• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 23 Aug, 2023
  • Admin

UNUNUZI WA VYOMBO NA VIFAA VYA KUHUBIRIA INJILI USHARIKA WA VUDEE NA NDOLWA - 2022

1.UTANGULIZI. 

Wapendwa wacharo tunamshukuru Mungu wetu kwa jinsi alivyotembea pamoja nasi wakati wote tulipokuwa tunaifanya kazi yake. Mwenyekiti wa Wacharo wa Vudee na Ndolwa aliteua kamati na kuipa kazi ya kuratibu na kusimamia ununuzi wa vyombo kwa ajili ya mikutano ya Injili Vudee na Ndolwa. Tarehe 27/3/2022 wanakamati waliandaa “Group la WhatsApp” ili kurahisisha majadiliano na mawasiliano kuhusu majukumu waliyopewa. Tu kutoka nashukuru sana dada Miriamu Ombeni Mnzava kwa kuwa “Administrator” mwema wa Group hili, wakati wote. Wajumbe wa kamati hii ni; 

i.Miriam O. Mnzava – Katibu 

ii.Mary A. Senkoro

iii.Dr. Ahadiel Senkoro

iv.Mr. Kazeni Heriel Mnzava – Mweka Hazina 

v.Grace Shaidi Mungwe.

vi.Dr. Cristopher P.Mgonja 

vii.Mr. Eliyuko N. Mnzava 

viii.Naelijwa F. Mnzava 

ix.Mr. Vincent M. Shaidi – Mwenyekiti. 

2.VIFAA VYA SAUTI 

Kamati iliandaa orodha ya vifaa vinavyohitajika pamoja na gharama zake.  Kamati ilikuwa na wajibu wa kuchangisha shs 13,530,000/= ili kukamilisha kazi hii. Hili lilionekana kuwa sio jambo rahisi ni jambo gumu linalohitaji uso wa Mungu uende pamoja nasi. 

3.IBADA

Kamati iliandaa ibada tarehe 24/4/2022 katika kanisa la Azania Front kumwomba Mungu ili uso wake uende pamoja nasi. Ibada iliongozwa na Mch. Gwakisa Andrew Mwaipopo. Katika ibada hiyo tulimsifu Mungu kwa kuimba nyimbo kutoka Tumwabudu Mungu wetu nambari 440 Zaeni matunda mema zaeni ya heri na Wimbo Na. 59 Kazi ni yako Bwanangu. Neno la Mungu lilitoka Mwanzo 18:14 “kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana.” Neno hili lilitutia moyo sana na kutupa matumaini makubwa katika BWANA. Neno hili lilituandaa kwa ajili ya wajibu tuliopewa. Baada ya Neno tulifanya maombi na kutoa sadaka zetu kwa BWANA. Sadaka tulizotoa tuliamua kumkabidhi Mch. Mwaipopo ambaye alizipokea na kisha kuzirudisha kwetu ili ziwe mbegu katika shamba la BWANA. Tunamshukuru Mungu kwa kuzitakabali sadaka zetu ambazo zimemzalia matunda mema. Tunamshukuru pia Mch. Gwakisa A. Mwaipopo kwa kututia moyo na kutuongoza katika ibada. Tuliendelea kutiana moyo kwa maombi, sala na Neno la Mungu Ezra 10:4 “Inuka maana shughuli hii ya kuhusu wewe, na sisi tu pamoja nawe, uwe na moyo mkuu ukaitende.” Haya yalikuwa maandalizi muhimu sana katika kuitenda kazi ya BWANA.


4.HARAMBEE. 

Harambee ilifanyika baada ya ibada katika Kanisa la Azania Front. Akaunti ya Benki Na 23510056049 ilifunguliwa Benki ya NMB – Tegeta ili kuhifadhi fedha zitakazopatikana. Madhumuni ya Harambee hii ilikuwa kupata fedha za kununulia vyombo / vifaa vitakavyowekwa wakfu na kutengwa kwa ajili ya kazi ya Mungu. Katika Harambee hii tulitarajia kupata kiasi cha shs 13,530,000/= Baada ya Harambee tuliendelea kupokea michango kutoka kwa Wacharo wa Vudee na watu wengine. Hadi mwisho tulipata Jumla ya shs 13,905,000/= zaidi ya matarajio yetu. Hakika BWANA ni mwema na fadhili zake ni za milele.

5.IBADA YA SHUKRANI 

Tunamshukuru Mungu aliyefanikisha kwa viwango vikubwa kupatikana kwa fedha kwa ajili ya kununulia vyombo au vifaa vya kuhubiria Injili katika mikutano ya nje Vudee na Ndolwa. Kamati iliandaa ibada ya shukrani kwa Mungu tarehe 24/07/2022 katika Kanisa la Azania Front. Ibada hiyo iliongozwa na Mwinjilisti Jonas Gwemelo ambapo tulimsifu Mungu kwa neno, nyimbo na sadaka; kwa kuwa alikuwa pamoja nasi. Tukakiri kuwa Hakuna jambo lililo gumu la kumshinda BWANA. 

6.UNUNUZI WA VYOMBO/ VIFAA. 

Kamati ilinunua vyombo na vifaa vyote hapa Dar es salaam na kuvisafirisha hadi Vudee. Vyombo/ vifaa hivyo viliwekwa wakfu na Mhe. Baba Askofu Charles Mjema wa KKKT – Dayosisi ya Pare katika ibada ya ufunguzi wa mkutano wa Injili Vudee tarehe 18/09/2022. Tunamshukuru Mungu kwa kutupatia Vyombo / vifaa vitakavyotumika kwa utukufu wake.

7.USHUHUDA. 

Wote tumeshuhudia muujiza huu alioufanya BWANA mbele ya macho yetu. Katika muujiza huu Mungu alijitukuza mwenyewe katika neno lake kwamba, Hakuna Neno lililo gumu la kumshinda BWANA. Nasi tunalihimidi Jina Lake maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu na uaminifu wa BWANA ni wa milele. Haleluya.

8.MAOMBI NA TOBA. 

Tumuombe Mungu aendelee kututumia katika shamba lake kwa kuwa tunajua ya kuwa mavuno ni mengi na watenda kazi ni wachache. Tumwombe Mungu atutume sisi nasi tuwe tayari kwenda. Tuimbe wimbo Na 390 BWANA asema nimtume nani kutoka kitabu cha Tumwabudu Mungu wetu. 

Tunafahamu kuwa katika kipindi chote cha maandalizi inawezekana kwamba tulimkosea Mungu kwa njia moja au nyingine kwa kuwaza, kwa kunena na kwa kutenda. Nakumbuka tukiwa Vudee wakati wa kujaribisha vyombo vijana walifunga umeme moja kwa moja kwenye nguzo ya TANESCO bila kupitia kwenye mita. Hili lilikuwa kosa la kuiba umeme wa TANESCO. Hili lilifanyika mbele yangu nikiona na sikulikemea. Leo ninaomba tufanye TOBA kwa yale yote ambayo hayakumpendeza Mungu ili atuhurumie, aturehemu na atusamehe dhambi zetu zote. Atusafishe kwa damu ya Mwanae Yesu Kristo na atupe neema ya Roho Mtakatifu wake. Tuimbe wimbo No 136 Njoo kwetu Roho mwema katika kitabu cha Tumwabudu Mungu wetu. 

9.HITIMISHO 

Ndugu zangu wacharo nawashukuru sana kwa jinsi mlivyojitoa kwa BWANA kuifanya kazi hii, mlitoa muda wenu mlitoa rasilimali zenu na zaidi sana mlimtolea BWANA sadaka kwa moyo wa kupenda. Namshukuru Mungu kwa kuwa sikujuta hata mara moja kuwa Mwenyekiti wa shughuli hii, mlinitia moyo na tulitembea pamoja kwa furaha na kicheko. Nina furaha kubwa juu yenu na zaidi sana juu ya BWANA wetu Yesu Kristo. Nawakaribisha tupongezane kwa makofi na vigelegele. Tumshangilie Mungu kwa kuimba wimbo Na 391 na Na 180 katika kitabu cha Tumwabudu Mungu wetu. 


_____________________________________________________________________


Share This