MAFUNDISHO YA NENO LA MUNGU
Mafundisho ya neno la Mungu ni muhimu kwa kila mtu kwa kuwa neno la Mungu ni mamlaka kwa kile tunachokiamini kuhusu Mungu na kile ambacho amefanya, anachofanya na atakachofanya hapa duniani na katika ulimwengu ujao. Neno la Mungu ni ujumbe wa Mungu kwa kila mwanadamu wenye pumzi ya Mungu unaotuelekeza jinsi ya kuishi hapa duniani tukimpendeza Mungu na wanadamu. 2 Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu,lafaa kwa mafundisho na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki”. Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu, hutumulikia kila tuendapo mchana na usiku. Tunatakiwa tuliweke neno la Mungu mioyoni mwetu na lisiondoke vinywani mwetu.
· Yesu Kristo ndiye Neno aliyekuwepo hapo mwanzo wakati wa kuumbwa kwa mbingu na nchi. Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu (Yohana 1:1-5). Yohana alimuona Yesu Kristo amevikwa vazi lilichovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu (Ufunuo 19:13). Hivyo ukiyashika maneno na mafundisho ya Yesu Kristo, basi umelishika neno la Mungu. Ukiyashika maagizo ya Yesu Kristo basi umeyashika maagizo ya neno la Mungu. Wakolosai 3:16 “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu”. Yesu Kristo anakiri wazi wazi kuwa neno wanalolisikia sio lake ila ni la Baba aliyempeleka (Yohana 14:24). Tena anasema, afadhali, heri walisikiao neno la Mungu na kulishika na kulifanya maana hao watakuwa ndugu zake na kisha watamzalia matunda kwa kuvumilia.
· Neno la Mungu lina nguvu nyingi sana lakini hapa nitaelezea mambo machache kati ya hayo Waebrania 4:12 “Maana neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo”.
Yohana
14:6 Neno la Mungu lina nguvu na uwezo wa kukuongoza katika njia ya uzima tena ni chakula cha uzima.
“Yesu (Neno) akamwambia mimi ndimi njia, na kweli na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Mathayo 4:4 “Naye akajibu akasema, imeandikwa, mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu. Neno la Mungu lina nguvu ya kutupa ujasiri na ushujaa. Yoshua 1:6-7 Mungu anamwambia Yoshua uwe hodari na moyo wa ushujaa, uwe hodari tu na ushujaa mwingi. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, usiogope wala usifadhaike, kwa kuwa BWANA Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendapo. Mitume wa Bwana Yesu Kristo nao walikuwa na ujasiri mwingi katika kuhibiri Habari njema.
Neno la Mungu lina nguvu ya kuumba. Waebrani 11:3 “Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu”. Neno la Mungu lina nguvu ya kuponya. Mathayo 8:8,13 Yule akida aliyekwenda kuwomba Yesu amponye mtum9ishi wake ugonjwa wa kupooza alimwambia Yesu sema neno tu, na mtumishi wangu atapona. Naye Yesu akamwambia yule akida, nenda zako; na iwe kwako kama ulivyoamini, mtumishi wake akapona saa ile ile.
Neno la Mungu lina nguvu ya kumshinda shetani. Waefeso 6:17 “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga waroho ambao ni neno la Mungu.
Tukimwamini Yesu Kristo na kulishika neno lake tunaweza kupata nguvu zinazopatikana katika Neno la Mungu na kufanya kazi alizozifanya BWANA wetu Yesu KRISTO na kubwa kuliko alizofanya. Yohana 14:12 “Amin, amin, nawaambieni, yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya, naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwakuwa mimi naenda kwa Baba”.
Mwenyezi Mungu na alibaliki neno lake, lijae kwa wingi katika moyo wako na kinywani mwako.