VUDEE WAMKUMBUKA NA KUMUENZI MHE. BABA WA TAIFA MWL. JULIUS KAMBARAGE NYERERE.
1.0 UTANGULIZI
Vudee ni kijiji kilichopo katika kata ya Vudee, wilaya ya Same, mkoa wa Kilimanjaro.
Kata ya Vudee inaidadi ya watu wapatao 6114 wanaume 3050 na wanawake 3064 ambao ni sawa na kaya 1436 kulingana na sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022. Wananchi wa kata ya Vudee wanashirikiana wote wanaume na wanawake katika kazi za maendeleo. Katika kazi mojawapo kubwa waliyofanya kwa ushirikiano mkubwa ni ujenzi wa barabara kutoka Bangalala hadi Vudee. Wanamkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa Mhe.Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa sababu alikuwa mdau muhimu sana katika kufanikisha kazi hiyo. Kabla ya uhuru mwaka 1961 wananchi wa Vudee waliteseka sana kwa kukosa barabara (miundombinu ya barabara). Baba wa Taifa Mhe. Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika kuwatia wananchi moyo alitembelea kijiji cha Vudee mara tatu mwaka 1961, 1967 na 1970.
1.1 Miundombinu ya barabara kabla ya uhuru 1961
Miundombinu ya barabara kutoka tambarare Bangalala hadi milimani Vudee wakati huo ilikuwa haipo kabisa. Hapakuwepo na barabara kwa hiyo usafiri wa watu ulikuwa kwa miguu. Kukosekana kwa usafiri mzuri wa gari kuliwatesa watu mno kwani walisafiri na mizigo mizito vichwani au mabegani mwao kwa mwendo mrefu hadi Bangalala au kutoka Bangalala hadi Vudee umbali wa takribani kilomita 8. Kazi nyingine iliyokuwa ngumu sana ni ya kubeba wagojwa kwa machela hasa akina mama wajawazito kutoka Vudee hadi hospitali ya wilaya ya Same. Shughuli nyingi za kiutawala na kiuchumi ziliwafanya watu watembee kwa miguu kutoka Vudee hadi Makanya, kilomita 20. Makanya ndio kilikuwa kituo kikubwa cha kiutawala na kibiashara kwa watu wa Vudee wanaokwenda Tanga na Moshi. Makanya ilikuwa station kubwa ya gari la moshi (treni) kutoka Tanga kwenda Moshi. Wafanyabiashara wanao kwenda kufungasha bidhaa kutoka Tanga au Moshi walitumia treni hii. Kutoka Makanya mizigo ilibebwa kwa kichwa hadi Vudee. Wakati huo wilaya ya Same ilikuwa mkoa wa Tanga kwa hiyo shughuli zingine za kiutawala zilimtaka mwananchi wa Vudee atembee kwa miguu hadi Makanya kupanda treni (gari la moshi) hadi Tanga. Wananchi wa kata ya Vudee kwa kujua umuhimu wa barabara wakajitolea ardhi zao zikatumika kwa ajili ya barabara bila ya kudai fidia ya aina yoyote ile. Wananchi wa Vudee walielewa kuwa ili wapate maendeleo wanahitaji ardhi ipatikane bila vikwazo au vizuizi vyo vyote.
1.2 Miundombinu ya barabara baada ya uhuru- 1961.
Wananchi wa kata ya Vudee kwa kutambua shida ya usafiri waliyokuwa nayo na kwa kutambua kuwa maendeleao ya uchumi na kijamii yanategemea sana miundo mbinu ya barabara waliamua kuchimba barabara kutoka tambarare Bangalala hadi milimani Vudee. Kazi hii ilianza Juni 1960 hadi tarehe 4/04/1970 kwa muda wa miaka 10. Mwaka 1961 Baba wa Taifa alitembelea Vudee eneo la Vudee – Nyika kwa mara ya kwanza wakati huo barabara ilipoanza kuchimbwa. Mwl. Julius K. Nyerere aliungana nao kwa kufanya kazi pamoja nao akawatia moyo na kuwapa misaada. Uchimbaji wa barabara hii kwa kutumia majembe na masururu ulikuwa mgumu sana kwa sababu ya miinuko mikali, milima, mawe makubwa na miamba. Haikujulikana kuwa barabara hii ingeweza kufika Vudee lakini wananchi wa Vudee kwa kauli moja chini ya viongozi wao walifanya kazi kwa kujitolea bila kuchoka wala kukata tamaa wakiongozwa na moto wa siasa ya Ujamaa na kujitegemea. Viongozi wa kabla ya uhuru walikuwa ‘mlao’ Njaule Dindeni na Mzee Tuvako
Sempombe aliyefanya sala wakati wa kuanza kazi. Mpima wa barabara alikuwa Mbazi Yosefu kutoka Halmashauri ya wilaya ya Same. Baada ya uhuru Diwani wa kata ya Vudee alikuwa Ndg. Fahamuel Kashingo na Mbunge alikuwa Mhe. Chedieli Yohana Mgonja. Viongozi hawa chini ya siasa safi ya ujamaa na kujitegemea na uongozi bora wa Mwl. J.K. Nyerere waliweza kuhamasisha wananchi kujitolea kuchimba barabara. Kwa kuwa walikuwa wazalendo wa nchi yao walifanya kazi kwa kutoa nguvu zao bila kudai malipo. Njia waliyotumia kuhamasisha watu ni njia ya tamasha lililojulikana kama ‘msaragambo’ kwa Kipare. Wananchi hupangiwa siku maalum ya kujitolea kuchimba barabara. Siku hiyo panda ikipigwa kila mtu alitakiwa kutoka na kwenda “msaragambo’’. Mtu akishindwa kwenda ‘msaragambo’ bila sababu ya msingi anatozwa faini ya fedha,kuku au mbuzi. Wazee ambao kwa ajili ya umri wao hawawezi kuchimba barabara wao walipangiwa kutoa ng’ombe mmoja ambaye ataliwa siku ya tamasha. Wazee waliheshimu mapatao hayo. Siku ya tamasha kila mshiriki alikatiwa kipande chake cha kuchimba ambacho kwa Kipare kiliitwa “kipinka’’ ukishindwa kumaliza “kipinka’’ chako siku ya tamasha utamaliza siku nyingine kwa wakati wako. Wananchi walifanikiwa kuchimba barabara hadi eneo linaloitwa Mhewe. Eneo hilo lina mwamba mkubwa au jabali kubwa ambalo ni lazima lipasuliwe ndio barabara iweze kupita hapo kwenda Vudee.
1.3 Baba wa Taifa Mhe. Mwl.Julius Kambarage Nyerere afika Mhewe.
Mwaka 1967 Baba wa Taifa Mhe. Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipokelewa kwa vifijo, shangwe na nderemo wakati alipofika Mhewe. Mhe. Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliambatana na viongozi wengi wa Serikali akiwemo aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje Mh. Oscar S.Kambona. Mwl.Nyerere aliwakuta wananchi wakiwa juu ya mwamba huo wakijibidisha kupasua mawe kwa kutumia vifaa na nyenzo duni sana. Walichoma mawe kwa moto wa kutumia kuni kisha walimwagia maji baridi jiwe lililochomwa na hatimaye kulivunja kwa kutumia nyundo. Wakati mwingine walichonga mawe kwa kutumia vipande vya nondo na kisha kuweka utambi ndani ya shimo lililochongwa na kuwasha utambi huo. Mawe yalipasuka kwa shida kubwa sana. Ujio wa Mwl.Nyerere uliwapa wananchi wa Vudee matumaini makubwa sana. Risala ya wananchi ilisomwa na Mwl. Napendaeli Tumaini Mgonja. Alisoma risala hiyo macho yake yakiwa wakati mwingi yanatazama jabali la Mhewe kwa kuwa alikuwa anatafuta jibu la namna ya kuvunja jabali hilo. Akijibu risala hiyo Mwl.Nyerere pamoja na kutoa msaada wa baruti kwa ajili ya kupasulia mwamba wa Mhewe au jabali la Mhewe aliwatia moyo wananchi wa Vudee. Mwl.Nyerere alifurahishwa sana na jinsi wananchi wa Vudee walivyokuwa wanafanya kazi kwa juhudi na bidii nyingi. Mwl.Nyerere akawafananisha na Wachina kwa kusema kuwa nimewaona Wapare – Wachina akiwa na maana kuwa wanafanya kazi kwa juhudi kama Wachina. Maneno hayo yaliwatia moyo wananchi wa Vudee wakaongeza kasi na bidii ya kazi. Mwl. Nyerere aliiagiza Serikali ishirikiane na wananchi katika kazi hiyo na aliahidi kuwa atarudi tena Vudee kuiona barabara hii itakapokamilika. Hatimaye waliweza kupasua mwamba wa Mhewe na barabara ikapita hapo hadi Vudee missioni. Kwa kuheshimu juhudi za Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika ujenzi wa barabara ya Vudee wananchi waliamua kumkaribisha kuwa Mgeni rasmi katika ufunguzi wa barabara.
1.4 Baba wa Taifa Mhe. Mwl. Julius Kambarage Nyerere afika Vudee mission.
Tarehe 4/4/1970 ilikuwa siku ya furaha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere alipofika Vudee kufungua barabara hiyo. Sherehe zilipambwa na ngoma za Kipare (madungu,mwelema na ijanja) pamoja na mashairi kwa Kipare (mbosia na nkani). Sherehe hizi zilifanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi Hembua. Risala ya wananchi iliyojaa upendo na shukrani nyingi kwa mara nyingine tena ilisomwa na Mwl. Napendaeli Tumaini Mgonja. Mhe. Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliweka alama ya uzinduzi kwa kupanda mti shuleni Nembua. Hadi leo hii mti huo unawakumbusha wananchi wa Vudee tukio hili la kihistoria. Tunapendekeza katika eneo hili ujengwe mnara wa kumbukumbu ili hata mti alioupanda ukizeeka na kukauka mnara huo utabaki kuwa kumbukumbu ya Mhe. Mwl. Julius Kambarage Nyerere. Vudee hatutamsahau Mhe. Baba wa Taifa Mwl.Julius Kambarage Nyerere. Ili kuenzi uasisi wake wa barabara hii ambayo iko chini ya TANROADS kuna changamoto ambazo zinatakiwa kutatuliwa.
2.0 CHANGAMOTO
Kata ya Vudee inazo changamoto nyingi lakini kubwa zaidi ni pamoja na hizi zifuatazo:-
2.1 Maboresho ya barabara.
Ubovu wa barabara aliyoihudumia Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere inahitaji kufanyiwa maboresho yafuatayo:-
2.1.1 Kuweka zege kwenye maeneo ya miinuko mikali na kwenye sehemu zenye udongo wa utelezi na kona kali kama vile Kanyota.
2.1.2 Kuweka mifereji ya maji ya mvua na ‘culverts’.
2.1.3 Kupanua barabara sehemu zote ambazo ni nyembamba sana.
2.1.4 Kuweka uzio kwenye maeneo hatarishi yenye miteremko mikali.
Haya yatakuwa maboresho ya ujenzi wa barabara Awamu ya kwanza. Awamu ya pili itakuwa ni kujenga barabara ya Bangalala – Vudee kwa kiwango cha lami. Tunapendekeza kuwa barabara hii ipewe jina la Julius Kambarage Nyerere.
Maboresho ya barabara hii pamoja na kumuenzi Baba wa Taifa yatasaidia kukuza uchumi wa wananchi wa Vudee katika kilimo, ufugaji na utalii. Itakumbukwa kuwa lengo mojawapo la Mwl. ni kuleta maendeleo ya wananchi ili kuondoa umaskini. Barabara hii itakuwa kivutio kikubwa cha utalii hasa eneo la mwamba wa Mhewe. Eneo hili linafaa kutumika kwa michezo na mashindano ya ‘rock climbing’. Vivutio vingine vya utalii ni mlima Shengena wenye vivutio vingi vya viumbe hai,miti ya dawa, na msitu mkubwa wa asili wenye vyanzo vya maji ya mito. Mtalii anaweza kufurahia kuona utamaduni wa Kipare na maisha ya asili ya Wapare na vifaa walivyo vitumia kwa kazi mbalimbali.
2.2 Ukosefu wa kituo cha Afya
Kata ya Vudee yenye vijiji 4 vya Ndolwa,Kisesa,Vudee na Menamu haina kituo cha Afya. Kata nzima ina zahanati moja tu ya serikali ya Ndolwa ambayo iko pembezoni mwa kata.
Wagonjwa kutoka vijiji vya mbali kama vile Kisesa hutembea kwa miguu hadi Ndolwa takribani kilomita 15. Ikumbukwe kuwa eneo hili ni la milimani. Wagonjwa wanaopewa rufaa inabidi waende Hospitali ya wilaya Same au kituo cha Afya Chome takribani kilomita 30 kutoka Vudee. Wagonjwa wengine hupoteza maisha kwa sababu ya ukosefu wa kituo cha Afya katika kata ya Vudee.
2.3 Ukosefu wa bweni la wasichana Sekondari ya Vudee.
Kata ya Vudee inazo shule za sekondari mbili, Vudee sekondari na Masheko sekondari. Shule hizi zina jumla ya wanafunzi wa kike 193 (2024). Wanafunzi wengine wanatoka vijiji vya mbali kama vile kijiji cha Kisesa kiasi cha kilomita 15. Wanafunzi hawa wanatembea kwa miguu kwenda shuleni asubuhi sana na kurudi nyumbani usiku. Wanafunzi hawa kando ya shida ya kutembea kwa miguu kwa muda mrefu wanapita maeneo yenye vichaka vikubwa na misitu. Shida nyingine wanayopambana nayo ni tatizo la mimba za utotoni. Mazingira haya ya kutembea usiku yanachochea upatikanaji wa mimba za utotoni. Wanafunzi wengine wameshindwa kutimiza ndoto zao kutokana na changamoto hii. Changamoto nyingine inayokabili shule hi ni ubovu wa barabara kutoka Vudee missioni hadi shuleni Kisingi. Barabara hii inahitaji matengenezo makubwa ili ipitike bila shida hasa wakati wa mvua.
3.0 MAOMBI YETU
Wananchi wa kata ya Vudee tuko tayari kushirikiana na Serikali kupitia nguvu za wananchi katika kutatua changamoto zinazotukabili. Tunaiomba Taasisi ya Kumbukumbu ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere itusaidie kufikisha changamoto hizi Serikalini ili kumuenzi Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere kwa juhudi zake kubwa alizofanya za kuleta maendeleo katika kata ya Vudee. Kipekee kabisa kwa heshima na taadhima tunaomba Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Mhe. Kayaza Mizengo Pinda na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini Mhe. Paulo Kimiti mtusaidie kufikisha kilio chetu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani. Tunamatumaini makubwa na Serikali yetu kuwa ni sikivu inayopenda maendeleo ya wananchi wake. Itakumbukwa kuwa azma ya Mwl. Julius Kambarage Nyerere toka hapo awali ilikuwa ni kuondoa maradhi, ujinga na umasikini kwa kuboresha maisha ya wananchi wake.
SHUKRANI ZETU
Tunaishukuru Serikali katika vita ya kupambana na ujinga kwa kuwa kata ya Vudee ina shule za msingi 4 na shule mbili za sekondari, zinazosaidia kuondoa ujinga katika jamii yetu. Vita hii ya kuondoa ujinga ambayo ilianzishwa na Mwl. Julius Kambarage Nyerere tunaiendeleza kwa nguvu zetu zote. Elimu iliyotolewa wakati huo ilizalisha watu mashuhuri nchini Tanzania kutoka Vudee akiwepo “Inspector General of Police” wa kwanza baada ya Uhuru mwaka 1961 – IGP Elangwa Shaidi. Mwingine kutoka Vudee ni aliyekuwa Waziri wa Elimu Mhe. Chedieli Yohana Mgonja (1968- 1972) wakati huo akiwa waziri kijana kuliko wote Tanzania. Baada ya hao Vudee imeendelea kutoa wataalam wengi ambao wameshika nyadhifu mbalimbali hapa nchini Tanzania na wengine wanaendelea kulitumikia Taifa hata sasa.
Tunamshukuru Mwl. Justin Mrindwa ambaye alisaidia kupata maelezo mbalimbali ya kihistoria yaliyosaidia kuandika taarifa hii. Mwl. Justin Mrindwa alizaliwa tarehe 6/5/1928. Mwl. Justin Mrindwa ndiye pia aliyeleta udongo ambao Mhe. Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliutumia kupanda mti wakati wa ufunguzi wa barabara ya Vudee.
Pamoja na taarifa hii tumeandaa “video” ambayo wazee wa Vudee wameelezea kumbukumbu zao kuhusu ujio wa Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere Vudee.
Wazee hao ni; Petro Imanuel Nashanda Mgonja, Barikieli Ezekieli Mmbaga, Stanley Elineema Mdoma. na Petro Mseli Mnzava.
Tunaishukuru pia kamati iliyoratibu upatikanaji wa taarifa hii; Dr. Ahadiel R. Senkoro, Dafrosa W. Mnzava, Vincent M. Shaidi, Grace Mungwe Shaidi, Kazeni Herieli Mnzava, Elineema Mdee na Keneth M. Shaidi.
Kwa taarifa zaidi wasiliana na Dafrosa W. Mnzava
Simu 0655 452 105 / 0754 462 105.
x