TUNAKATAA NA KUYAFUTA MANENO YOTE MABAYA YALIYOSEMWA KUHUSU UZAO WETU.
Tunamshukuru Mungu kwa matendo yake makuu na ya ajabu aliyotutendea na anayotutendea wakati wote wa miasha yetu. Tukaokolewa na watu wasio haki, wabaya, maana si wote walio na imani (2 Wathesalonike 3:2). Watu hawa ambao tunaweza kuwaita watesi wetu waliinuka na kusema maneno mabaya juu ya uzao wetu wakisukumwa na chuki, wivu na hasira. Kando ya maneno mabaya yaliyosemwa na watu hawa hata sisi wenyewe wakati mwingine tumejinenea maneno mabaya na wakati mwingine tumewanenea watu wengine na ndugu zetu. Wakati wa mababu zetu kuna maneno mabaya yaliyosemwa na watesi wa mzee Shaidi Nziamwe Mkaza. Mama mmoja akasema kwa hasira kubwa kuwa wana wa uzao wa Shaidi watazikwa hadi Magemo. Kutoka nyumbani kwa mzee Shaidi hadi eneo linaloitwa Magemo kuna umbali wa kilomita kama nne (4). Mzee mmoja naye akasema kwa chuki kumbe huu uzao wa mbari ya Mkaza bado upo duniani hadi leo? Na mwingine akasema atauharibu uzao wa mzee Shaidi akilenga kuharibu watoto wake.Mzee Shaidi alienda kumshitaki mzee huyo katika mahakama ya mwanzo – Kisiwani. Sisi hatuendi mahakamani bali tunakwenda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tunakwenda na wazee wetu, vijana wetu, watoto wetu, wakwe zetu na wajukuu, vitukuu na vilembwe wa uzao wa Shaidi pamoja na sadaka zetu kwa kuwa inatupasa kumfanyia BWANA sikukuu. Tunakwenda kumshukuru na kumtolea sadaka za shukrani kwa kutuokoa na watesi wetu, watu wasio haki, wabaya na wasio na imani. Tunamatumaini kwa kuwa Bwana ni mwaminifu atakayetufanya imara na kutulinda na yule mwovu shetani. Kwa nguvu zake tutawaangusha watesi wetu; kwa jina lake tutawakanyaga watupingao. Wewe ndiwe uliyetuokoa na watesi wetu; na watuchukiao umewaabisha. Tunakataa na kufuta maneno yote mabaya tuliyonenewa au kuwanenea au kujinenea wenyewe kwa damu ya Yesu na Jina la Yesu. Tutamshinda shetani muuaji, mwizi na mharibifu kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda wetu. Ushindi huu unapatikana kwa wale ambao hawakupenda maisha yao hata kufa, wale ambao wamefua mavazi yao na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo. Je mimi na wewe ndugu yangu tumeshafua mavazi yetu katika damu ya Mwanakondoo? Je tunalo neno gani la ushuhuda? Twende mbele za BWANA sio kwa sadaka tu za shukrani bali kwa kuomba Toba na Rehema. 1 Yohana 1:9 “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote”. Mungu mwenye rehema na fadhili nyingi aturehemu na atuhurumie sisi wakosefu. Na jina lake tutalishukukuru milele.