TUNAMWOMBA MUNGU TUWE MZAO MTEULE KWAKE
Tunajifunza katika neno la Mungu kuwa uzao wa baba yetu wa imani Ibrahimu ni mzao teule kwa BWANA. Mungu alimbariki kwa kumfanya awe na uzao mwingi sana, akamzidisha na kumwongeza. Mungu akafanya agano na Ibrahimu kuwa atakuwa baba wa mataifa mengi na wafalme watatoka kwake. Mwanzo 17:7 “Agano langu nitalifanya imara kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako na vizazi vyao kuwa agano la milele”. Hata sisi tumerithi baraka za Ibrahimu, katika Mwanzo 22:18 “Na katika uzao wako mataifa yote ya dunia watabarikiwa, kwa sababu umetii sauti yangu”. Bwana wetu Yesu Kristo ni uzao wa Ibrahimu. Waebrania 2:16 “maana ni hakika hatwai asili ya malaika, ila atwaa asili ya mzao wa Ibrahimu”. Wagalatia 3:16 “Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa uzao wake. Hasemi, kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, kwa mzao wako, yaani Kristo”.
Kwa kuwa tunamwamini Yesu Kristo na sisi ni mzao mteule kwa Bwana. Warumi 8:17 “na kama tu watoto basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo, naam, tukiteswa pamoja nae ili tupate kutukuzwa pamoja nae”. 1 Petro 2:9 “Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu”. Je wewe na mimi tuko tayari kuzitangaza fadhili za Mungu, kwa vizazi vyetu na kwa watu wote?
Mfalme Daudi katika Zaburi 89:1 anasema, “Fadhili za Bwana nitaziimba milele, kwa kinywa changu nitavijulisha vizazi vyote uaminifu wako”. Mungu ni mwenye fadhili nyingi na fadhili zake hazikomi, huruma zake hazina mwisho kila kunapokucha ni mpya kabisa, uaminifu wake ni mkuu mno.
Ukimtii Bwana Mungu wako kwa bidii na ukifuata maagizo yake yote utabarikiwa uzao wa tumbo lako, na uzao wa nchi yako yote, na uzao wa wanyama wako wa mifugo, maongeo ya ng’ombe wako na wadogo wa kondoo zako (Kumbukumbu la Torati 28:4). Na sisi sote tunaomtolea Mungu sadaka zetu za shukrani,tunamwomba Mungu uzao wetu na vizazi vyetu tuwe mzao mteule kwake, atubariki, atuzidishe na kutuongeza sawa sawa na Neno Lake. Amen