MUNGU HUINUA MAMBO DHAIFU NA MANYONGE ILI KUAIBISHA VYENYE NGUVU
Mungu huinua vitu vinyonge au dhaifu au vilivyodharauliwa ili kuviaibisha vyenye nguvu vya dunia. Mungu anataka mwanadamu yoyote asije akajisifu mbele yake na ikiwa anaona fahari na aone fahari juu ya Bwana. Mungu anajitukuza kwa njia hii kwa kuwa yeye ndiye peke yake anayestahili kutukuzwa. 1Wakoritho 1:26-31 “Maana ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviabishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu,aliyefanywa kwetu hekima itokanayo kwa Mungu,na haki, na utakatifu, na ukombozi kusudi kama ilivyoandikwa, Yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana.” Imani yetu inatakiwa isiwe katika hekima ya mwanadamu, hekima yenye kustawisha akili za watu, bali katika nguvu za Mungu. 1-Wakorintho 3:18-19” Mtu asijidanganye mwenyewe, kama mtu akijiona kuwa mwenye hekima miongoni mwenu katika dunia hii, na awe mpumbavu, ili apate kuwa mwenye hekima. Maana hekima ya dunia hii ni upuzi mbele za Mungu”. Nguvu za Mungu hudhihirishwa kwetu kwa njia ya Roho Mtakatifu wake, maana Roho huchunguza yote hata mafumbo ya Mungu. Roho Mtakatifu atusaidie kutafsiri fumbo hili au kanuni hii ya Mungu ya kuinua vitu dhaifu na vinyonge kuaibisha vyema nguvu kwa ajili ya utukufu wake. Bwana wetu Yesu Kristo anadhihirisha fumbo hili katika Mathayo 11:25-26 “Wakati ule Yesu akajibu akasema,Nakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi,kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akilli,ukawafunulia watoto wachanga. Naam Baba, kwa kuwa ndivyo ilivyopendekeza mbele zako.” Katika neno hili Bwana wetu Yesu kristo alikuwa anaikemea miji ile ambamo ndani yake ilifanyika miujiza yake iliyo mingi, kwa sababu haikutubu (Miji ya Korazini, Bethsaida na Kapernaumu). Lakini miujiza hiyo ingelifanyika katika Tiro, Sidoni na Sadoma wangilitubu zamani kwa kuvaa magunia na majivu. Hekima ya dunia huwapendelea matajiri na kuwaonea hata kuwavunjia heshima maskini. Yakobo 2:5 “Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je! Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao.” Kwa kuwa wanasema, mimi ni tajiri, nimejitajirisha wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge na mwenye mashaka na maskini na kipofu na uchi. Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii ukatubu (Ufunuo 3:17, 19). Neno la Mungu katika Yeremia 9:23-24 “BWANA asema hivi, mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake; bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi na kunijua ya kuwa mimi ni BWANA, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi, maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema BWANA.”Mungu katika nyakati mbalimbali ametumia watu wasio na sifa, wasio na umaarufu wowote katika kutimiza kusudi lake duniani. Tunayo mifano mingi lakini katika somo hili tutatafakari mifano michache tu. Musa mchunga kondoo wa Yethro mkwewe alitokewa na malaika wa BWANA akatumwa kwa Farao ili awatoe wana wa Israel katika Misri. Musa akamwambia Mungu, mimi ni nani hata niende kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Mungu akamwambia akasema, bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe. Kama hiyo haikutosha. Musa inaendelea kumwonyesha Mungu kuwa yeye ni dhaifu katika kusema. Kutoka 4:10 “Musa akamwambia BWANA Ee Bwana, mimi si msemaji, tokea zamani, wala tokea hapo uliposema na mtumishi wako, maana mimi si mwepesi wa kusema na mtumishi wako, maana mimi si mwepesi wa kusema,na ulimi wangu ni mzito.”Mungu akampatia Musa ndugu yake aitwaye Haruni ambaye anaweza kusema vizuri. Musa huyu ambaye alijiona kuwa dhaifu Mungu alimwinua juu ya Farao, makuhani, walawi, na wazee wa Israeli. BWANA akamwambia Musa, Angalia nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyu ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. Mungu anawainua hata maskini katika utumishi wake kama alivyomwinua Gideoni ili awaokoe wana wa Israeli kutoka kwa Midiani. Waamuzi 6:14-16, 24-28” BWANA akatazama akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma? Akamwambie Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu. Bwana akamwambia hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja. Ndipo Gideoni akamjengea. BWANA madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-shalom; Hivyo Midiani walishidwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni. Mungu huwainua pia vijana wadogo ambao kwa akili na hekima za kibinadamu wasingepewa madaraka makubwa. Katika hili tunayo mifano ya nabii Yeremia na mfalme Daudi. Yeremia 1:4 “Neno la Bwana lilimjia kusema, kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa, nimekuweka kuwa nabii wa mataifa. Ndipo niliposema, Au Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema maana mimi ni mtoto. Lakini BWANA akaniambia usiseme, mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru. Usiogope kwa sababu yao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema BWANA. Angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung’oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda. Mtu mwingine ambaye Mungu alimwinua akiwa kijana mdogo hadi kuwa mfalme wa Israeli ni Daudi mwana wa Yese. Mungu alimtuma nabii Samweli kwenda nyumbani kwa Yese ili akamtie mafuta mmoja wa wanae kuwa mfalme. BWANA akamwambia Samwel, usitazame uso wake, wala urefu wa kimo chake kama waangaliavyo wanadamu; maana wanadamu huangalia sura ya nje bali BWANA huutazama moyo. Yese akawapitisha wanae saba mbele ya Samweli. Samweli akamwambia Yese, BWANA hakuwachagua hawa (1Samweli 16:1-10). 1Samweli 16;11-13 “Kisha Samweli akamwambia Yese, watoto wako wote wapo hapa? Naye akasema, amesalia mdogo wao,na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, tuma watu wamlete; Kwa maana hatutaketi hata atakapokuja huku. Basi akamtuma mtu, naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake lilikuwa la kupendeza. BWANA akasema, Ondoka umtie mafuta; maana huyo ndiye. Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya BWANA ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile.”Huyu ndiye yule Daudi ambaye akiwa na umri mdogo tu wa miaka kumi na saba (17) alipigana na kumshinda Goliathi ambaye alikuwa akiyatukana majeshi ya Israeli akitaka apewe mtu wa kupigana naye. Israeli wote waliposikia maneno hayo ya Mfilisti Goliathi; wakafadhaika wakakimbia na kuogopa sana. Daudi akajitolea kwenda kupigana na Mfilisti huyu. Mfalme Sauli akamwambia Daudi, huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe ukijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake. Daudi akasema, BWANA aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi , enenda na BWANA atakuwa pamoja nawe. Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laina matano katika kijicho cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake; akamkaribia yule Mfilisti. Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau;kwa kuwa ni kijana tu mwekundu,tena ana sura nzuri. Mfilisti akamwambia Daudi, Je! mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, wewe unanijia mimi na upanga na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana. Daudi akamwambia nitakupiga ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA,haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake (1 Samweli 17:33-50), Katika habari hii tunamwona Mungu akimwinua kijana mdogo Daudi, aliyedharauliwa, aliyekuwa na silaha zilizoonekana kwa macho ya kibinadamu kuwa dhaifu; mawe laini, fimbo na kombeo. Nguvu ya Daudi ilikuwa katika neno la BWANA kwa kujua kuwa vita ile sio yake bali ni ya BWANA. Mungu akaliaibisha jeshi la Wafilisti lililokuwa linaonekana kuwa na nguvu kwa kuwa walitegemea miungu yao. Tukimtegemea Mungu haijalishi tuko katika hali gani Yeye akiwa pamoja nasi upande wetu hakika tutashinda majaribu na vita yoyote itayoinuka juu yetu. Tuangalie mahali pengine tena ambapo Mungu aliwainua wakoma wanne juu ya jeshi kubwa lenye nguvu la Washami. 2 Wafalme 7:3-7 “Basi walikuwepo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, mbona tunakaa hapa hata tufe. Tukisema, tutaingia mjini,mjini mna njaa,nasi tutakufa humo,nasi tukikaa hapa tutakufa vilivile. Haya! Twendeni tukaliendee jeshi la Washami, wakituhifadhi hai tutaishi, wakituua, tutakufa tu. Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami, kumbe hapana mtu, kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, tazama mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti na wafalme wa Wamisiri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo wakaondoka wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vilevile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.”Katika habari hii wakoma wanatambua kuwa jambo lililofanyika kwao ni habari njema ambayo hawana budi kwenda kuwaambia watu wa nyumba ya mfalme. Neno la BWANA lililomjia Elisha ya kuwa panapo kesho saa hii kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shairi kwa shekeli, langoni pa Samaria likatimia sawasawa na neno la BWANA. Hapa tunamwona Mungu akiwainua wakoma wanne tu waliokuwa wanadharauliwa na kutengwa katika jamii za wakati ule wa Elisha wakilishinda jeshi kubwa la Washami. Mungu akalitazama neno lake na kulitimiza kwa ajili ya utukufu wa jina lake. Tukio lingine ambalo Mungu alitumia vitu dhaifu visivyo na nguvu za kivita ni katika anguko la mji wa Yeriko uliokuwa umefugwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia. BWANA akamwambia Yoshua, tazama nimeutia Yeriko katika mkono wako na mfalme wake, na mashujaa wake. Yoshua 6:20,27 “Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta, hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta, hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta, hao watu wakapiga kelele, kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji. Basi BWANA alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile . “Naye BWANA, yeye ndiye atayekutangulia, atakuwa pamoja nawe, hatakupungukia wala kukuacha; usiogope wala usifadhaike. Katika Agano Jipya tunajifunza kutoka Mathayo 23:11 “Naye aliyemkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na yeyote atakayejikweza atadhiliwa na yeyote atakayejidhili atakwezwa.” Warumi 8:31-32 “ Basi tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwapo upande wetu, ni nani aliye juu yetu? Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote, atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye.” Mtume Paulo anaendelea kutufundisha kuwa uweza wa Mungu hutimilika katika udhaifu. 2 Wakorintho 12:9-10 “Naye akamwambia, neema yangu yakutosha, maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae ndani yangu. Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.” Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu ili habari njema za ufalme wa Mungu nizitangaze kwa utimilifu katika mataifa yote watu waokolewe. Bwana atakuokoa na kila neno baya, na kukuhifadhi hata ufike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye milele na milele Amina.