NGUVU YA NENO LA SHUKRANI NA SADAKA YA SHUKRANI KWA MUNGU
Kushukuru ni jambo jema mbele za Mungu wetu. Neno la Mungu linatuagiza tushukuru kwa kila jambo kwa maana hayo ndiyo mapenzi ya Mungu. Tunatakiwa tushukuru kwa moyo mkunjufu. Tunatakiwa kumshukuru Mungu kwa matendo yake makuu na ya ajabu kwetu. Tumshukuru Mungu kwa wema na fadhili zake kwetu; amezidisha uzao wetu na kuulinda, ametubariki kwa baraka nyingi tusizoweza kuzihesabu.
· Neno la shukrani lina nguvu ya kuzidisha au kuongeza vile ulivyonavyo. Tunajifunza kwa Bwana wetu Yesu Kristo alipolisha makutano kwa mikate saba (7) na visamaki vichache. Mathayo 15:36(a) “Akaitwaa ile mikate saba na vile visamaki, akashukuru akavimega,” wakawapa makutano, wakala wakashiba. Nao waliokula walikuwa wanaume elfu nne, bila wanawake na watoto.
· Neno la shukrani hufufua na kuvirejesha vitu vilivyokufa kimwili na kiroho. Bwana wetu Yesu Kristo alipomfufua Lazaro aliinua macho yake juu akasema, Baba, nakushukuru kwa kuwa umenisikia (Yohana 11:41-42). Naye akiisha kusema hayo akalia kwa sauti kuu, Lazaro, njoo huku nje. Akatoka nje yule aliyekufa. Tukiamini tutauona utukufu wa Mungu na vitu vyetu vilivyokufa kama vile biashara yako, elimu, ndoa, kazi na chochote kile Yesu Kristo atakifufua. Twendeni kwake kwa moyo wa shukrani.
· Neno la shukrani lina nguvu ya wokovu. Nguvu hii tunaiona wakati Bwana wetu Yesu Kristo alipo waponya wale wakoma kumi, mmoja wao Msamaria ndiye aliyerudi kushukuru (Luka 17:11-19). Akamtukuza Mungu kwa sauti kuu, akaaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru. Bwana wetu Yesu Kristo akamwambia, inuka, enenda zako, Imani yako imekuokoa. Tukiwa na Imani katika Yesu Kristo Bwana wetu na tukimpa utukufu atatuponya miili yetu na roho zetu.
· Sadaka zetu za shukrani tutakazozitoa Vudee tarehe 21/09/2025 zimpe Mungu utukufu ili azitakabali, ziguse moyo wake na ziwe manukato mazuri kwake. Sadaka ya shukrani ikitolewa kwa moyo mkunjufu inagusa moyo wa Mungu na inakuweka karibu na Mungu. Sadaka ya shukrani inakupa kibali mbele za Mungu yaani kukubaliwa.
Mambo ya Walawi 22:29 “Tena mtakapomchinjia BWANA dhabihu ya kushukuru, mtachinja ili mpate kukubaliwa”.
Na sisi tunaotoa sadaka za shukrani tumwombe Mungu azikubali sadaka zetu ili tupate kibali cha kumwabudu katika roho na kweli. Tupate kibali cha kulitangaza jina la BWANA na kuyasimulia matendo yake kwa kuimba. Tutoe sadaka zetu za shukrani kwa roho iliyovunjika; moyo uliovunjika na kupondeka. Tunamshukuru Mungu kwa kumtoa mwanawe mpendwa Yesu Kristo kuwa Pasaka wetu. 1Wakorintho 7(b) “Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo”. Tuenende katika upendo, kama Kristo naye alivyotupenda sisi tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato. Sisi tunaotoa sadaka za shukrani nyumbani mwa BWANA tuseme kwa sauti za furaha na shangwe; “Mshukuruni BWANA wa majeshi, maana BWANA ni mwema, rehema zake ni za milele”. Amen.