• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 22 Aug, 2023
  • Admin

Katika somo hili tutatafakari namna ya kuomba inayompendeza Mungu. Lengo la somo sio aina ya maombi bali ni kwa namna gani tunaweza kufanya maombi yanayompendeza na yeye kutujibu maombi yetu.  Maombi ni tamko la hitaji au tamanio la moyo wako ambalo wewe mwenyewe huweza kujitosheleza, hivyo unahitaji msaada kutoka kwa Mungu.Maombi ni njia ya   kumjulisha Mungu haja za moyo na ni njia ambayo Mungu ametupa ya kuweza kuongea naye au kusemezana naye. Katika neno lake anasema kuwa tumwombe naye atasikia kuomba kwetu. Katika vipengere  tutakavyovitafakari katika somo hili ni pamoja na;

  • ·       Kuomba kwa jina la Yesu kwa msaada wa Roho Mtakatifu
  • ·       Kuomba kwa Imani
  • ·       Kuomba Toba na Utakaso
  • ·       Kuomba kwa unyenyekevu
  • ·       Kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu
  • ·       Kuomba kwa juhudi na bidii bila kukoma
  • ·       Kuomba kwa kuzitaja ahadi za Mungu

 

  • ·       Kuomba kwa jina la Yesu kwa msaada wa Roho Mtakatifu.

Tunapoomba ni lazima tujue kuwa tunamwomba Baba yetu aliyembinguni .Tuonyeshe utukufu na ukuu alionao Mungu tunayemuomba. Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana, Mungu wa miungu, Bwana Mungu wa majeshi aliyeumba mbingu na nchi na vitu vyote vilivyomo vinavyoonekana na visivyoonekana .Mkono wake una nguvu na uweza, usioshindwa na jambo lolote lile.Wewe peke yako ndiwe unayestahili heshima, sifa , utukufu na enzi kwa kuwa hivi vyakustahili wewe peke yako .Tunakuomba utege sikio lako utusikie, fungua macho yako utuone, uyasikie maombi ya watoto wako walioitwa kwa jina lako. Tutaje  Jina lake na sifa zake zinazoonyesha ukuu wake.Tukiomba neno lolote mbele ya uso wake kwa heshima kwa kutumia jina la Yesu atasikia kuomba kwetu na atafanya au atatupa kwa ajili ya utukufu wa jina lake.Yohana 14:13 “ Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu , hilo nitalifanya , ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana”.  Yesu Kristo mwenyewe anasisitiza neno hili katika Yohana Mtakatifu 16:23-24. “Tena siku ile hamtaniuliza neno lolote. Amin, amin nawaambia , mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu.Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu, ombeni nanyi mtapata, furaha yenu iwe timilifu.”   Mungu akamkirimia jina lipitalo majina yote mbinguni na duniani kwa ajili ya utukufu wa Mungu Baba.Wafilipi 2:9-11 “ Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina, ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni na vya duniani , na vya chini ya nchi na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa Mungu Baba. “Jina la Yesu lina mamlaka na nguvu mbinguni hata duniani,na katika ulimwengu ujao. Waefeso 1:21-23 Mungu akamweka “ juu sana kuliko ufalme wote na mamlaka na nguvu na usultani na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini  ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote.” Yesu Kristo amefanyika bora kupita malaika , kwa kadri ya jina alilolirithi lilivyo tukufu kuliko lao (Waebrania 1:4).Huyu ndiye Yesu Kristo Mnazareti Mwana wa Mungu ambaye tunatakiwa kuomba kwa jina lake hata tukiwa zaidi ya mtu mmoja.Mathayo 18:19-20 “ Tena nawaambia ya kwamba wawili wenu watakapokutana duniani katika jambo lolote watakaloomba , watafanyiwa na Baba yangu aliye mbinguni.Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami  nipo papo hapo katikati yao.” Katika Yohana Mtakatifu 15:16 Yesu Kristo anasema , “ Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi, nami nikawaweka mwende mkazae matunda , na matunda  yenu yapate kukaa; ili kwamba lolote mumwombalo. Baba kwa jina langu awapeni” Mungu atatusikia tukimwomba kwa jina la Mwanae Yesu Kristo kwa kuwa huyu ni mwanae mpendwa anayependezwa naye. Yesu Kristo kwa upendo wake ulio mkuu sana kwetu ametukirimia Roho Mtakatifu wake ili atusaidie kuomba kwa kuwa hatujui kuomba itupasavyo. Warumi 8:26 “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu,  kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Unapoomba mkaribishe Roho  Mtakatifu akufundishe na akuongoze katika maombi yako ili yampendeze Mungu na upate kibali katika jambo unaloliombea. Yohana 14:26 “Lakini huyu Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu ambaye Baba atampeleka kwa jina langu,atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.” Tukiwa na Roho Mtakatifu ndani yetu atatufundisha kuomba katika kweli na roho. Yohana 14:16-17 “Nami nitamwomba Baba naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.” Kwa kuwa wote wanaoongozwa na roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu.

 

  • ·       Kuomba kwa imani.

Mungu anapendezwa na kufurahishwa tunapoomba kwa imani naye husikia kuomba kwetu na kutujibu.Kuomba kwa imani ni kuamini bila shaka yoyote kuwa ulichokiomba umeshakipokea.Imani ya kweli ni kwamba Mungu tayari ametimiza matakwa yako. Waebrania 11:1” Basi imani ni kuwa na hakika ya mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.  Katika Injili ya Marko 11:22-24 neno la Mungu linasema, “Yesu akajibu akamwambia mwamini Mungu. Amin nawaambia, yeyote atakayeuambia mlima huu, ng’oka ukatupwe baharini wala asione shaka  moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametokea yatakuwa yake, kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini  ya kwamba  mnayapokea, nayo yatakuwa yenu” Mungu anapendezwa na maombi yanayofanywa kwa imani. Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza, kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Neno la Mungu linatufundisha kuwa” Na yoyote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea” (Mathayo 21:22). Katika Waraka wa Yakobo 1:5-7 neno la Mungu linasema “Lakini mtu wa kwenu akipungukiwa hekima, na aombe dua kwa Mungu awapaye wote kwa ukarimu, wala hakemei  naye atapewa. Ila na aombe kwa imani pasipo shaka yoyote , maana mwenye shaka ni kama wimbi la bahari lililochukuliwa na upepo na kupeperushwa huku na huku. Maana mtu kama huyo asidhani atapokea kitu kwa Bwana.” Kuomba kwa imani kunaweza kumwokoa mgonjwa na Bwana akamwinua hata ikiwa amefanya dhambi.Mfano mzuri wa jambo hili ni yule akida aliyemjia Bwana Yesu akamwomba amponye mtumishi wake ugonjwa wa kupooza. Yesu alipoona imani ya akida yule akasema , “ Amin nawaambieni sijaona imani kubwa namna hii kwa yeyote katika Israeli naye Yesu akamwambia yule akida nenda zako na iwe kwako kama  ulivyoamini.Mtumishi wake akapona saa ile ile (Mathayo 8:5-13).Katika Biblia wako watu wengi walioponywa kutokana na imani zao. Yule binti aliyetokwa damu miaka kumi na miwili aligusa upindo wa vazi la Yesu akiamini kuwa utapona.Yesu akamwambia imani yako imekuponya.Yule mwanamke akapona tangu saa ile (Mathayo 9:20-22). Yesu aliwaponya vipofu wawili walipoamini kuwa anaweza kuwaponya. Ndipo alipowagusa macho akasema, kwa kadri ya imani yenu mpate.Macho yao yakufumbuka (Mathayo 9:27-30) .Hii ni mifano michache tu ya imani iokoayo. Ili nguvu hii ya uponyaji ifanye kazi ndani yetu tunatakiwa tuungame dhambi zetu na kuombeana. 

  • ·       Kuomba Toba na Utakaso.

Mungu anapendezwa na watu wanaomwomba wakiwa wamekwisha tubu dhambi zao na kutakaswa mioyo yao kwa damu ya Mwana – Kondoo , Yesu Kristo Bwana wetu. Kuomba msamaha wa dhambi ni jambo la lazima kwa mwanadamu yoyote yule lakini pia katika maombi yako jifunze kuunganisha na kuomba kutakaswa .Zaburi 51:1-2 “Ee Mungu, unirehemu, sawasawa na fadhili zako, kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, unitakase dhambi zangu” Ee Mungu, uniumbie moyo safi. Kujitakasa kunakuja baada ya kuomba toba mbele za Mungu tukimwomba atuhurumie na kuturehemu sisi wakosaji.  Ufanye toba kwanza ili uwe na mahusiano mazuri na Mungu wako. Mungu anasema maombi ya mwenye dhambi ni kelele mbele zake na maombi ya mwenye haki ni kama manukato .Mithali 15:8, 29 “ Sadaka ya mtu mbaya ni chukizo kwa BWANA, bali maombi ya mtu mnyofu ni furaha yake. BWANA yu mbali na wasio haki,bali huisikia sala ya mwenye haki.” Macho ya BWANA huwaelekea wenye haki na masikio yake hukielekea kilio chao.Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi , bali mtu akiwa mcha Mungu na kuyafanya mapenzi yake, humsikia huyo (Yohana 9:31) .Kwa kuwa wote tumetenda dhambi tunatakiwa kutubu dhambi zetu zote. 1Yohana 1:8-10 “Tukisema kwamba hatuna dhambi twajidanganya wenyewe wala kweli haimo mwetu”. Tukiziungama dhambi zetu. Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu na kutusafisha na udhalimu wote.Tukisema kwamba hatukutenda dhambi twamfanya yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu” Tukiisha kutubu dhambi zetu neno la Mungu linasema kuwa lolote tuombalo twalipokea kwake,kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. Baada ya toba Mungu anataka tumkaribie kwa utakaso, ili tuwe watakatifu kama yeye alivyo mtakatifu. Yakobo 4:8 “Mkaribieni Mungu naye atawakaribia ninyi.Itakaseni mikono yenu enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu enyi wenye nia mbili.” Tunatakaswa na Mungu mwenyewe kupitia damu ya mwanaye Yesu Kristo Bwana wetu. 1 Wathesolonike 5:23-24 “ Mungu wa amani  mwenyewe awatakase kabisa , nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya. “Katika mapenzi hayo mmepata utakaso , kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu(Waebrania 10:10). Kama vile Mungu Baba alivyotangulia kuwajua katika kutakaswa  na  Roho, hata mkapata kutii na kununyiziwa damu ya Yesu Kristo (1Petro 1:2). Wakati tunaomba toba na utakaso tukumbuke kuwasamehe ndugu zetu na watu wengine wote waliotukosea ili na sisi Mungu atusamehe dhambi zetu. Marko11:25-26 “Nanyi kila msimamapo na kusali, sameheni mkiwa na neno juu ya mtu, ili Baba yenu aliye mbinguni awasamehe na ninyi makosa yenu. Lakini kama ninyi hamsamehe wala Baba yenu aliye mbinguni hatawasamehe ninyi makosa yenu”. Kuhusu kusamehe ndugu neno la Mungu linasisitiza kuwa heri uiache sadaka yako madhabahuni uende ukapatane kwanza na ndugu yako, ndio uje utoe sadaka yako.

Mathayo 5:23-24 “Basi ukileta sadaka yako madhabahuni na huku ukikumbuka ya kuwa ndugu yako ana neno juu yako, iache     sadaka yako mbele ya madhabahu uende zako. Upatane kwanza na ndugu yako, kisha urudi uitoe sadaka yako. “Patana na mshitaki wako upesi tena waombeeni adui zenu. Mathayo     5:43 -44 “Mmesikia kwamba imenenwa umpende jirani yako na umchukie adui yako; lakini mimi (Yesu Kristo) nawaambia wapendeni adui zenu waombeeni  wanaowaudhi” Kuwaombea kwetu msamaha na sisi wenyewe kuwasamehe ndugu, majirani na watu wote, maombi hayo yafanyike kwa unyenyekevu mkubwa.   

 

  • ·       Kuomba kwa Unyenyekevu

Uyenyekevu ni hali ya ndani ya moyo wa mtu. hali ya mtu kujishusha, hali ya kutojisifu au kujiona kuwa ni bora  kuliko wenzako.Hali ya kujiona maskini pamoja  na kuwa wewe ni tayari. Bwana Yesu anawaita watu wa namna hii maskini wa roho ambao amesema ufalme wa mbinguni ni wao. Kinyume cha unyenyekevu ni kiburi, kujiona, kujisifu, jeuri,dharau, kujivuna au kujigamba.Mungu anapendezwa na mtu anaemwendea  kwa maombi akiwa na moyo wa unyenyekevu  ili kuomba huruma,upendo na rehema zake.Unyenyekevu ni hitaji la msingi  la Mungu mwenyewe ili akuinue kutoka maisha ya unyonge  na dhambi ili  uonje huruma,upendo na rehema zake.Majivuno yasitoke vinywani mwetu hata pale Mungu  anapotubariki kiasi tunyenyekee mbele ya mkono wa Bwana na kumrudishia sifa, utukufu na shukrani. Yakobo 4:6 “lakini hutujalia sisi neema  iliyozidi, kwa hiyo husema, Mungu  huwapinga  wajibu kwao, bali huwapa neema wanyenyekevu” Mungu humhesabia haki mtu  anayekwenda  mbele zake kwa unyenyekevu. Luka 18:9-14 Huu ni mfano alioutoa Bwana wetu Yesu Kristo  kuhusu maombi ya farisayo mmoja na mtoza ushuru wakati wakutoa  sadaka. Farisayo alijihesabia  haki akasimama akiomba hivi moyoni mwake, Ee Mungu ,nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi,wala si kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili  kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama  mbali , wala hakuthubutu hata kuinua  macho yake mbinguni, alijipiga piga  kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Yesu akawaambia, huyu alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko yule farisayo, kwa maana  kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Yesu akawaambia mfano mwingine wa wale walioalikwa ambao huchagua  vitu vya mbele. Luka 14:8-11 “Ukialikwa na mtu harusini, usiketi katika kiti cha mbele, isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika  wewe na yeye  na kukuambia, mpishe huyu! ndipo utakapoaanza kwa haya  kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapo kuwa  na utukufu  mbele ya wote  walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa” Mifano hii inaonyesha wazi kuwa kiburi  cha mtu kitamshusha, bali mwenye roho ya unyenyekevu ataheshimiwa ingawa BWANA yuko juu amwona mnyenyekevu,naye amjua  mwenye  kujivuna tokea mbali. Mungu huwapa wanyenyekevu  na kuwaokoa  kwa mkono wake hodari lakini huwapinga  wenye kiburi. Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha unyenyekevu  kwa vitendo pale  alipoonewa lakini alinyenyekea hadi mauti Isaya 53:7. “Alionewa, lakini alinyenyekea wala hakufunua kinywa chake.” Yesu Kristo Bwana  wetu ili atuokoe  kutoka katika ulimwengu wa dhambi alijifanya  kuwa hana utukufu, akatwaa  namna  ya mtumwa, akawa ana  mfano wa meanadamu ; tena alipoonekana  anaumbo kama mwanaadamu, alijinyenyekeza  akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba (Wafilipi 2:5-8). Mfano mwingine  wa unyenyekevu  aliotuonyesha  Yesu Kristo ni pale  alipowaosha  miguu wanafunzi wake. Yohana 13:5, 14,-15 “Kisha akatia maji katika bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta  kwa kile kitambaa  alichojifunga. Basi ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, ninawatawadha miguu, inawapasa  vivyo kutawadhana  miguu ninyi kwa ninyi. Kwa kuwa nimewapa kielelezo, ili kama mimi  nilivyowatendea  nanyi mtende vivyo. “Neno la Mungu  linatutaka  kunyenyekeana katika kicho cha  Kristo, kwa unyenyekevu,wote na upole kwa  kuvumiliana,na  kuchukuliana kwa upendo.  Wakolosia  3:12-14 “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule  wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole , uvumilivu,  mkichukuliana na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Baba  alivyowasamehe nunyi, vivyo na ninyi. Zaidi wa hayo yote  jivikeni upendo, ndio kifungo  cha ukamilifu”. “Neno la Mungu  linafundisha  vijana  kuwa wnyenyekevu ili Mchungaji  mkuu atakapodhihirishwa  waipokee taji  ya utukufu ile isiyokauka -1 Petro 4:5-6 “vivyo hivyo ninyi  vijana , watii wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu, mpate kuhudumiana kwa sababu  Mungu huwapinga  wenye kiburi, lakini huwapa wanyenyekevu neema. Basi nyenyekeeni chini ya  mkono wa Mungu ulio hodari, iliawakweza kwa wakati wake  “Mungu wetu anapendezwa na ibada ya maombi inayofanyika katika moyo wa unyenyekevu na kicho; maana Mungu wetu ni moto ulao. Tikijinyenyekesha  na kuomba kwa kweli huku tukiuangalia uso wa BWANA  yeye ni mwaminifu atasikia kuomba kwetu na kutupatia mahitaji yetu sawa sawa  na mapenzi yake.

Share This