• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

TUNAMSHUKURU MUNGU KWA MAFANIKIO MAKUBWA YALIYOPATIKANA KATIKA ELIMU.

Tunamshukuru Mungu kwa neema kubwa mno aliyompa mzee wetu Shaidi Nziamwe Mkaza kupokea mafundisho ya neno la Mungu na kukubali kubatizwa na kuwa mfuasi wa Yesu Kristo Bwana wetu. Mzee Shaidi Nziamwe na mkewe Kompeho Msangi Narundu walibatizwa tarehe 25 Oktoba 1914 katika usharika wa Vudee. Mzee Shaidi alipata elimu na mafunzo ya uashi kutoka kwa wamissionari wa Kijerumani wa chama cha mission cha Leipzig chini ya uongozi wa Mch. Michel mwaka 1911 na baadaye mwaka 1925 – 1933 chini Mch. Steimer na Mch. Gruth. Mzee Shaidi Nziamwe hakumwacha elimu aende zake bali aliwasomesha watoto wake wote wa kiume na wakike. Wazee wenzake wa wakati wake walimcheka na kumshangaa kwa vile vijana wa kiume walihitajika katika kazi za kuchunga mifugo. Vijana wa kike waliandaliwa kwa ajili ya kuolewa na kuipatia familia mahari. Mifugo ya mzee Shaidi Nziamwe ilikosa wafugaji kwa kuwa wafugaji kwa maana ya watoto wake walikuwa mashuleni na vyuoni. Watoto wa Shaidi Nziamwe walisoma na kupata elemu na kushika nyadhifu mbalimbali katika Kanisa; Serikali na jamii kwa ujumla. Matokeo ya maono haya ya mzee Shaidi Nziamwe tunayaona hata leo hii kwa wajuu, vitukuu na vilembwe. Tuseme nini kama sio kumshukuru Mungu kwa neema hii kubwa mno. Tumwombe Mungu elimu katika uzao wetu itusaidie kupata akili, ujuzi na maarifa katika kumtumikia (Mungu). Akili tutakazopewa na tulizopewa zimsaidie kila mmoja wetu kumpenda Bwana Mungu wetu kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote na kwa akili zake zote, na kwa nguvu zake zote. Tunamwomba Mungu atufunulie akili zetu tupate kuelewa na maandiko na atupe akili katika mambo yote. Tuombe kwa akili na tuimbe kwa akili pia. Elimu itusaidie kupata ujuzi katika kazi tunazozifanya. Mungu atuite na sisi na uzao wetu kama alivyomwita Bezaleli katika Kutoka 35:31 “naye amemjaza (Bazaleli) roho ya Mungu katika hekima na maarifa na ujuzi na kazi ya ustadi wa kila aina”. Tunamwomba Mungu aujaze uzao wetu akili za moyoni ili tutumike katika kazi za ubunifu na uvumbuzi wa kila aina kwa utukufu wa Jina Lake. Atujaze Roho Mtakatifu wake, katika hekima na maarifa ili tusije kuangamia kwa kukosa maarifa. Roho Mtakatifu mwalimu mwema utufundishe yote na kutukumbusha yote Bwana wetu Yesu Kristo aliyotuambia, utuongoza na kututia kwenye kweli yote, katika jina la Mungu wa utatu (Baba na Mwana na Roho Mtakatifu). Amen.

Share This