TUNAMWOMBA MUNGU TUWE WATEULE WAKE.
Wateule wa Mungu ni watu ambao Mungu amewatenga wao na mataifa au amewatenga na uovu wote, dhambi na machukizo ya kila aina. Hawa ni watu walioteuliwa na Mungu mwenyewe kwa neema ya wokovu. Kwa maana nyingine wateule ni wale waliovua mwenendo wa kwanza na kuvaa utu mpya ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika hali na utakatifu wake wa kweli (Waefeso 4:22). Wamevua utu wa kale pamoja na matendo yake, hawa ndio wale walioonekana kumkiri Yesu Kristo kuwa ni Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Hawa wamekuwa tunu kwa Mungu kwa maana wametii sauti ya Mungu na kulishika neno lake. Hawa ni wale wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu wake. Zaburi 16:3 “Watakatifu waliopo duniani ndio walio bora, hao ndio niliopendezwa nao”. Wakolosai 3:12 “Basi kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana na kusameheana”. Zaidi ya hayo yoye jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Iweni na imani ya Kristo Yesu mioyoni mwenu na tena iweni watu wa shukrani kwa Mungu. Marko 13: 27 “Ndipo atakapowatuma malaika na kuwakusanya wateule wake toka pepo nne, toka upande wa mwisho wa nchi hata upande wa mwisho wa mbingu”. Mungu amewahesabia haki na akawatukuza kwa hiyo hakuna anayeweza kuwashitaki wateule wa Mungu.
Warumi 8:33 “Ni nani atakaye washitaki wateule wa Mungu? Mungu ndiye mwenye kuwahesabia haki”. Na sisi ndugu zangu tunaotoa shukrani zetu kwa Mungu tuombe neema hii ya Mungu ili tuwe wateule wake tutakaokuwa pamoja na Mwanakondoo, Bwana wa Mabwana na Mfalme wa Wafalme atakapokuja kulichukua kanisa lake.