• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

ULINZI WA MUNGU KWETU

Tunamshukuru Mungu kwa kuzidisha uzao wetu na kuulinda. Katika maisha yetu yote tumeshuhudia ulinzi wa Mungu kwetu. Mungu ndiye alindaye hakuna mwingine awezaye kulinda isipokuwa Yeye peke yake. 1 Petro 1:5 “Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho”. Wala hakuna mtu awezaye kutupokonya katika mkono wa BWANA. Hakika mkono wa BWANA si mfupi hata ushindwe kuokoa. Tunaomba ulinzi wa Mungu kwetu na kwa vizazi vyetu kwa kuwa BWANA ni mwaminifu na wa haki. 2 Wathesalonike 3:3 “lakini BWANA ni mwaminifu atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu”. Tunamwomba Mungu awe mlinzi wetu, atulinde na mabaya yote, azilinde nafsi zetu. BWANA atulinde tutokapo na tuingiapo. BWANA atutie nguvu, atusaidie na atushike kwa mkono wa kuume wa haki yake. Tunamwomba Mungu ulinzi wa nyumba zetu, familia zetu na miji yetu. Zaburi 127:1 “BWANA asipojenga nyumba waijengao wafanya kazi bure, sisi hatutakesha bure kwa kuwa tutakukimbilia wewe. Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso. Hatutaogopa kwa sababu BWANA wa majeshi yu pamoja nasi Mungu wa Yakobo ni ngome yetu. BWANA anatuambia wana wa Marko’s tusiogope tusonge mbele. Tusiogope kwa sababu BWANA wa majeshi yupo pamoja nasi, atatulinda, atatupigania. Zaburi 121: 3-5, 7 “Asiuache mguu wako usogezwe, asisinzie akulindaye, Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi. Yeye aliye mlinzi wa Israel. BWANA ndiye mlinzi wako, BWANA ni uvuli mkono wako wa kuume. BWANA atakulinda na mabaya yote, atakulinda nafsi yako. BWANA atakulinda utokapo na uingiapo, tangu sasa na hata milele.

Zaburi 27:1, 4 “BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, nimhofu nani? Neno moja nimelitaka kwa BWANA, nalo ndilo nitakalolitafuta, nikae nyumbani mwa BWANA siku zote za maisha yangu. Niutazame uzuri wa BWANA, na kutafakari hekaluni mwake”.

BWANA sikia kuomba kwetu AMEN.

Share This