NIPE ULIMI MPYA
Bwana wetu Yesu Kristo tunakuomba umpe kila mmoja wetu ulimi mpya. Wote tunafahamu kazi ya ulimi kuwa ni kutamka maneno (kusema, kuongea, kunena) na kuimba mambo mazuri au mabaya. Ulimi uko ndani ya kinywa chako kwa hiyo maneno hutamkwa kupitia kinywa chako. Ulimi una nguvu za kubariki au kulaani, nguvu za uzima na mauti (Mithali 18:21). Ikiwa ulimi una nguvu kubwa namna hii kuna haja ya kujua namna sahihi ya kuutumia.
Yakobo 3:8-9 “Bali ulimi hakuna awezaye kuufuga: ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti. Kwa huo twamhimidi Mungu Baba yetu, na kwa huo twalaani wanadamu waliofanywa kwa mfano wa Mungu. Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu haifai mambo hayo kuwa hivyo”. Katika somo hili tutatafakari zaidi maneno unayoyasema wewe mwenyewe na sio yale unayonenewa na watu wengine.
Kutumia ulimi vibaya
Ulimi ni kiungo kidogo kiwezacho kuwasha moto wa uharibifu. Yakobo 3:5-6 “Vivyo hivyo ulimi nao ni kiungo kidogo, nao hujivuna majivuno makuu. Angalieni jinsi moto mdogo uwashavyo msitu mkubwa sana. Na ulimi ni moto, ule ulimengu wa uovu, ule ulimi umewekwa katika viungo vyetu, na ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwasha moto na jehanum”.
•Usijinenee maneno mabaya yaani usikiri udhaifu wako kama vile kusema sina uwezo wa kufanya jambo hili wakati unajua ni jambo jema, mimi sitapona ugonjwa huu, ninaogopa kujaribu na mambo mengine mengi mabaya. Maneno mabaya unayo jinenea yanaweza kuathiri vibaya mwenendo wako wa maisha. Shetani anafuatilia maneno mabaya unayoyanena na kuhakikisha kuwa yanatimia au yanatokea kama ulivyosema au ulivyokiri. Mithali 6:2 “Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako. Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako”.
•Usiwanenee maneno mabaya watu wengine. Ukimnenea mtu maneno mabaya unaamsha roho ya kisasi na uharibifu. Uharibifu kwenye maisha yako binafsi na si tu kwa yule ambaye unamwelekezea maneno hayo. Mithali 13:3 “Yeye alindaye kinywa chake huilinda nafsi yake; bali afunuaye midomo yake atapata uharibifu”.
Maarifa ya kushindana na ubaya wa ulimi
Neno la Mungu linatufundisha maarifa ya kushindana na ubaya wa ulimi.
•Jifunze kunyamaza unapogundua kuwa maneno yako yatamjeruhi mwenzako, maneno yako yataleta picha mbaya isiyo na utukufu mbele za Mungu. 1 Wakorintho 15:33 “Msidanganyike; mazungumzo mabaya huharibu tabia njema”.
•Jifunze kuzuia maneno mabaya yasitoke kinywani mwako kama vile kusema uongo, matusi, masengenyo, majivuno, manung’uniko na mengine mengi ya aina hiyo. Uwe mtu aendaye kwa ukamilifu na kutenda haki. Asemaye ukweli kwa moyo wake. Zaburi 15:3 “Asiyesingizia kwa ulimi wake. Wala hakumtenda mwenziwe mabaya, wala hakusengenya jirani yake”.
•Jifunze kunyamaza unapokuwa na hasira ili kuilinda nafsi yako na taabu. Waefeso 4:26 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka, wala msimpe Ibilisi nafasi”. Hasira ni mlango wa shetani unaotuingiza katika kusema mambo bila kutumia akili. Mithali 14:17 “Yeye aonaye hasira upesi atatenda kwa ujinga; na mtu mwenye hila mbaya huzirwa”. Mtu wa hasira huchochea ugomvi; bali asiye mwepesi wa hasira hutuliza mashindano (Mithali 15:18).
•Jiepushe na maneno ya mzaha ili usije ukahukumiwa. Mithali 19:29 “Hukumu zimewekwa tayari kwa wenye mzaha; na mapigo kwa mgongo wa wapumbavu”. Jiepushe na mizaha ambayo inamdhalilisha Mungu, wewe mwenyewe na familia yako. Heri mtu yule asiyeketi barazani pa wenye mizaha.
•Jiepushe kusema maneno mabaya na hila. 1 Petro 3:10 “Kwa maana, atakaye kupenda maisha, na kuona siku njema, auzuie ulimi wake usinene mabaya, na midomo yake isiseme hila”.
•Jiepushe na maneno ya upuuzi, machafu na ya aibu. 2 Timotheo 2:16 “Jiepushe na maneno yasiyo na maana, ambayo si ya dini, kwa kuwa wataendelea zaidi katika maovu. Tena maneno ya upuuzi wala ubishi, hayo hayapendezi; bali afadhali kushukuru”, (Waefeso 5:4). Mhubiri 10:13 anasema, “Mwanzo wa maneno ya kinywa chake ni upuuzi; na mwisho wa usemi wake ni wazimu wenye hatari”. Jiepushe na maneno yasiyompa Mungu utukufu.
Kutumia ulimi vizuri
Mungu ametuumba kwa mfano wake akatupa ulimi na kinywa ili tuwabariki wengine, tuwafundishe neno lake la uzima na imani ya Kikristo. Tutumie ulimi kwa kusali, kuabudu, kusifu, kuomba na kushukuru. Autumiaye ulimi wake vizuri huyo ni mkamilifu mbele za Mungu. Yakobo 3: 2(b) “Mtu asiyejikwaa katika kunena huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu”. Ili uweze kuwa mkamilifu na uweze kutumia ulimi wako vizuri unahitaji kuwa na maarifa ambayo yanapatikana katika neno la Mungu.
•Tumia ulimi wako kubariki wengine
Mungu anataka tuwabariki watu wake. Hesabu 6:23 “Nena na Haruni na wanae, hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israel, mtawaambia; Bwana akubariki na kukulinda; Bwana akuangazie nuru ya uso wake, na kukufadhili; Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani”. Tuwabariki watu kwa kuwapa vitu wanavyohitaji katika maisha yao. Wafilipi 2:4 “Kila mmoja wenu asiangalie mambo yake mwenyewe tu, bali pia ajishughulishe kwa faida ya wengine”. Jinsi unavyo wabariki watu ndivyo hivyo hivyo Mungu atakubariki na wewe. Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa, kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”. Umebarikiwa ili uwabariki wengine.
•Tumia ulimi wako na kinywa chako kuwafundisha watu neno la Mungu liletalo uzima wa milele.
Watu wamjue Mungu wa pekee na wa kweli ili waokoke na kumkubali Yesu Kristo kuwa Bwana na Mwokozi wa maisha yao. Yohana 14:6 “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima, mtu haji kwa Baba ila kwa njia ya mimi”. Mungu ameonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu na kwa ajili ya ukombozi wetu. Tumekombolewa kwa damu ya thamani, kama ya Mwanakondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani Kristo. Tufundishe kwa bidii kama alivyofanya Bwana wetu Yesu Kristo. Ili uweze kufundisha vyema; Jaza mafundisho ya neno la Mungu moyoni mwako, kwa kuwa yale yaujazayo moyo wa mtu ndiyo yanayomtoka. Neno la Mungu likae kwa wingi ndani yako. Neno la Bwana hudumu hata milele.
•Tumia ulimi wako kusifu na kuabudu
Mtumishi wa Mungu mfalme Daudi alijua umuhimu wa kumpa Mungu sifa na utukufu. Zaburi 71:8 “Kinywa changu kitajazwa sifa zako, na heshima yako mchana kutwa”. Daudi anasema, kinywa chake kitasimulia haki na wokovu wa Mungu mchana kutwa. Zaburi 35:28 “Na ulimi wangu utanena haki yako, na sifa zako mchana kutwa”. Tumwimbie Mungu nyimbo na zaburi za sifa na za kuabudu siku zote za maisha yetu. Tumwabudu Mungu katika roho na kweli. Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli. Luka 4:8 “Yesu akajibu akawaambia, Imeandikwa Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke ake”.
•Tumia ulimi wako kuomba na kushukuru
Mungu anatukaribisha tumwombe jambo lolote lile naye atalifanya. Yohana 14:13-14 “Nanyi mkiomba lolote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili Baba atukuzwe ndani ya Mwana. Mkiomba neno lolote kwa jina langu, nitalifanya”. Tukikaa ndani ya Yesu na tukilishika neno lake anasema tuombe tutakalo naye atatutendea. Tunatakiwa tuombe kwa imani na kuamini kuwa hayo tunayoyaomba yatatokea. Marko 11:24 “Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu”. Ikiwa tutapata hayo yote tuombayo hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kuwa Mungu ni mwema na fadhili zake ni za milele. Ulimi wangu utasimulia matendo yake makuu na ya ajabu kwetu. Nitasimulia kwa furaha, vicheko na kelele za shangwe. 1 Wathesalonike 5: 16-18 “Furahini siku zote; ombeni bila kukoma, shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu”. Ndugu zangu kila mmoja wetu amwombe Mungu ampe nguvu ya kuomba kwa roho, tena kuomba kwa akili pia, kuimba kwa roho, tena kuimba kwa akili pia.
•Je, ni maneno gani yanayotoka kinywani mwako?
Maisha ya mtu yanachangiwa kwa sehemu kubwa na maneno yake mwenyewe, akiutumia vizuri ulimi wake ataishi vizuri lakini akiutumia ulimi wake vibaya mabaya yatakuwa juu yake, huyu anahitaji ulimi mpya kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Ulimi mpya unapatikana kwa maombi ya toba na rehema. Nenda mbele za Mungu umwombe Mungu akusamehe dhambi zote zinazotokana na ulimi wako na umwombe akurehemu na akupatie uwezo wa kuzuia ulimi wako. Maneno ya kinywa chako na mawazo ya moyo wako yapate kibali mbele za Mungu.
•Maombi ya toba na rehema.
Mungu mwenye enzi yote, muumba wa mbingu na nchi ninakuja mbele zako kwa toba na rehema. Nimekutenda dhambi kwa maneno yangu, fikra zangu na matendo yangu. Ninazijutia dhambi zangu na kutubu kweli. Ninajua wewe ni Mungu mwenye rehema nyingi, ninakuomba unirehemu unisamehe dhambi zangu zote. Ninakuomba unirehemu unitakase moyo wangu na nia yangu kwa damu ya Yesu Kristo, Mwanakondoo wa Mungu aichukuaye dhambi ya ulimwengu. Uniondolee mbali maneno mabaya yanayotoka kinywani mwangu ili niweze kukukaribia katika maombi yangu, nikuabudu katika roho na kweli
Bwana wangu Yesu Kristo ninakuomba unirehemu unipe uwezo wa kudhibiti ulimi wangu na kunikomboa kutoka katika roho ya kujiangamiza. Unisafishe ulimi wangu kutoka kwenye kila uchafu. Nipe ulimi mpya uliokombolewa kwa damu yako ya thamani iliyomwagika pale msalabani Calvary. Ulimi wangu mpya utakupa wewe Mungu wangu sifa,heshima na utukufu.
Ninakushukuru kwa kuwa wema na fadhili zako kwangu ni nyingi na za milele. Naomba niwe baraka kwa wengine. Naomba niwe daraja kwa wote ili waje kwako. Nisiwe sababu ya wengine kuumia, kukwazika wala nisiwe sababu kwa wengine kuteseka kwa sababu ya maneno ya kinywa changu. Maneno ya kinywa changu, na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako. Kinywa changu kisimulie haki na wokovu wako na ulimi wangu unene haki yako na sifa zako mchana kutwa. Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu. Mngojezi mlangoni pa midomo yangu ili nisikutende dhambi. Roho Mtakatifu karibu ndani yangu na mimi niwe ndani yako ili unisaidie na uniongoze katika haki yote kwa jina la Yesu, jina lipitalo majina yote mbinguni na duniani. Utukufu una wewe na ukuu na uweza na nguvu, tangu sasa na hata milele. AMINA.
Share This