NGUVU YA NENO LA SHUKRANI KWA MUNGU.
UTANGULIZI.
Mungu huguswa sana tunaposhukuru kwa moyo wa unyenyekevu, Mungu anatutendea mambo mengi sana lakini tunashindwa kurudisha shukurani ipasavyo. Unatakiwa kurejea mbele za BWANA kwa kushukuru kwa moyo wako wote . Hata kabla Mungu hajakutendea jambo ukaliona kwa macho haya ya nyama tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa lile tulilolimba kwa Imani kuwa atatenda kwa majira yake. Ibada ya kweli ya shukrani huanzia moyoni na kuishia katika matendo. Neno la Mungu linasema tushukuru kwa kila jambo. Wathesalonike 5: 18 “Shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu; Msijisumbue kwa neno lolote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru haja zenu zijulikane na Mungu (Wafilipi 4: 6). Shukrani zetu zimpe BWANA utukufu. Tunakushukuru Mungu kwa ajili ya utukufu wako mkuu juu mibnguni na duniani. Ikiwa umekusudia kumshukuru Mungu, basi jitahidi kuandaa sadaka yako ya shukrani. Ni jambo jema sana maombi yako ya shukrani kuyasindikiza na sadaka. Shukuru kwa kwa moyo wa ukunjufu mbele za uso wa Mungu. Zaburi 9:1 “Nitamshukuru BWANA kwa moyo wangu wote, nitayasimulia matendo yako yote ya ajabu, nitafurahi na kukushangilia wewe, nitaliimbia jina lako, wewe ulie juu”. Mtoleeni Mungu dhabihu za kushukuru, mtimizie aliye juu nadhiri zako.
1.0 Shukrani ina nguvu ya wokovu.
Neno la Mungu katika Mathayo 26:27 “Akakitwaa kikombe, akasukuru, akawapa akisema, Nyweni nyote katika hiki kwa maana hii ndio damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi “. Katika wale wakoma kumi waliomba uponyaji kwa Bwana Yesu ni mmoja tu aliyerudi kumshukuru.Bwana Yesu akamsamehe dhambi zake na kumtangazia wokovu. Luka 17: 15- 19 “Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu, akaanguka kifudifudi miguuni pake akamshukuru; naye alikua Msamaria, Akamwambia Inuka, enenda zako, Imani yako imekuokoa. Msamaria huyu amepata uponyaji wa mwili na roho lakini wale kenda ambao hawakurudi kushukuru wamepata uponyaji wa mwili tu.Wakristo tunatakiwa kutoa shukrani kwa Mungu kwa kuwa hiyo ndiyo shukrani ya wokovu wetu.
2.0 Shukrani ina nguvu ya kuongeza au kuzidisha kile ulichonacho.
Yesu Kristo katika neno lake anatufundisha kuwa tushukuru kwanza kwa kile kidogo tulichonacho kabla ya kuhitaji kikubwa zaidi. Kidogo kwako wewe kwake kitazidi, Yeye anao uwezo wa kuongeza akiba yako. Mathayo 15:33-39 “Wanafunzi wake wakamwambia, (Yesu) Tupate wapi mikate mingi hapa nyikani, hata kushibisha mkutano mkuu namna hii? Yesu akawaambia, mnayo mikate mingapi? wakasema saba, na visamaki vichache. Akawaambia mkutano wakati chini; akatwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega, akawapa wanafunzi wake nao wanafunzi wakawapa makutano.Wakala wote wakashiba ;wakayaokota masazo ya vipande vya mikate makanda saba yamejaa . Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila ya wanawake na watoto.Neno hili linatukumusha tumshukuru Mungu kabla ya kuanza kula chakula naye atatushibisha na kusaza. Tumshukuru Mungu kwa kila jambo.
3.0 Shukrani ina nguvu ya kufufua mambo yako yaliyokufa kimwili na kiroho.
Lazaro alikuwa maiti kaburini siku nne Yesu alipofika na kumfufua. Yohana 11:41-44 “Basi wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema Baba Nakushukuru kwa kuwa umenisikia. Naye akaiisha kusema hayo, akalia kwa sauti kuu Lazaro njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa, amefungwa sanda miguuni na mikononi, na uso wake amefungwa leso. Naye Yesu akawaambia, mfungueni, mkamwacha aende zake. Hata leo hii Bwana wetu Yesu Kristo anaweza kufufua mambo yako yaliyokufa. Katika maisha tunayoishi hapa duniani, kuna vitu vingi vinaweza kufa. Kwa mfano, biashara, elimu, ndoa, au viungo vya mwili wako. Unaweza pia kufa kiroho.Mtu ambaye hana Roho Mtakatifu ndani yake, huyo amekufa kiroho, ni mfu kwa sababu hana uzima wa milele ndani yake. Dawa ya kufufuka katika hali ya ufu ni kwa njia ya kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na Mwokozi wa maisha yako, yaani kuokoka. Ni kufanya toba ya kweli kuacha dhambi na kumgeukia Mungu. Bwana akiisha tufufua kiroho na kuvifufua vitu vyetu vilivyokufa hatuna budi kumshukuru na kumwimbia kama mfalme Daudi.Zaburi 100:4-5 “Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; nyuani mwake kwa kusifu, Mshukuruni, lihimidini jina lake. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema, rehema zake ni za milele; Na uaminifu wake wa vizazi na vizazi. Mungu na ashukuriwe atupaye kushinda kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Tushangilie ushindi wetu juu ya vitu vyetu vilivyokufa kwa kumpatia Mungu shukrani kwa vizazi vyetu vyote. Tumpe Mungu roho zetu zilizo dhaifu ili azikamilishe. Damu aliyotoa, ndiyo itoshaji, kuosha wakosaji hata wewe vivyo.Ninakushukuru Mungu kwa upendo huu na ninakupa moyo wangu. Uniumbie moyo safi maana heri mwenye moyo safi maana hao watamwona Mungu. Neema ya Mungu iokoayo ikuponye katika madhaifu yako yote.
4.0 Sadaka ya shukrani inakupa kibali mbele za BWANA yaani kukubaliwa.
Katika kitabu cha Mambo ya Walawi 22:29 Mungu anasema “Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya shukrani, mtachinja ili mpate kukubaliwa”. Sadaka ya shukrani itolewayo sawa sawa na mapenzi ya Mungu ni manukato mbele ya Mungu ndiyo impendezayo. Ni sadaka yenye kibali; “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo yesu” (Wakolosai 4:19). Sauti zao waletao shukrani nyumbani mwa BWANA zitakaposikiwa ataibariki nchi yao.Yeremia 33:11 “Itasikilikana tena sauti ya furaha na sauti ya shangwe , sauti ya bwana harusi na sauti ya bibi harusi, sauti yao wasemao Mshukuruni BWANA wa majeshi, maana BWANA ni mwema, rehema zake ni za milele, na sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani kwa BWANA.Kwa kuwa nitawarudisha wafungwa wa nchi hii kama kwanza asema BWANA”. Unapotoa sadaka yako ya shukrani kwa Mungu kumbuka kuomba kibali chake katika kila eneo la maisha yako ili uweze kufanikiwa na kustawi. Sadaka yako ipate kibali baada ya kutakaswa na Roho Mtakatifu. Mungu akitumie kibali hicho kwa utukufu wa Jina lake.1 Petro 5: “Basi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake;huku mkimtwika fadhaa zenu zote, kwa maana yeye hujishugulisha sana kwa mambo yenu”.Mshukuru Mungu wa mbinguni; kwa maana fadhili zake ni za milele. Uweza una yeye hata milele na milele. Amina.