• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

TUNAMSHUKURU MUNGU KWA KUZIDISHA UZAO WETU

Wote tunashuhudia kuwa Mungu amezidisha uzao wetu kuanzia kwa Shaidi Nziamwe Mkaza na mkewe Kompeho Msangi Narundu hadi wajukuu wao na vitukuu vyao. Tunamwomba Mungu azidi kutubariki na kuzidisha uzao wetu, kwa kuwa sisi ni uzao wa Ibrahimu baba yetu wa imani. Mwanzo 22:17(a), 18 Katika kubariki nitakubariki, na katika kuzidisha nitauzidisha uzao wako, na “katika uzao wako mataifa yote ya dunia watajibarikia; kwa sababu  umetii sauti yangu”. Na sisi uzao wa Shaidi, Mungu atatubariki na kuzidisha uzao wetu tukitii sauti yake. Sauti yake inasema nasi kwa njia mbalimbali kupitia ndoto, maono na katika neno lake. Kwa hiyo tukilisoma neno la Mungu na kutii amri zake na maagizo yake yote atatubariki na kuzidisha uzao wetu. Kama tukikubali na kumtii Mungu tutakula mema ya nchi (Isaya 1:19). Utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii na kutunza na kuyafanya maagizo yake yote akuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya dunia na utabarikiwa mjini, utabarikiwa mashambani. Utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako (Kumbukumbu la Torati 28:1-6). Isaya 1:20 “Bali kama mkikataa na kuasi mtaangamizwa kwa up anga; maana kinywa cha BWANA kimenena haya”. Wote kama familia moja ya Mungu tumwombe kuwa asiwepo yoyote wa uzao wa Shaidi katika kundi hili la kuangamizwa. Roho Mtakatifu atufundishe jinsi ya kumtii Mungu kwa bidii zetu zote ili wote tuingie katika ufalme wa mbinguni. Mimi na wewe tunaotoa sadaka za shukrani tunatakiwa tuwe watii na wanyenyekevu mbele za Mungu. Kwa sababu kipimo kizuri cha utoaji matoleo si wingi tu wa sadaka au ukubwa wa sadaka bali ni utii. Utii ni bora kuliko dhabihu. Basi ndugu zangu tumtii Mungu siku zote za maisha yetu kwa kuogopa na kutetemeka kwa kuwa yeye ni Alpha na Omega.

Jina la BWANA lihimidiwe. Amen

Share This