· Kuomba kwa bidii na juhudi bila kukoma.
Katika shughuli zetu na maisha yetu ya kawaida tunaposema kufanya jambo lolote kwa bidii na juhudi tunamaanisha kulifanya jambo hilo kwa kiwango kikubwa zaidi ya kawaida. Kuomba kwa bidii na juhudi ni kuwa ufahamu wetu na mioyo yetu izame katika kuomba, kwa kumaanisha, kwa kung’ang’ania au kwa msisitizo mkubwa, kwa ujasiri na viwango vya hali ya juu bila kukata tamaa na bila kukoma. Mungu anataka tumwombe kwa bidii si walegevu tukiwa na juhudi katika roho zetu tukimtumikia Bwana (Warumi 12:11). Neno la Mungu linasema maombi ya mwenye haki yafaa sana tena akiomba kwa bidii.Haki inayotajwa hapa inapatikana katika kumuamini Bwana Yesu Kristo bila shaka yoyote kuwa ni Bwana na mwokozi wa maisha yako. Ili uweze kuomba kwa bidii na juhudi huna budi kukaa ndani yake naye kukaa ndani yako. Tukiomba kwa bidii na juhudi kwa hisia na shahuku kubwa, kwa ufanisi na kumaanisha Mungu anazo ahadi kwetu. Wafilipi 4:19 “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadri ya utajiri wake katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu. Mungu hujitokeza kwa viwango vikubwa visivyopimika tunapomwomba kwa bidii na juhudi bila kukoma tukionyesha kumtegemea yeye peke yake. Huku tukimtwika yeye fadhaa zetu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana kwa mambo yetu. Zaburi 55:22 “Umtwike Bwana mzigo wako naye atakutegemeza, hatamwacha mwenye haki aondoshwe milele. Tukiomba kwa bidii na juhudi bila kukoma huku tukimtwika fadhaa zetu Mungu aweza kufanya mambo yasiyowezekana kwa wanaadamu bali yawezekana kwa Mungu. Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuomba kwa bidii pale alipofunga na kuomba kwa siku 40 mfululizo, ili apate nguvu ya kutosha ndani yake ili aweze kuikabili kwa ujasiri mkubwa kazi iliyokuwa mbele yake. Mathayo 1:2,11- “ Kisha Yesu alipandishwa na Roho nyikani ili ajaribiwe na Ibilisi. Akafunga siku arobaini mchana na usiku, mwisho akaona njaa. Bwana Yesu aliposhinda majaribu ya Ibilisi malaika wakaja wakamtumikia. Tunajifunza pia kwa Bwana Yesu kuomba kwa bidii kama alivyofanya katika mlima wa Mizeituni. Luka 22:44 “ Naye kwa vile alivyokuwa katika dhiki, akazidi sana kuomba, hari yake ikawa kama matone ya damu yakidondoka nchini. Malaika kutoka mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Hata wewe mkristo mcha Mungu utakaposhinda majaribu ya shetani Mungu atakutia nguvu. Tunayo mifano mingi ya watu wa Mungu waliomba kwa bidii na juhudi na Mungu akasikia maonbi yao. Katika somo hili tutatafakari mifano michache. Yakobo 5:17-18 “Eliya alikuwa ni manaadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua asinyeshe na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita. Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua ,nayo nchi ikazaa matunda yake.Eliya aliomba kwa bidii mara saba bila kukata tamaa ndipo mvua ikanyesha. Katika kitabu cha Mwanzo 32:24,25 “Yakobo akakaa peke yake, na mtu mmoja akashindana naye mweleka hata alfajiri. Akasema niache niende, naona kunapambazuka, akasema sikuachi usiponibariki. Yakobo aling’ang’ania ombi lake hilo hadi akambariki huko Penueli, maana alisema nimeonana na Mungu uso kwa uso na nafsi yangu imeokoka Kung’ang’ania katika maombi kunaonyesha imani na pia uvumilivu ambalo nitendo la Roho Mtakatifu linalotawala maisha yote ya wokovu. Mfano mwingine wa kuomba kwa juhudi ni pale kanisa la kwanza lilipoomba kwa ajili ya Mtume Petro aliyekuwa amefungwa gerezani. Watu wengi walikutana katika nyumba ya Mariamu wakiomba kwa ajili ya Petro. Matendo ya Mtume 12:5 “Basi Petro akalindwa gerezani nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake. Mungu akampeleka malaika wake akamtokea Petro na kumtoa gerezani. Neno la Mungu linatutaka tuombe kwa bidii na juhudi bila kukoma. Kwa maana nyingine tunatakiwa kudumu katika maombi siku zote za maisha yetu. Kuomba ni kuwa na mazungumzo na Mungu kwa hiyo kuomba bila kukoma ni kuwa na uhusiano wa kudumu na Mungu katika pendo lake. Hii ni njia nzuri ya kuendelea kutegemea neema ya Mungu katika maisha yetu. Hana alipodumu katika kuomba na kumimina moyo wake kwa BWANA, Mungu alimjaalia haya yake aliyomwomba na kumpatia mototo mume akamwita jina lake Samweli akisema kwa kuwa nimemuomba kwa BWANA 1 Samweli 1:12,17 “Ikawa, hapo alipodumu kuomba mbele za BWANA, Eli alimwangalia kinywa chake. “Eli alitambua ya kuwa Hana alikuwa akinena moyoni mwake na kuimimina roho yake mbele za BWANA. “Ndipo Eli akijibu, akasema, Enenda kwa amani na Mungu wa Israeli akujalie haya yako uliyomwomba. Katika Agano Jipya neno la Mungu linatufundisha kuwa tufurahi siku zote na tuombe bila kukoma kwa maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwetu katika Kristo Yesu. Waefeso 6:18 “Kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote.” Bwana wetu Yesu Kristo anatutaka tukeshe katika kuomba kama vile alivyokesha alipokuwa akiomba katika mlima wa Mizeituni ili tusije tukaingia majaribuni. Mathayo 24:24,44 “Kesheni basi, kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu. “Kwa sababu hiyo ninyi niwekeni tayari, kwa kuwa katika saa msiyo dhani Mwana wa Adamu yuaja. Basi kesheni ninyi kila wakati mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea na kusimama mbele za Mwana wa Adamu (Luka 21:36). Bwana wetu Yesu Kristo alisisitiza sana umuhimu wa kuomba siku zote. Luka 18:1 “Akawaambia mfano ya kwamba imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa .Akawapa mfano wa kadhi dhalimu na mwanamke mjane aliyekuwa akimuendea endea akisema, nipe haki na adui wangu. Naye kwa muda alikataa, halafu akasema moyoni mwake, ijapokuwa simchi Mungu wala sijali watu, lakini kwa kuwa mjane huyu ananiudhi nitampa haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima. Luka 18:2-8 “Na Mungu je! Hatawapa haki wateule wake wanaomlilia mchana na usiku, naye ni mvumilivu kwao. Nawaambia, atawapatia haki upesi; walakini atakapokuja Mwana wa Adamu, je!Ataiona imani duniani? Mungu anataka tudumu katika kuomba kwa juhudi na bidii bila kukoma; tukijiombea sisi wenyewe, watakatifu wote, kanisa la Mungu, watawala na watu wote, Wakolosai 4:2 “Dumuni sana katika kuomba, mkikesha katika kuomba huku na shukrani. Katika neno hili tunajifunza kuwa tunatakiwa kuwa na maombi ya shukrani kwa Mungu Katika sehemu inayofuata tutatafakari umuhimu wa kumshukuru Mungu.
· Kumshukuru Mungu.
Lengo la somo hili sio kuhusu aina ya maombi ya shukrani bali ni kuonyesha kuwa maombi yetu ya ambatane na shukrani kwa Mungu wetu. Kila tunapoomba tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa kutupatia nafasi ya kumwomba. Mungu anapendezwa na watu wenye moyo wa shukrani, wanaotambua kuwa yote waliyonayo yanatoka kwake. Tusisubiri kumshukuru Mungu wakati amejibu maombi yetu tu bali tumshukuru kila wakati tukitambua kuwa wakati mwingi Mungu kwa neema yake iliyo kuu hutupa vitu au mahitaji yetu hata kabla hatujamwomba.Kumbuka kuwa Roho Mtakatifu naye hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa naye anazijua haja zetu zote. Isaya 65:24 “Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu, na wakiwa katika kunena, nitasikia.” Kwa kila jambo tunaloliomba tunapaswa kumshukuru Mungu kwa imani kuwa tulichokiomba tumeshapokea katika ulimwengu wa Roho na kuwa kitadhihirika katika ulimwengu wa mwili, sawasawa na mapenzi ya Mungu. 1 Wathesalonike 5:18 “Furahini siku zote, ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo, maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.” Katika Agano la Kale tunajifunza kuwa wana wa Israeli na watumishi wa Mungu walipomshukuru Mungu walipata mafanikio kwa kuwa Mungu alisikia kuomba kwao. 2 Samweli 22:1,50 “Basi Daudi akamwambia BWANA maneno ya wimbo huu, siku ile BWANA alipomwokoa mikononi mwa Sauli”, Akasema “Basi, BWANA, nitakushukuru kati ya mataifa, nami nitaliimbia jina lako”. 2 Mambo ya Nyakati 20:21 “Naye (Yehoshafati) alipokwisha kufanya shauri na watu,akaweka wale watakaomwimbia BWANA, na kumsifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi na kusema, Mshukuruni BWANA kwa maana fadhili zake ni za milele.” Walipomwimbia BWANA nyimbo za shukrani walishinda vita ile wakawapiga adui zao. Mfalme Daudi alitambua wema na ukuu wa Mungu katika maisha yake, alitambua kuwa ni neno jema kumshukuru Mungu usiku, asubuhi na mchana na ndio maana ameandika na kuimba Zaburi nyingi za kumshukuru Mungu. Zaburi 92:1-2 “Ni neno jema kumshukuru BWANA, na kuliimbia jina lako, Ee uliye juu. Kuzitangaza rehema zako asubuhi, na uaminifu wako wakati wa usiku.” Zaburi 100:4-5 “Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru; nyuani mwake kwa kusifu; Mshukuruni, lihimidini jina lake; kwa kuwa BWANA ndiye mwema,rehema zake ni za milele, na uaminifu wake vizazi na vizazi.” Zaburi 109:30 “Nitamshukuru BWANA kwa kinywa changu, naam, nitamsifu katikati ya mkutano.” Zaburi 118:21,29 “Nitakushukuru kwa maana umenijibu, nawe umekuwa wokovu wangu. Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema, kwa maana fadhili zake ni za milele.” Na sisi kama Daudi tunatakiwa kutambua kuwa Mungu amesikia maombi yetu na ametutendea mambo makuu katika maisha yetu hivyo tumrudishie sifa na shukrani. Bwana wetu Yesu Kristo alimshukuru Mungu na kutoka kwake tunajifunza kumshukuru Mungu. Mathayo 26:27 “Akakitwaa kikombe, akashukuru, akawapa akisema, nyweni nyote katika hiki.” Wakati Bwana Yesu alipomfufua Lazaro wakaliondoa lile jiwe. Yesu akainua macho yake juu, akasema,Baba nakushukuru kwa kuwa umenisikia (Yohana 11:41). Baada ya maneno hayo ya kumshukuru Mungu muujiza mkubwa wa ufufuo wa Lozaro ulitokea. Bwana wetu Yesu Kristo alipowalisha wanaume elfu tano kwa mikate mitano na samaki wawili alishukuru. Marko 6:41 “Akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni akashukuru, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi wake wawaandikie; na wale samaki wawili akawagawia wote.”Baada ya Bwana Yesu kushukuru ulitokea muujiza mkubwa; wakala wote wakashiba. Wakaokota vipande vilivyomegwa vya kuweza kujaza vikapu kumi na viwili na vipande vya samaki pia. Tunapata mfano mwingine wa umuhimu wa kushukuru pale Bwana wetu Yesu Kristo alipowatakasa watu kumi wenye ukoma lakini kati ya hao mmoja tu ndiye aliyerudi kumshukuru Bwana Yesu. Luka 17:15-19 “Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu, akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru, naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu akanena, hawakutakaswa wote kumi? Akamwambia Inuka,nenda, zako, imani yako imekuokoa. Hapa tunajifunza kuwa kwa kumshukuru Bwana Yesu yule Msamaria alipata jambo la ziada ambalo ni wokovu. Mtume Paulo anatufundisha kumshukuru Mungu kwa kuwa ndiye aliyetuokoa. Wakolosai 1:12-13 “Mkimshukuru Baba aliyewastahilisha kupokea sehemu ya urithi wa watakatifu katika nuru. Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake.” Tunapomshukuru Mungu hupokea shukrani zetu kwa kutubariki na kutufungulia mlango sawasawa na neno lake. Neno la Mungu linatutaka tumshukuru Mungu kwa ajili ya waumini wa Kristo pamoja na watu wote.Waefeso 1:15-16 “Kwa sababu hiyo mimi nami, tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu.” Shukrani zitolewe kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, tuishi maisha ya utulivu na amani, katika utauwa wote na ustahivu. Hili ni nzuri nalo lakubalika mbele za Mungu Mwokozi wetu ambaye hutaka watu wote waokolewe, na kupata kujua yaliyo kweli (1 Timotheo 2:1-4). Neno la Mungu linatutaka kuimba na kumshangilia mioyoni mwetu; na kumshukuru Mungu Baba siku zote kwa mambo yetu, katika jina lake Bwana wetu Yesu Kristo. Tukifanya hivi kwa mioyo safi pamoja na baraka za Mungu tunapata amani ya Mungu. Wafilipi 4:7 “Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.” Wakolosai 3:15 “Na amani ya Kristo iamue mioyo ni mwenu, ndiyo mliyotiwa katika mwili mmoja, tena iweni watu wa shukrani.” Watu wa shukrani wanaomshukuru Bwana Mungu wao kwa mioyo yao yote wanahitajika kuonyesha shukrani zao kwa matendo yaani wataonyesha kwa kumtolea Mungu sadaka iliyo njema machoni pa Bwana wao. Unapotoa sadaka ya shukrani tambua ya kuwa unatengeneza mazingira ya Mungu kujifunua zaidi kwako, kukuokoa siku ya mateso au taabu yako kukupa kibali katika njia zako. Mtu anapomtolea Mungu sadaka ya shukrani anampa Mungu utukufu na heshima kwa mambo yote aliyomtendea. Mungu ameagiza tumtolee dhabihu za kushukuru. Zaburi 50:14-15,23.“Mtoleeni Mungu dhabihu za kushukuru; mtimizie aliye juu nadhiri zako. Ukaniite siku ya mateso; nitakuokoa, na wewe utanitukuza. Atoaye dhabihu za kushukuru ndiye anayenitukuza. Naye autengeneza mwenendo wake, nitamwonyesha wokovu wangu.” Neno la Mungu linatufundisha kuwa sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani mwa BWANA zitasikilikana tena sauti za furaha na sauti za shangwe nao watakubalika mbele za BWANA. Atukuzwe Mungu wetu awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuwazayo. Atukuzwe katika kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.
SALA YA TOBA
- MUNGU BABA KATIKA JINA LA YESU, NIMESIKIA NENO LAKO NA NIME KUTAMBUA KUWA NI MWENYE DHAMBI. NINAKUOMBA UNISAMEHE DHAMBI ZANGU ZOTE NILIZOZIFANYA KWA KUNENA NA KWA KUWAZA NA KWA KUTENDA. LEO NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE, NAKUOMBA UNISAMEHE NA KUNIOSHA
KWA DAMUYA MWANAO YESU KRISTO.
- LEO NINAWEKA AHADI NA WEWE MUNGU, KUWA MALI YAKO NA MTOTO WAKO NIKUPENDE KWA MOYO WANGU WOTE NA AKILI ZANGU ZOTE NA NIKUTUMIKIE KWA UWAMINIFU MPAKA NITAKAPO KUFA.
- LEO NINAMKATAA SHETANI NA KAZI ZAKE ZOTE
NA MAMBO YA KEYOTE. NAJITOA KUWA WAKO EE BWANA MUNGU. BABA, MWANA NA ROHO MTAKATIFU, ILI NIKUTEGEMEE NAKUKUTUMIKIA KWA UAMINIFU HATA NITAKAPO KUFA.
- BWANA YESU FUTA JINA LANGU KATIKA KITABU CHA HUKUMU, ANDIKA JINA LANGU KATIKA KITABU CHAKO CHA UZIMA WA MILELE.
- NENO LA MUNGU TOKA WARUMI 10:9
Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa mungu alimfufua katika wafu utaokoka.
- NINA MKIRI YESU KRISTO KUWA NI BWANA NA NIMEAMINI KUWA MUNGU ALIMFUFUA KATIKA WAFU NA YUKO MBINGUNI AMEKETI MKONO WAKO WA KIUME AKINIOMBEA.
- ASANTE MWENYEZI MUNGU KWA KUNIOKOA. AMINA