TATHIMINI YA MKUTANO WA INJILI ULIOFANYIKA KATIKA USHARIKA WA VUDEE TAREHE 15/09/2019-22/09/2019
UTANGULIZI
Wacharo wa Vudee (wanaoishi nje ya Vudee )waliandaa mkutano wa Injili katika vituo viwili vya Vudee kati (missioni) na Ndolwa kuanzia tarehe 15/09/019-22/09/2019 .Neno kuu la mkutano lilitoka 2 Mambo ya Nyakati 7:14.
Ikiwa watu wangu walioitwa kwa jina langu ,watajinyenyekesha na kuomba na kunitafuta uso na kuziacha njia zao mbaya basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao,na kuiponya nchi yao .Neno hili ndilo lililoongoza mafundisho katika mkutano huu.Wanenaji katika mkutano huu walikuwa Mch.Samson Mbwambo, Mtumishi Tunzo N. Mnzava,Mtumishi Tumainieli Mbwambo na Mtumishi Nico(Kenneth)M.Shaidi.Waimbaji walioongoza katika kumsifu na kumwabudu Mungu ni Praise and Worship Team,na kwaya za Usharika wa Vudee. Waimbaji binafsi walikuwa Tinna Mnzava,Eliyuko Mnzava na Danieli (Hassani) wa Ndolwa. Tunawashukuru wanenaji wa Neno pamoja na waimbaji wote kwa kazi nzuri waliyofanya.
1. Mgeni Rasmi.
Katika mkutano huu mgeni rasmi alikuwa msaidizi wa Askofu wa kanisa la KKKT-Dayosisi ya Pare Mch.Ibrahim Ndekia ambaye alifungua mkutano katika vituo vyote viwili vya Ndolwa na Vudee-Kati ,Aliyefunga mkutano alikuwa ni Mkuu wa Jimbo la Tambarare kanisa la KKKT-Dayosisi ya Pare Mch.Senkoro.Tunawashukuru kwa kukubali wito wetu wa kuhudumu katika nafasi hizo,kipekee tunampongeza Mch.Mpinda wa Usharika wa Vudee kwa kusimamia shughuli zote katika mkutano huu na kuhakikisha kuwa ratiba ya mkutano inazingatiwa.
2.0. Kamati za maandalizi
Ziliundwa kamati kuu tatu kamati ya maombi, kamati ya uratibu na kamati ya chakula. Tunamshukuru Mungu kwa kazi nzuri ya kumtumikia iliyofanywa na wanakamati.Mkutano huu ulisimamiwa vyema na uongozi wa Wacharo- Dar es salaama chini ya Mwenyekiti wake Dr.Ahadieli Senkoro,Mtunza Fedha Kazeni H.Mnzava na Katibu Julius M.Shaidi .Mungu awabariki kwa kujitoa kwao kumtumikia kwa uaminifu.Taarifa ya tathimini ilifanyika katika kikao cha Wacharo tarehe 27/10/2019 kwa kuzingatia kamati kuu za mkutano.
2. Kamati ya Maombi
Kamati ya maombi ya Wacharo iliongozwa na Mtumishi Nico.M Shaidi.Kamati hii iliundwa na wacharo na kamati za maombi za Usharika wa Vudee.Kamati ya Vudee ilishirikisha waombaji kutoka madhehebu mengine kando ya kanisa la KKKT.Kamati ya maombi Vudee iliongozwa na Mwenyekiti Mbonea Mbazi. Kamati hizi kwa ushirikiano mkubwa walifanya maombi mchana na usiku na siku zingine walifanya maombi ya kufunga.Walifanya maombi kanisani, majumbani na katika viwanja vya mkutano.Tunawashukuru sana kwa kubeba mzigo huu wa maombi kwa ajili ya mkutano ili mkutano umzalie BWANA matunda mema.
3. Kamati ya Uratibu
Kamati ya uratibu ilikuwa na kazi kubwa ya kuratibu shughuli zote katika mkutano huu.Majukwaa yote mawili yalijengwa Vudee kati na Ndolwa na kupambwa kwa vitambaa vizuri na maua ya kupendeza.Kamati ilihakikisha kuwa wanenaji na waimbaji pamoja na vifaa vya muziki vinafika vituoni kwa wakati. Vyombo vya muziki vilivyopangwa kununuliwa vilinunuliwa .Kamati hii iliundwa na wacharo pamoja na washarika wa Vudee wakiongozwa na Mwenyekiti mama Grace Mbazi. Kamati ya Uratibu imeandaa picha za mnato na picha za video za tukio hili kubwa. Kikao kimeweka utaratibu mzuri wa jinsi ya kutunza kumbukumbu hizi kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.Tunamshukuru Mungu kwa ushirikiano ulioonyeshwa katika kamati hii.
2.3Kamati ya chakula
Kamati ya chakula ya Vacharo kwa kushirikiana na kamati ya usharika wa Vudee iliongozwa na Mwenyekiti Mama Bertha Tajaeli. Kamati ilihakikisha kuwa wageni wote wamehudumiwa kwa chakula na vinywaji kulingana na bajeti iliyowekwa.Wapishi watatu kutoka Same walihusika na huduma ya mapishi kwa siku zote nane.
(8).Tunawashukuru kwa kazi nzuri waliyofanya.
3. Sadaka
Katika mkutano huu wakristo walitoa aina mbili za sadaka.Siku ya Alhamisi tarehe 19/09/2019 wakristo walitoa sadaka baada ya kufanya Toba.Wakristo walitoa sadaka ya vitu hai kama vile kuku na mazao kutoka mashambani mwao pamoja na fedha.Siku ya terehe 22/09/2019 wakristo walitoa sadaka ya shukrani.Hii ilikuwa ndio siku ya kilele na ya kufunga mkutano. Jumla ya sadaka iliyopatikana katika kituo cha Vudee kati ni Tsh 1,865,050 na Ndolwa 438,500 na kufanya Jumla kuu ya sadaka iliyotolewa kwa BWANA kuwa ni Tsh 2,303,550.Tunamshukuru Mungu kwa wale wote waliomtolea kwa moyo wa upendo, unyenyekevu na shukrani.
4. Taarifa ya Fedha
Katika kikao hiki Mtunza Fedha wa Wacharo wa Dar es salaam ameandaa taarifa ya fedha ambayo imeambatishwa. Kikao kiliridhishwa na utunzaji wa michango yote iliyotolewa pamoja na matumizi yake.Kikao kilijiridhisha kuwa matumizi yalizingatia bajeti iliyopangwa. Kikao kiliazimia kuwa wale wote walioahidi wajitahidi kutimiza ahadi zao kwa kuzituma kwa Mtunza fedha Kazeni H.Mnzava-0787671212.Fedha hizo pamoja na zingine zitatumika katika mikutano ijayo.
5. Kikao cha Tathimini
Kikao cha tathimini kilifanyika tarehe 27/10/2019 chini ya Mwenyekiti wa Vacharo Dr. Ahadieli R.Senkoro.Kikao kilifunguliwa kwa sala iliyoongozwa na Mtumishi Elineema Mdee.Wajumbe walimsifu Mungu kwa kuimba nyimbo namba 121 na 129 kutoka kitabu cha Kipare cha Ngazo ya Mrungu.Mwimbaji binafsi Tinna Mnzava aliimba wimbo wake maarufu unaojulikana kwa jina la Wafunge midomo yao.Baada ya kujadili utumishi wa Kamati zote tatu mambo yafuatayo yalipendekeza.
· Picha za mnato na za video zitunzwe katika ofisi ya usharika wa Vudee,wale wote watakaohitaji nakala binafsi wawasiliane na Vincent M.Shaidi 0782788816
· Kamati ya maombi ya Ndolwa ilisifiwa kwa kazi kubwa waliyofanya .Kamati ya Vudee kati ilionekana kuwa haikuwa na watu wengi kama ilivyotarajiwa. Kamati ya maombi ya Wacharo ilisifiwa sana kwa kuamka usiku na kudumu katika maombi.
· Ilipendekezwa kuwa ni vyema mnenaji akapewa nafasi ya kuhudumu katika kituo kimoja mfululizo kwa siku tatu au zaidi ili kutokatisha mafundisho.
· Kuwe na semina kwa ajili ya kuwatunza na kuwaimarisha wakristo waliookoka ,kila Mtaa uandae semina za kuimarisha wakristo waliokata shauri.
· Kuwe na semina za mafundisho ya Neno la Mungu kwa makundi mbalimbali ndani ya kanisa kama vile vijana, wanawake (wasichana) na wababa.
· Kila mtaa uandae mkutano wa Injili au mikutano ya Injili na Usharika uandae mikutano miwili ya Injili mwezi wa nne na wa tisa. Wacharo watashiriki kuwezesha mkutano wa mwezi wa tisa kila mwaka, ingawaje watu binafsi wanaweza kushiriki katika kuwezesha mikutano ya mitaa.
· Mtunza ratiba amiliki muda ipasavyo ili muda uliotengwa kwa ajili ya mahubiri,maombi na maombezi utoshe.
· Kikao kilisifu wazo la kuwa na kambi ya mombi na utaratibu mzima wa mkutano kwa kufikia mahali pamoja.
· Maandalizi ya mkutano yaanze mapema kila mwaka ili kuwa na wakati wa kutosha kwa ajili ya kutoa michango
6. Changamoto
Kikao kiliainisha changamoto mbalimbali zilizojitokeza na kushauri ipasavyo.
· Changamoto ya ukatikaji wa umeme inatakiwa kuangaliwa kwa kuhakikisha kuwa generator zimeandaliwa na kuwekwa mafuta wakati wote wa mkutano.
· Kwaya za Usharika ziandaliwe mapema ili ziweze kushiriki ipasavyo.
· Vyombo vya kwaya vilivyopo chini ya usimamizi wa mitaa viandaliwe mapema na kuwasilishwa usharikani kwa ajili ya kazi ya Mungu.
7. Hitimisho
Tunamshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo alijifunua kwetu na kwa watu wake.Katika mkutano huu watu walikata shauri, waliponywa magonjwa na Mungu ameiponya nchi ya Vudee.Tunamrudishia sifa,utukufu na enzi kwa kuwa anastahili yeye peke yake.
Tunawashukuru watu wote waliojitolea kwa hali na mali kufanikisha mkutano huu.Tunawashukuru wanenaji wote kwa kujitolea kwao kuhudumu nyumbani kwao.Tunawashukuru wana maombi wote na kipekee tunamshukuru Elia Kisimbo na familia yake kutoka Korogwe waliohudumu katika kikundi cha maombi Ndolwa kwa siku zote nane za mkutano. Mungu awabariki ninyi nyote mliojitoa kumtumikia.
Picha na Video ya tukio hili zinapatikana kwa kubovya link hii hapa- BOFYA HAPA