• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

TUNAMSHUKURU MUNGU KWA KUULINDA UZAO WETU

Ndugu zangu katika Yesu Kristo Bwana wetu, ni kweli kuwa tunaishi kwenye ulimwengu huu wenye vita vya kimwili na vya kiroho. Watesi wetu pamoja na ibilisi yule aitwaye shetani wako pande zote wakituvizia ili watuangamize. Waefeso 6:12 “Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho”. Je, tutapataje kupona katika vita hii? Vita yetu tumkabidhi BWANA, vita ni vikali lakini Mungu akiwa upande wetu ni nani aliye juu yetu? Macho yetu yamtazame BWANA wa majeshi, tusiogope wala tusifadhaike mioyoni mwetu kwani vita si yetu bali ni ya Mungu wetu. BWANA akiwa pamoja nasi atatupigania nasi tutanyamaza kimya (Kutoka 14:14). Katika vita yoyote itakayoinuka juu yetu tumtegemee Mungu peke yake tuseme kama mtumishi wa Mungu Daudi katika Zaburi 23:4 “Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti, sitaogopa mabaya; kwa maana Wewe upo pamoja nami, gongo lako na fimbo yako vyanifariji”.  BWANA ndiye kimbilio letu na ngome yetu. BWANA atakulinda na mabaya yote utokapo na uingiapo tangu sasa na hata milele. Ni watu gani hao ambao Mungu anawapa ulinzi mkubwa namna hii? Mungu anawalinda watu wake wamchao na kuzishika amri na maagizo yake yote. Watu wanaomtii na kulishika neno lake takatifu. Yeye ni ngao kwa wote wanaomkimbilia, wanaomtumaini na kumtegemea. Mithali 18:10 “Jina la BWANA ni ngome imara; wenye haki huikimbilia, wakawa salama”. BWANA anasema atawafanyia wamchao matakwa yao; Naye atasikia kilio chao na kuwaokoa. BWANA huwahifadhi wote wampendao na huwaokoa waadilifu wake katika mabaya yote. BWANA huwahurumia watumishi wake na kuwalinda (Zaburi 34:22, Isaya 41:8-10). Je mimi na wewe tuko kwenye kundi lipi?

Tukishaamua kutembea na Mungu, kumtegemea, kumtumainia na kumtazama Yeye tu na kutimiza amri, maagizo na mafundisho ya neno lake tutapata ulinzi wake na amani kamili. Hapo ndipo maombi ya BWANA wetu Yesu Kristo katika Yohana 17:15 yatakuwa yetu, “Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali uwalinde na yule mwovu”. Amen. 

Share This