TUNAKATAA NA KUJITENGA NA IBADA ZA MIUNGU NA SANAMU
Wapare kama jumuiya ya watu wenye historia moja na utamaduni mmoja kabla ya Ukristo kufika Upareni waliabudu miungu yao. Hata katika maandiko matakatifu ya Biblia utasoma kuhusu makabila au koo mbalimbali zisizomcha Mungu zilikuwa na miungu yao, kwa mfano miungu ya Waamori, miungu ya Wakaldayo, miungu ya Wafilisti nakadhalika. Koo za Kipare zilikuwa na zingine bado zinatumia misitu au mawe/miamba mikubwa kama maeneo yao ya ibada au matambiko. Kwa hiyo utasikia kuhusu msitu wa Wagonja, Wanzava, Wakramweni, Wambughu na mingine mingi. Uzao wa Shaidi ni uzao wa Kipare unaojulikana kama Wachome Waviombo. Msitu wa Wachome Waviombo (Vyachome Vyaviombo) uko Chome eneo la Mpeta. Tunamshukuru sana Mungu kwa kuwa mzee Shaidi Nziamwe baada ya kupata neema ya ubatizo na kuwa Mkristo yeye na watoto wake waliachana na ibada za miungu ya Vachome Vyaviombo. Na sisi wa uzao wake tunakataa na kujitenga na ibada za sanamu na miungu popote pale zinapofanyika. Uzao wetu wala majina yetu yasitajwe huko. Kwa kuwa tunajua kuwa matambiko na kuabudu miungu ni machukizo mbele ya Mungu tunayemwabudu. Neno la Mungu katika Kutoka 20:3-6 linasema, “Usiwe na miungu mingine ila mimi”. Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu chochote kilicho mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia. Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, BWANA, MUNGU wako ni Mungu mwenye wivu, nawapaliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao, nami nawarehemu maelfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”. Sisi tunaompenda Mungu na kuzishika amri zake na tuliotayari kumtolea Mungu sadaka za shukrani tunainua na tunasimamisha mioyoni mwetu madhabahu ya Mungu wetu aliye hai na aliye juu ya vitu vyote. Kila mmoja wetu asimamishe jina la BWANA katika madhabahu ya moyo wake. Damu ya Yesu Kristo na Jina la Yesu Kristo kwa njia ya maombi ya Toba na rehema tunatupa nguvu na uhalali wa kukataa na kujitenga na ibada za miungu na sanamu. Waebrania 12:24 na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili”. Wakolosai 3:17 ‘’Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye’’. Tutasogeza sadaka zetu za shukrani madhabahuni pake ili kwamba tupate kukubaliwa. Yeye ndiye tutakayemcha, yeye ndiye tutakaye msujudia, yeye ndiye tutakaye mtolea sadaka zetu za shukrani. Tunamshukuru Mungu aliye tuokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake; ambaye katika yeye tunaukombozi, yaani msamaha wa dhambi (Wakolosai 1:13-14). Je, haya sio matendo makuu na ya ajabu tunayotakiwa kusimulia vizazi vyetu? Wana wa Israeli wanasimulia jinsi Mungu alivyo watoa utumwani Misri na sisi tunasimulia na kumshukuru Mungu jinsi alivyo tutoa kutoka utumwa wa dhambi na kutuingiza katika ufalme wake. Simulizi zote hizi ni kwa ajili ya kumshukuru Mungu, kumrudishia sifa, heshima na utukufu. Atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.