TUTUNZE UUMBAJI
Bwana Yesu asifiwe. Karibuni tutafakari somo hili tulilopewa kuhusu utunzaji wa uumbaji wa Mungu.
UTANGULIZI
Tuanze kwa kujiuliza swali: Uumbaji wa Mungu tunaotakiwa kuutunza ni upi?
· Uumbaji: (Mwanzo 1:1-31)
Kazi ya uumbaji ilimchukua Mungu siku sita mfululizo na katika siku hizo akaumba mbingu na nchi.
(i) Siku ya kwanza: Nuru na giza (mchana na usiku)
(ii) Siku ya pili: Anga (Mbingu)
(iii) Siku ya tatu: Nchi kavu na bahari; nchi yenye majani, miti ya matunda na mbegu.
(iv) Siku ya nne: Mianga (jua, mwezi na nyota) itoe nuru juu ya nchi.
(v) Siku ya tano: Viumbe wa baharini na ndege wa angani.
(vi) Siku ya Sita:
(a)Wanyama wa kufungwa, wa mwituni na watambaao
(b)Mtu kwa mfano na sura ya Mungu (mwanamume na mwanamke). Nitoe wito kwa kila familia ya Kikristo kuwafundisha watoto mpango huu wa uumbaji wa Mungu.
Mungu akaona kuwa kila kitu alichokiumba ni chema sana; mbingu na nchi zikakamilika na jeshi lake lote (Mwanzo 2:1). Ndio maana tunakiri katika imani yetu ya Kikristo kuwa ni Mungu mwenye enzi yote, muumba wa mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.
· UWAKILI
Ili kulinda na kutunza uumbaji wa Mungu serikali nyingi duniani zimeweka sera na sheria mbalimbali kama vile; sheria za bahari, sheria za ardhi, mazingira, misitu na sheria za kulinda wanyama pori na viumbe wengine wengi. Uwekaji wa sheria hizi ni jambo jema lakini jambo kubwa zaidi ni kuzingatia sheria na maagizo ya Mungu. Kazi ya utunzaji wa uumbaji huu tumekabidhiwa sisi wanadamu kulinda, kutawala na kuitiisha nchi. Wakili ni mtu aliyekabidhiwa mali ya mtu mwingine ailinde, aitunze na kuiongoza. Mungu ametukabidhi uumbaji wake ambao ni mali yake ili tuulinde, tuutunze na kuuongoza. Mwanzo 2:15 BWANA, Mungu akamtwaa huyo mtu akamweka katika bustani ya Edeni, ailime na kuitunza ; atawala wanyama na ndege na kuwapa majina.
Mungu ameturuhusu vitu alivyoviumba viwe chakula chetu Mwanzo 1:29. “Mungu akasema, Tazama nimewapa kila mche utaoa mbegu ulio juu ya uso wanchi yote pia,pia na kila mti, ambao matunda yake yenye mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu.” Pamoja na majani yote ya miche. Mwanzo 9:2-3 “Kila mnyama wa katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani; pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote.” . Jambo moja muhimu katika uwakili ni uaminifu, kwa hiyo tunatakiwa kuwa waaminifu kwa Mungu; kwani tutatoa hesabu siku Bwana atakapo kuja. Tunawajibika kwake kwa matumizi sahihi ya uumbaji yaani mbingu na nchi. Zaburi 24:1 “Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya BWANA, dunia na vitu vyote, vilivyomo ndani yake. I Wakorintho 4:1-2 “Mtu na atuhesabu hivi, kuwa tu watumishi wa Kristo, na mawakili wa siri za Mungu. Hapo tena inayo hitajiwa katika mawakili, ndiyo mtu aonekane kuwa mwaminifu.” Bwana wetu Yesu Kristo katika Luka 12:41-42 “Bwana akasema, ni nani basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule ambaye bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo.” Na kila aliyepewa vingi kwake huyu vitatakiwa vingi; naye waliye mwekea amana vitu vingi kwake huyo watataka zaidi. Mfano mzuri ni ule wa mtu aliye weka mali zake kwa watumwa wake watatu. Watumwa wawili waliweza kuzalisha talanta zao lakikini watatu hawakuzalisha chochote. Akawaambia wale waliozalisha ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya Bwana wako. Yule ambaye hakuzalisha akanyang’anywa hiyo talanta akapewa aliyenazo kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongozewa tele; lakini asiye na kitu hata kile alichonacho atanyang’anywa (Mathayo 25;14-29). Wakili mwema mwenye busara hulinda mali ya BWANA wake na kuendelea kuzalisha na kuzaa matunda mpaka BWANA wake atakapokuja.
· Je, tutautunzaje uumbaji huu?
Tutautunza uumbaji huu kwa kuzishika na kuzitii amri kumi za Mungu, sheria na maagizo yake yanayopatikana katika neno lake takatifu pamoja na kudumu katika maombi bila kukoma. Amri hizi zinatusaidia kutambua mahusiano sahihi kati yetu na Mungu na kati yetu na wanadamu wenzetu na vitu vyote alivyoviumba. Nitoe wito kwa familia za Kikristo kuwafundisha watoto kuhusu amri kumi za Mungu, na maana zake.
Mwanzo 1:22 “Mungu akavibarikia, akasema zaeni mkaongezeke mkayajaze maji na bahari, ndege wazidi katika nchi.” Tunatakiwa tuvitunze na kuviendeleza vitu hivi vyote Mungu alivyoviumba ; nchi kavu, bahari, mito, wanyama, misitu, anga na wanadamu. Tulime na kutafuta riziki zetu kwa maarifa bila ya kuharibu uumbaji wa Mungu. Hata hivyo mwanadamu amekuwa mharibifu wa uumbaji kwa njia mbalimbali kama vile;
· Uvuvi wa kutumia sumu na mabomu na nyavu zisizofaa,
· Ukataji wa misitu,
· Ujangili wa wanyama pori ,
· Silaha za maangamizi, na
· Uharibifu wa hali ya hewa (viwanda vichafu) na mengine mengi.
Matokeo yake ni pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi, majanga, ukame, njaa, kiu, magonjwa, mafuriko, maporomoko ya ardhi na madhara mengine mengi. Watu wengine wanaiba rasilimali hizi na kuzitumia vibaya kwa tamaa zao wenyewe. Amri ya saba inasema- Usiibe; wala tusipunje bali tusaidie kuongeza rasilimali na kuzilinda.
· Utunzaji wa mwanadamu;
Mwanadamu ni zao la uumbaji wa Mungu linalotakiwa kutunzwa .Mwanadamu anazo sehemu kuu tatu; mwili , roho na nafsi. Ili kutunza uumbaji huo kuna mambo muhimu ya kufanya.
Kutunza uzazi ili watu wazaane na kuongezeka na kuijaza nchi .(Mwanzo 1:28) “Mungu akawabarikia, Mungu akawaambia, zaeni, mkaongezeke mkaijaze nchi,na kuitiisha, mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi.” Nanyi zaeni, mkaongezeke, zaeni katika nchi, mkaongezeke ndani yake. Mambo Walawi 26:9 “Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza, nami nitalithibitisha agano langu,pamoja nanyi.” Nami nitakwenda kati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Shetani anapinga mpango huu wa Mungu kwa njia mbalimbali ambazo ni machukizo mbele ya Mungu kama vile, ndoa za jinsia moja, kuzuia uzazi na kuharibu mimba, kutupa watoto wachanga , magonjwa n.k Mambo ya Walawi 18:22-23 “Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo wala usilale na mnyama yoyote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye ni uchafuko.” Kwani mtu awaye yote atakaefanya machukizo hayo moja wapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao. Katika kitabu hicho hicho cha Mambo ya Walawi 20:13,15-16 Neno la Mungu linasema, “Tena mtu mume akilala pamoja na mtu mume, kama alalavyo na mtu mke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa, damu yao itakuwa juu yao. Tena mtu mume akilala na mnyama,hakika atauawa; nanyi mutamwua huyo mnyama. Tena mwanamke akimkaribia mnyama yoyote na kulala pamoja naye, mtamwuwa huyo mwanamke, na mnyama pia.” Kumbukumbu la Torati 23:17-18 “Pasiwe na kahaba katika binti za Israel, wala pasiwe na hanithi katika wana wa Israel wanaume. Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya BWANA, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yoyote; kwani hayo ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako, yote mawili.” Kuna vitu anavyovichukia BWANA vilivyo chukizo kwake. Mithali 6:16-19 “Kuna vitu sita anavyovichukia BWANA; naam viko saba vilivyo chukizo kwake. Macho ya kiburi, ulimi wa uongo,na mikono imwagayo damu isiyo na hatia, moyo uwazao mawazo mabaya; miguu iliyo myepesi kukimbilia maovu; shahidi wa uongo asemaye uongo, naye apandaye mbegu za fitina kati ya ndugu.” Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya Mungu ni uzima wa milele katika Kristo Yesu Bwana wetu kwa njia ya toba.
Kutunza uhai wa kila mwanadamu.
Amri ya tano inasema Usiue. Maana yake tusimuumize mwili wake wala kumdhulumu haki yake ila tumwokoe na kumsaidia katika shida zote. Mwanzo 9:6, “ Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na mwanadamu, maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu. Mathayo 5:21 mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, usiue, na mtu akiua, itampasa hukumu.”
· Kutunza miili yetu ; Kwa kuwa ni hekalu la Mungu.1Wakoritho 3:16 “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu”. I Wakorintho 6:19-20 “Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mlipewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu.” Warumi 12;1 “Basi ndugu zangu, na wasihi kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai takatifu ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.” Wala msifuatishe namna ya dunia hii na taama zake. Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi. Neno hili linasisitizwa kwenye I Petro 1:18-19 “Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa babu zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani ya Kristo.” Mlinunuliwa kwa thamani; msiwe watumwa wa dhambi au watumwa wa wanadamu. Mtume Paulo anafundisha kuwa Kristo ataadhimishwa katika mwili wake (Paulo) ikiwa kwa maisha yake au ikiwa kwa mauti yake. Huu ni msimamo wenye nguvu kuhusu Bwana wetu Yesu Kristo kwa maana anasema kwake yeye kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.
Kimbia mambo yote yatakayolinasi hekalu la Mungu; mambo yote ya uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sananu, uchawi, uadui; ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi na mambo yanayofanana na hayo (Wagalatia 5:19) Amri ya sita inasema Usizini. Haya yote ni machukizo kwa BWANA, Mungu wako. Tumwombe Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu wake tusiingie majaribuni. Neno la Mungu linatutaka tuitoe miili yetu iwe dhabihu iliyo hai takatifu ya kumpendeza Mungu. Pamoja na kutunza afya zetu kiroho tunatakiwa pia kutunza afya zetu kimwili kwa kula chakula kinacholeta afya njema, kufanya kazi, kupumzika na kufanya mazoezi. Mungu ameturuhusu vitu alivyoviumba viwe chakula chetu. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa , kama kikipokelewa kwa shukrani, kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu (1Timotheo 4:1-5) .Mungu alipumzika siku ya saba na Amri ya tatu inasema; Ikumbuke siku ya BWANA uitakase. Imekupasa kumwogopa Mungu na kumpenda kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.Neno la Mungu linasema, ombeni msije mkaingia majaribuni.
· Kutunza na kulinda roho yako; Ili uishi na kuenenda kwa Roho. Wagalatia 5: 22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani uvumilivu, utu wema, fadhili . uamininfu, upole, kiasi, juu ya mambo kama haya hakuna sheria”. Wokovu wa roho zetu utatokana na kukimbia mambo yote yaliyo kinyume na tunda la Roho ambayo ni machukizo mbele ya Mungu. Neno la Mungu linasema jihadharini roho zenu msije mkatenda kwa hiana. Malaki 2:15(b) “ Kwa hiyo ihadharini nafsi zenu, mtu awaye yoyote asimtende mke wa ujana wake mambo ya hiana.” Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo maana ndipo zitokako chemchem za uzima(Mithali 4:23). Tumwombe Roho Mtakatifu atufunulie siri za Mungu ili tuwe mashuhuda wa Neno lake .Neno la Mungu linatuonya kwamba siku za mwisho kutakuwa na roho zidanganyazo. 1 Timotheo 4:1-5 “Basi roho anena wazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani,wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamira zao wenyewe, wakiwazuia watu wasioe, na kuamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokelewa kwa shukrani, kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba.”
·
Kutunza na kulinda
nafsi yako ili imhimidi BWANA
Kumbukumbu la Torati 11:16 “Jitunzeni nafsi zenu, mioyo yenu isije ikadanganywa , mkageuka na kutumikia miungu mingine na kuiabudu.”. Zaburi 103:1-2 “ Ee, nafsi yangu umhimidi BWANA, Naam, vyote vilivyo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu, Ee nafsi yangu, umhimidi BWANA wala usizisahahu fadhili zake zote.” Tunaendelea kujifunza kutoka kwa mtume Paulo. Katika 1Timotheo 4:16“Jitunze nafsi yako na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia”.
2 Wathesalonike 3:6 “Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapata kwetu”. Tumwombe Mungu azifanye nafsi zetu kuwa imara na atulinde na yule mwovu, ili nafsi zetu ziwe kielelezo kwa watu wote wanaomfuata Bwana wetu Yesu Kristo.
· TOBA
Ezekieli 18:27-28 “Tena mtu mwovu atakapoghairi na kuacha uovu wake alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa hai. Kwa sababu atafakari na kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa.” Tupilieni mbali nanyi makosa yenu yote mlioyakosa,jifanyieni moyo mpya na roho mpya. Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwa lazima uzaliwe mara ya pili kwa maji na roho ili uwe kiumbe kipya na mtu wa Mungu aliye hai.
Tukitubu na kughairi maovu yetu na kutenda yaliyo halali na haki Mungu kwa msaada wa Roho Mtakatifu wake atatuwezesha kutunza uumbaji wake ambao ni msingi wa imani yetu ya Kikristo. 1Wathesalonike 5:23 “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” Amina.
· Mbingu mpya na nchi mpya.
Naomba niwakumbushe kuwa Mungu ametuahidi mbingu mpya na nchi mpya baada ya kuiangamiza dunia iliyopo sasa yenye maovu na machukizo mengi kwa BWANA. Isaya 65:17 ‘’Maana tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya na mambo ya kwanza hayatakumbukwa,wala hayataingia moyoni. Lakini furahini mshangilie daima kwa ajili ya hivi niviumbavyo, maana tazama ,naumba Yesusalemu uwe shangwe na watu wake wawe furaha .Katika mstari ule wa 22 anasema BWANA, Kama vile mbingu mpya na nchi mpya nitakazofanya zitakavyokaa mbele zangu asema BWANA ,ndivyo uzao wenu na jina lenu litakavyokaa.Waraka wa pili wa Petro 3:7, 11-14 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto kwa neno, lilohilo, zikilindwa hata siku ya hukumu na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. Basi kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu na kuihimiza ambayo katika hiyo mbingu zitafunuliwa zikiungua na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka.Lakini kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya ,ambavyo haki yakaa ndani yake,kwa hiyo wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.Ndipo mtakapofurahi sana katika BWANA nafsi zenu zitashangilia katika BWANA wenu,maana amewavika mavazi ya wokovu amewafunika mavazi ya haki kama bwana harusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi harusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu (Isaya 61:10). Roho wa Mungu anayaambia makanisa kuwa kama umelishika neno lake atakulinda utoke katika saa ya kuharibiwa iliyo tayari kuujilia ulimwengu wote. Shika sana ulicho nacho, asije mtu akaitwaa taji yako.Ufunuo 3:12 Yeye ashindaye, nitamfanya kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, wala hatatoka humo tena kabisa, nami nitaandika juu yake jina la Mungu wangu, huo Yerusalemu mpya, ushukao kutoka mbinguni kwa Mungu wangu,na jina langu mwenyewe lile jipya .Nao watamwona uso wake na jina lake litakuwa katika vipaji vya nyuso zao.Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kitu change cha enzi,kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi (Ufunuo 3:21) .Mungu wa amani mwenyewe awatakasa kabisa,nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili,bila lawama ,wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo (1 Wathesalonike 5:23).Mungu alibariki neno lake.Amina