Wapendwa ndugu zangu katika Yesu Kristo Bwana wetu na Mwokozi wa maisha yetu. Ninayo furaha kuleta mbele yenu mambo machache kwa ajili ya maandalizi ya kutoa sadaka ya ukoo, Vudee 2025. Ni vyema tufanye maandalizi ya kimwili na kiroho nimeyagawa katika sehemu kuu tatu kama ifuatavyo;
i. Shukrani zetu kwa Mungu.
ii. Maombi yetu kwa Mungu.
iii. Mafundisho na tafakari ya Neno la Mungu.
1.0 SHUKRANI ZETU KWA MUNGU
Kama Familia moja ya Mungu wote tutamshukuru Mungu kwa ndimi za kelele za furaha na shangwe zilizojaa kicheko kwa kuwa BWANA ni mwema na fadhili zake kwetu ni nyingi na njema. BWANA ametutendea matendo makuu na mema na ya ajabu machoni petu. Ni vyema na itapendeza kumshukuru Mungu kuanzia sasa hadi kilele cha siku ya kutoa sadaka Vudee tarehe 21/9/2025. Siku ile ya kutoa sadaka tutamshukuru Mungu kwa pamoja kama familia moja ya Mungu. Tumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu kwetu na ya ajabu.
Ø Tumshukuru Mungu pia kwa kuzidisha uzao wetu na kuulinda.
Ø Tumshukuru Mungu kwa ajili ya zawadi ya watoto aliotupa.
Ø Tumshukuru Mungu kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika elimu.
Roho Mtakatifu atutangulie katika jambo hili na atufundishe kushukuru kwa kila jambo.
2.0 MAOMBI YETU KWA MUNGU
Pamoja na shukrani zetu kwa Mungu tutapeleka haja za mioyo yetu kwa Mungu wetu. Mungu anatukaribisha tumwombe jambo lolote lile naye atalifanya. Yohana 14:13-14 “ Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya”. Tunatakiwa kuomba kwa imani na kuamini kuwa hayo tunayoyaomba yatatokea (Marko 11:24). Ninajua kuwa kila mtu atapeleka haja za moyo wake na familia yake kwa Mungu.
Kwa pamoja kama familia moja ya Mungu.
Ø Tumwombe Mungu aubariki uzao wa Shaidi uwe mzao mteule kwake na umiliki mlango wa adui (1 Petro 2:9 na Mwanzo 22:17).
Ø Tumwombe Mungu neema ya wokovu (Waefeso 2:8-10).
Ø Tumwombe Mungu upendo wa ndugu na umoja udumu kati yetu (Yohana 13:34 na 2 Petro 1:7).
Roho Mtakatifu atufundishe kuomba itupasavyo.
3.0 MAFUNDISHO NA TAFAKARI YA NENO LA MUNGU
Maandalizi yetu ya kutoa sadaka ya ukoo yaambatane na kujifunza na kutafakari neno la Mungu. Kila mmoja wetu awe na muda wa kusoma na kutafakari neno la Mungu kwani neno la Mungu ndio taa na mwanga katika maisha yetu hapa duniani. Kila mtu atafakari kama Roho Mtakatifu atakavyomwongoza.
Tunaweza kujifunza na kutafakari;
Ø Nguvu ya neno la shukrani.
Ø Sifa ya sadaka inayompendeza Mungu.
Roho Mtakatifu awatie nguvu, awape maarifa na ujuzi wale wote watakaokuwwa tayari kutushurikisha mafundisho ya neno la Mungu.
Kwa utukufu wa Mungu wetu. Jina la BWANA lihimidiwe.