• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 06 Feb, 2024
  • Admin

 

MAMBO MUHIMU KATIKA IBADA YA KIKRISTO

Ibada ya Kikristo inazo hatua muhimu kama ifuatavyo; kusifu, kuabudu, maombi na maombezi, shukrani yenye sadaka na mafundisho ya neno la Mungu. Tuanze kwa kuangalia sifa kuu za Mungu.

1.     Tumsifu Mungu wetu.

Mungu wetu anazo sifa nyingi sana wala hatuwezi kuzitaja zote hapa. Naomba nitaje sifa kuu chache.

·       Mungu ni mwenye enzi yote, muumba wa mbingu na nchi na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.

·       Mungu ni Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.

·       Mungu ni Roho yupo kila mahali wakati wote halali wala kusinzia.

·       Mungu ni mwenye upendo wa Agape, rehema, huruma, baraka, neema na fadhili nyingi.

·       Mungu ni Alfa na Omega – wa milele.

·       Asiyebadilika wala kuchoka ni yule yule jana, leo, kesho na hata milele.

·       Mungu ni Mtakatifu, mwema na mwenye haki hana upendeleo.

·       Mungu hashindwi na jambo lolote lile lililo gumu ni mwenye nguvu  na muweza wa yote.

Unapofanya maombi mtaje Mungu katika ukuu wake ukitaja sifa zake na ahadi zake.

Msifuni BWANA kwa matendo yake makuu na ya ajabu.msifuni Mungu katika patakatifu pake. Msifuni kwa kadiri ya wingi wa ukuu wake na uweza wake. Msifuni kwa kumuimbia nyimbo za sifa. Kila mwenye pumzi na amsifu BWANA. Kwa njia hii unaweza kumgusa Mungu, katika patakatifupake. Jambo linalofuata ni kumuabudu mungu wetu katika roho na kweli.

 

 

2.     Tumwabudu Mungu wetu

Ninawakaribisha wote tumwabudu Mungu wetu Zab.95:6 Njooni tumwabudu, tusujudu, tupige magoti mbele ya BWANA aliyetuumba. Kumwabudu Mungu ni kumfanyia Ibada katika Roho Mtakatifu na katika Neno lake.

Kuabudu ni hali ya kusujudu, kushuka, kunyenyekea na kumtumikia Mungu aliyetuumba.

Kwa nini tunamwabudu Mungu?

Ufunuo 4:11 “Umestahili wewe BWANA wetu na Mungu wetu kuupokea utukufu na heshima na uweza, kwa kuwa wewe ndiwe uliyeumba vitu vyote  na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa”.

Mungu anahitaji aabudiwe YEYE peke yake mchana na usiku. Mathayo 4:10“ “Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako shetani kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake”.

Namna sahihi ya kumwabudu Mungu.

Yohana 4:23-24 “Waabudio halisi watamwabudu Baba katika Roho na kweli kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu. Mungu ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika Roho na kweli”. Roho anayeongelewa hapa ni Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu akiwa ndani yetu na sisi ndani yake ndipo tutakapoweza kumwabudu Mungu katika Roho. Na kweli ni nini? Neno la Mungu ndiyo kweli Yohana 17:17 “Uwatakase kwa ile kweli, neno lako ndiyo kweli”. Ili tuweze kumwabudu Mungu katika roho na kweli tunahitajika tuombe uwepo wa Roho Mtakatifu katikati yetu na tujifunze Neno la Mungu na kulishika au kuliishi. Neno la Mungu liwe ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu. Tendo la tatu ambalo ni muhimu katika ibada ni kufanya maombi na maombezi.

 

 

3.     Maombi yetu kwa Mungu

Siku ya Ibada tunafanya maombi ambapo tunapeleka haja zetu au hoja zetu mbele ya Mungu wetu. Haja zetu zijulikane na Mungu ili tuweze kupokea yale tuliyomwomba. Hata hivyo tukiomba vibaya hatutapokea lakini tukiomba vizuri atatusikia na kutupa haja za mioyo yetu.

Tutaombaje vizuri?

·       Twende mbele za Mungu kwa unyenyekevu, heshima na upendo, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote na kwa akili zako zote.

·       Mtukuze BWANA kwa sifa za ukuu wake.

·       Omba toba na rehema kwa kuwa Mungu hapokei maombi ya mwenye dhambi kwa hiyo ungama dhambi zako zote na kuzitubu kwa kumaanisha na kuziacha (Yohana 9:31, 1Yohana 1:8-9).

·       Omba kwa jina la Yesu na damu ya Yesu. Yohana 14:13-14 “Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiniomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya”. Ihusishe damu ya Yesu katika maombi yako kwa kuwa kuna nguvu kubwa sana katika damu yake.

·       Omba nguvu ya Roho Mtakatifu. Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa”.

·       Omba sawa sawa na mapenzi ya Mungu yanayopatikana katika Neno lake (Wakolosai 3:16-17). Neno lake ndio kweli na uzima.

·       Omba kulingana na ahadi za Mungu. Maombi yako yajengwe katika ahadi za Mungu kwetu kama zinavyopatikana katika Neno lake. Kumbuka Mungu analiangalia Neno lake ili alitimize (Yeremia1:12).

·       Omba kwa bidii tena kwa kung’ang’ania usikate tamaa mpaka upate haki yako kwa wakati wa BWANA (Mwanzo 23:26 Yakobo 5:17 -18).

·       Omba kwa ajili ya watu wengine (I Timotheo 2:1-4). Wafilipi 2:4 “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine”. Hapa ndipo mahali pa kufanya maombezi kwa niaba ya watu wengine. Yaani kuyaombea mahitaji ya  wengine au ya nchi kwa Mungu.        

 

·       Wasamehe wote waliokukosea ili na Mungu akusamehe dhambi zako. Mathayo 6:14-15 “Kwa maana mkiwasamehe watu makosa yao, na Baba yenu wa Mbinguni atawasamehe ninyi. Bali msipowasamehe watu makosa yao wala Baba yenu hatawasamehe ninyi makosa yenu”.

·       Omba kwa Imani. Waebrania 11:1 “Basi Imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo ni bayana ya mambo yasiyoonekana.”

Ni maombi yangu kuwa tafakari hii itusaidie kuomba vizuri ili tuweze kupokea yale tunayoyaomba yawe yetu. Amani ya Bwana wetu Yesu Kristo ikae nasi sote sasa na hata milele.

Hatua nyingine muhimu sana katika ibada yoyote ile ya Kikristo ni kumshukuru Mungu wetu.

4.     Tumshukuru Mungu wetu

Kumshukuru Mungu ni kumuelezea jinsi tunavyomthamini, tunavyomtegemea na kumtumainia, tunavyomheshimu na kumpenda kwa wema wake, fadhili zake na baraka zake kwetu.

·       Tunamshukuru Mungu aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni, katika ulimwengu wa roho, ndani ya Bwana wetu Yesu Kristo, ili audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu.

·       Tunamshukuru Mungu kwa vinywa vyetu, mioyo yetu na matendo yetu (Zaburi 9:1-2).

·       “Nitamkushuru BWANA kwa moyo wangu wote; nitayasimulia matendo yake yote ya ajabu. Nitafurahi na kukushangilia wewe; nitaliimbia jina lako wewe Uliye juu.

·       Tunamshukuru Mungu kwa wema wake na fadhili zake kwetu.

Zab. 136:1-3 “Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele”. Mshukuruni Mungu wa miungu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Mshukuruni Bwana wa mabwana; kwa maana fadhili zake ni za milele.

·       Kumshukuru Mungu ni jambo jema kwa wateule wake Kristo (Wakolosai 3:15). Ni neno jema kumshukuru BWANA, na kuliimbia jina lako, Ee Uliye juu. Kuzingatia rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku (Zab. 92: 1-2).

·       Tunatakiwa tudumu katika kumshukuru Mungu bila kukoma (Wakolosai 4:2 na (Wathesalonike 2:13,­ 5:18). Mungu anatutaka tushukuru kwa kila jambo maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwetu katika Kristo Yesu,

·       Tujifunze kushukuru hata kabla ya kupokea kutoka kwa Mungu. Tushukuru kwa imani kwamba jambo tuliloliomba kwa Mungu tayari limetendeka kwenye ulimwengu wa roho na kwamba litatimia kwenye ulimwengu wa mwili.      

Tunao mfano mzuri sana wa Bwana wetu Yesu Kristo siku ile alipotwaa ile mikate 5 na samaki 2 alishukuru kabla muujiza ule haujatokea (Marko 6:41).

·       Tunakamilisha shukrani zetu kwa Mungu kwa kumtolea sadaka. Tumuombe Mungu azikubali na kuzitakabali sadaka zetu ziwe harufu ya manukato ya kumpendeza.

Ibada haiwezi kukamilika kama haina mafundisho ya neno la Mungu.

 

5.     Mafundisho ya Neno la Mungu

Mafundisho ya neno la Mungu ni muhimu kwa kila mtu kwa kuwa neno la Mungu ni mamlaka kwa kile tunachokiamini kuhusu Mungu na kile ambacho amefanya, anachofanya na atakachofanya hapa duniani na katika ulimwengu ujao. Neno la Mungu ni ujumbe wa Mungu kwa kila mwanadamu wenye pumzi ya Mungu unaotuelekeza jinsi ya kuishi hapa duniani tukimpendeza Mungu na wanadamu. 2 Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu,lafaa kwa mafundisho na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki”. Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu, hutumulikia kila tuendapo mchana na usiku. Tunatakiwa tuliweke neno la Mungu mioyoni mwetu na lisiondoke vinywani mwetu.

·       Yesu Kristo ndiye Neno aliyekuwepo hapo mwanzo wakati wa kuumbwa kwa mbingu na nchi. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu (Yohana 1:1-5). Yohana alimuona Yesu Kristo amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu (Ufunuo 19:13). Hivyo ukiyashika maneno  na mafundisho ya Yesu Kristo, basi umelishika neno la Mungu. Ukiyashika maagizo ya Yesu Kristo basi umeyashika maagizo ya neno la Mungu. Wakolosai 3:16 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu”. Yesu Kristo anakiri wazi wazi kuwa neno wanalolisikia sio lake ila ni la Baba aliyempeleka ( Yohana 14:24). Tena anasema, afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika na kulifanya maana hao watakuwa ndugu zake na kisha watamzalia matunda kwa kuvumilia.

·       Neno la Mungu lina nguvu nyingi sana lakini hapa nitaelezea mambo machache kati ya hayo. Waebrania 4:12 “Maana neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi  kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”.

Yohana 14:6 Neno la Mungu lina nguvu na uwezo wa kukuongoza katika njia ya uzima tena ni chakula cha uzima.

“Yesu (Neno) akamwambia mimi ndimi njia, na kweli na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, imeandikwa, mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Neno la Mungu lina nguvu ya kutupa ujasiri na ushujaa. Yoshua 1:6-7 Mungu anamwambia Yoshua uwe hodari na moyo wa ushujaa, uwe hodari tu na ushujaa mwingi. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, usiogope wala usifadhaike, kwa kuwa BWANA Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendapo. Mitume wa Bwana Yesu Kristo nao walikuwa na ujasiri mwingi katika kuhubiri Habari njema(Injili ya Yesu Kristo).

Neno la Mungu lina nguvu ya kuumba. Waebrani 11:3 “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu”.  Neno la Mungu lina nguvu ya kuponya. Mathayo 8:8,13 Yule akida aliyekwenda kumwomba Yesu amponye mtumishi wake ugonjwa wa kupooza alimwambia Yesu sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Naye Yesu akamwambia yule akida, nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini, mtumishi wake akapona saa ile ile.

Neno la Mungu lina nguvu ya kumshinda shetani. Waefeso 6:17 “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa roho ambao ni neno la Mungu.

Tukimwamini Yesu Kristo na kulishika neno lake tunaweza kupata nguvu zinazopatikana katika Neno la Mungu na kufanya kazi alizozifanya BWANA wetu Yesu KRISTO na kubwa kuliko alizofanya. Yohana 14:12 “Amin, amin, nawaambieni, yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba”.

Mwenyezi Mungu na alibariki neno lake, lijae kwa wingi katika moyo wako na kinywani mwako.

HITIMISHO

Katika Ibada zetu tuendelee kutafakari sifa za ukuu wa Mungu, ili tumwabudu katika roho na kweli. Tutafakari wakati wote namna nzuri ya kufanya maombi na shukrani. Msifu BWANA kwa matendo yake makuu, mwabudu BWANA kwa uzuri wake. Mshukuru kwa kuwa ni mwema na fadhili zake ni za milele.


Share This