• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

TUNAMSHUKURU MUNGU KWA NEEMA YA WOKOVU

Tunamshukuru Mungu kwa unyenyekevu sana kwa kuwa neema ya wokovu imefunuliwa kwetu sisi na kwa watu wote. Tito 2:11 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa.” Neema hii ni zawadi au upendeleo wa kuchaguliwa pasipo kustahili tena bure si kwa sababu ya matendo yetu bali kwa Yesu Kristo Bwana wetu. Neema ya Mungu inatufundisha kuacha ubaya na tamaa za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa (Tito 2:12). Tunaokolewa kwa neema ya Mungu, wala si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi, bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa mara ya pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu, ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu, ili tuhesabiwe haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini   letu (Tito 3:4-7). Waefeso 2:8-9 "Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zetu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu." Tunapataje wokovu? Tunaokolewa kwa njia ya imani. Warumi 10:9-10 "Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka." Kwa kuwa, kila atakayeliitia jina la Bwana ataokoka. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu, litupasalo sisi kuokolewa kwalo. (Matendo ya Mitume 4:12) Ole wetu tusipojali wokovu mkuu namna hii. Bwana wetu Yesu Kristo ametukomboa kwa hiyo, wewe si mtumwa tena bali ni mwana, na kama ni mwana, basi, u mrithi kwa Mungu (Wagalatia 4:7). Ni wajibu wetu sisi sote tunatoa sadaka zetu za shukrani kuamini, kuheshimu, kupokea na kuishi katika neema hii ya wokovu ya Yesu Kristo Bwana wetu. Tunamshukuru Mungu kwa maana hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu bali uokolewe katika yeye. Amina.

Share This