• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

 MAOMBI NA SHUKRANI ZETU KWA MUNGU KWA KUTUPATIA ZAWADI YA WATOTO

Neno la Mungu katika Wafilipi 4:6 linasema, “Msijisumbue kwa neno lolote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru”. Mungu mwenye enzi yote Baba wa rehema tunakushukuru kwa kutupa zawadi ya watoto. Tunatanguliza shukrani zetu kabla ya kuleta haja za mioyo yetu kwa kuwa tunajua hatukustahili jambo hili bali tumelipata bure tu kwa neema yako iliyo kubwa mno. Neema yako yatosha. Tunawaleta watoto wetu kwako, ili uwaguse, uwakumbatie, uweke mikono yako juu yao, uwabariki (Marko 10:13-6). Tunawaacha mikononi mwako ili wakue katika njia ipasayo wakue katika hekima na kimo wakikupendeza Wewe na wanadamu. Wakujue Wewe Mungu wa pekee na wa kweli na mwanao Yesu Kristo uliyemtuma. Watambue ya kuwa Yesu Kristo Bwana wetu ndio njia ya kweli na uzima. Njia hii wasiiache hata watakapokuwa wazee. Tunakuomba Mungu, muumba wa mbingu na nchi uwafundishe watoto wetu neno lako takatifu. Uwafundishe kusikiliza maagizo yako yote na kuyafuata kwa utii ili siku zote wawe vichwa katika mambo ya kimwili na kiroho na kamwe wasiwe mikia.

Kipekee tunawaleta mbele za uso wako wazaliwa wetu wa kwanza ambao ni malimbuko kwako. Baba katika jina la Yesu Kristo Bwana wetu tunakushukuru na kusema Ahsante kwa ajili ya wazaliwa wote wa kwanza katika uzao wetu. Tunawainua mbele zako tukikuomba kuwa kusudi lako kwenye maisha yao litimie. Tunajua kuwa unawawazia mawazo yaliyo mema na yenye matumaini. Maisha yao yawe mfano mzuri wa kuigwa na ndugu zao. Wape nguvu za kiroho na kimwili, hekima na busara katika kufanya maamuzi. Wape ujuzi, maarifa na nguvu ya kutawala, kuongoza na kumiliki kwa mkono wenye nguvu kwa Jina la Yesu, jina lipitalo majina yote. Wezi wa haki na nafasi ya mzaliwa wa kwanza tunawapinga kwa moto wa damu ya Yesu Kristo.

 Tunakuomba Mungu uwalinde na kuwatetea watoto wetu wote kinyume na nguvu zote za giza. Tunakuomba uwasamehe uovu wao wote, wala dhambi yao usiikumbuke tena. Sadaka tutakazotoa zikasimame kama zile za mtumishi wako Ayubu (Ayubu 1:5). Tunawafunika watoto wetu wote kwa damu ya Yesu, damu inayonena mema kinyume na mabaya yote. Tunasambaratisha kila mpango wa adui juu yao kwa jina la Yesu Kristo Bwana wetu.

Na sisi wazazi wao hatutawaficha watoto wetu matendo yako makuu na ya ajabu. Tutawaeleza sifa zako na nguvu zako. Tutawasimulia matendo yako makuu Wewe uliye juu kwa furaha na mashangilio. Jina la Yesu Kristo ni tamu sana, onjeni muone. Amen.

Share This