga hila za shetani au kwa maana nyingine kuweza kumiliki mlango wa adui. Tusimame na kuvaa dirii ya haki vifuani mwetu. Waefeso 6:16-7 “Zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu,na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu. “Ndugu zangu wapendwa tuufunge mlango wa adui shetani na tubishe hadi mlangoni pa Bwana wetu Yesu Kristo,kwa kuwa ametukaribisha na ameahidi kutufungulia. Mathayo 7:7-8 “Ombeni,nanyi mtapewa; tafuteni nanyi mtaona; bisheni nanyi mtafunguliwa. Kwa maana kila aombaye hupokea,naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa.” Katika Ufunuo 3:8 Neno la Mungu linasema, “Nayajua matendo yako. Tazama, nimekupa mlango uliofunguliwa mbele yako, ambao hapana awezaye kuufunga, kwa kuwa unazo nguvu kidogo, nawe umelitunza neno langu,wala hukulikana jina langu.” Tujitahidi kuingia katika mlango ulio mwembamba kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze (Luka 13:24).

Tunamwomba Mungu kwa neema yake kuu aturehemu tuingie kupitia mlango mwembamba unaoenda wokovu.

 

ULINZI WA MUNGU KWETU

Tunamshukuru Mungu kwa kuzidisha uzao wetu na kuulinda. Katika maisha yetu yote tumeshuhudia ulinzi wa Mungu kwetu. Mungu ndiye alindaye hakuna mwingine awezaye kulinda isipokuwa yeye peke yake 1 Petro 1:5 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wakovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.” Wala hakuna mtu awezaye kutupokonya katika mkono wa BWANA. Hakika mkono wa BWANA si mfupi hata ushindwe kuokoa. Tunaomba ulinzi wa Mungu kwetu na kwa vizazi vyetu kwa kuwa Bwana ni mwaminifu na wa haki. 2 Wathesalonike 3:3 “Lakini Bwana ni mwaminifu atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.” Tunamwomba Mungu awe mlinzi wetu, atulinde na mabaya yote, azilinde nafsi zetu. BWANA atulinde tutokapo na tuingiapo. BWANA atutie nguvu, atusaidie na atushike kwa mkono wa kuume wa haki yake. Tunamwomba Mungu ulinzi wa nyumba zetu, familia zetu na miji yetu. Zaburi 127:1 “BWANA asipoijenga nyumba waijengao wafanya kazi bure sisi hatutakesha bure kwa kuwa tutakukimbila Wewe. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Hatutaogopa kwa sababu BWANA wa majeshi yu pamoja nas, Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. BWANA anatuambia wana  wa Marko’s tusiogope tusonge mbele. Tusiogope kwa sababu BWANA wa majeshi yupo pamoja nasi, atatulinda, atatupigania AMEN.  

Share This