• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 26 Nov, 2023
  • Admin

NENO LA MUNGU KUHUSU KIJANA “KUKOLOKA”

Tumeelezea kuwa katika tamaduni za Kipare kijana “anakuloka” pale anapofikia umri wa kuoa. Anatoka katika hatua ya ujana na kuingia katika hatua ya kuwa mtu mzima anayeweza kuruhusiwa na wazazi wake kuoa.

Tumeona pia kuwa anapoomba kwa wazazi wake kuingia katika hatua hiyo ya kuwa mtu mzima kunafanyika uchunguzi ili wazazi waridhike kuwa kijana “amekuloka”. Uchunguzi huu hufanywa kwa kumuuliza kijana maswali mbalimbali yatakayosaidia kuonyesha kuwa “amekuloka”. Katika sehemu hii tutaangalia Neno la Mungu linasema nini kuhusu suala hili la “kukoloka”.  Maswali anayoulizwa kijana yanalenga katika mambo yafuatayo:-

·       Kijana awe mchapakazi hodari, asiwe mvivu;

  • ·       Kijana awe na akiba ya chakula kwa ajili ya dharura kama vile msimu wa ukame na njaa;
  • ·       Kijana apate mke mwema mwenye hofu ya Mungu;
  • ·       Kijana aoe katika familia (au ukoo) unaomwabudu Mungu.
  • ·       Kijana awe na nyumba yake ya kuishi na familia yake.

Kijana awe mchapakazi hodari asiwe mvivu.

Tuangalie Neno la Mungu linasema nini kuhusu kijana kuwa mchapakazi hodari Mithali 20:29. Fahari ya vijana ni nguvu zao. Mtume Paulo anasema amewaandikia vijana kwa sababu wana nguvu na Neno la Mungu linakaa ndani yao nao wamemshinda yule mwovu Mungu hapendezwi na uvivu, alitaka Yoshua awe hodari na shujaa asiwe mtu wa kujihurumia hurumia bali awe mwepesi wa kwenda anakotakiwa, kutekeleza majukumu ambayo Mungu angempa inavyotakiwa kwa wakati unaotakiwa na pasipo hofu. Mithali 21:25 Matakwa yake mtu mvivu humfisha, kwa maana mikono yake hukataa kufanya kazi Mithali 13:23. Alimaye shamba lake kwa bidii atakuwa na chakula tele bali afuataye mambo ya upuuzi hana ufahamu na atapata umasikini wa kumpotosha Neno la Mungu linasema kuwa”kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi” (Mwanzo 3:19).

Neno la Mungu linamtaka kijana afanye kazi kwa juhudi akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. Mtume Paulo naye anaagiza kuwa ndugu wajitahidi kutulia na kutenda kazi kwa mikono yao wenyewe ili waenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala wasiwe na haja ya kitu chochote. Nukuu inayofuata ni mistari ya Biblia kutoka kitabu cha Mithali. Mkono wa mwenye bidii utatawala, bali mvivu atalipishwa kodi.Mtu mvivu hapiki mawindo yake bali mwenye bidii anazo mali za thamani. Nafasi ya mtu mvivu hutamani asipate kitu, bali nafuu ya mwenye bidii itanenepeshwa. Kila aliye na busara hutenda kazi kwa maarifa, bali mpumbavu hueneza upumbavu.Katika kila kazi mna faida bali maneno ya midomo huleta hasara tu. Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake, ni ndugu yake aliyemharibu. Uvuvi humtia mtu katika usingizi mzito na nafsi yake mvivu itaona njaa. Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini, ila hataki hata kuupeleka kinywani pake.Mtu mvivu hataki kulima wakati wa baridi, hivyo wakati wa mavuno ataomba hana kitu.Mtu mvivu husema simba yuko nje nitauwawa katika njia kuu. Nalipita karibu na shamba la mvivu na shamba la mizabibu la mtu asiye na akili kumbe! lote pia limemea miiba, uso wake ulifunikwa kwa viwawi na ukuta wake wa mawe umebomoka. Kijana anayechapa kazi kwa uhodari nyumbani mwake manyasi huchukuliwa, na majani mabichi huonekana na maboga ya milimani hukusanyika. Wanakondoo hufaa kwa mavazi yake na mbuzi ni thamani ya shamba. Tena yatakuwepo maziwa ya mbuzi ya kumtosha kwa chakula chake na chakula cha watu wa nyumbani mwake, na posho la vijakazi vyake.

Je! wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme, hatasimama mbele ya watu wasio na cheo. Mawazo ya wenye bidii huuelekea utajiri tu, bali kila mwenye pupa huuelekea uhitaji. Atendaye mambo kwa mkono mlegevu huwa masikini, bali mkono wake aliye na bidii hutajirisha.

Kijana awe na akiba ya chakula kwa ajili ya dharura kama vile msimu wa ukame na njaa

Neno la Mungu katika Mithali 6:6-8 linasema hivi, “Ewe mvivu mwendee chungu, zitafakari njia zake upate hekima kwa maana yeye hana akida wala msimamizi, wala mkuu, lakini hujiwekea akiba ya chakula wakati wa njaa. Hukusanya chakula chake wakati wa mavuno”. Mitahli 15:6 “Katika nyumba ya mwneye haki mna akiba nyingi bali mapato ya mtu mbaya huwa taabu tupu” Akiba huwekwa wakati wa upatikanaji wa vitu kama vile wakati wa mavuno. Akiba ni msingi mzuri kwa wakati ujao. Mali iliyopatikana kwa haraka itapunguka, bali yeye achumaye kidogo kidogo atazidishiwa. Akusanyaye wakati wa hari ni mwana mwenye hekima, bali asinziaye wakati wa mavuno ni mwana mwenye kuaibisha.

Tujifunze zaidi hekima hii ya kuweka akiba kwa kuangalia mfano wa njaa iliyotabiriwa nchini Misri kupitia ndoto ya Farao (Mwanzo 41:28-36). Yusufu mwana wa Yakobo alitafsiri ndoto ile kwa kumweleza Farao kuwa Mungu amemwonyesha Farao atakayoyafanya hivi karibuni Kutakuwa na kipindi cha miaka saba ya kwanza kitakachokuwa na shibe nyingi ya chakula na kipindi cha pili cha miaka saba kitakuwa na njaa nzito. Farao akamweka Yusufu kuwa msimamizi wa kukusanya chakula wakati wa mavuno, wakaweka akiba ya nafaka mkononi mwa Farao wakakilinda kuwa chakula katika miji. Na hicho chakula kitakuwa akiba ya nchi kwa ajili ya miaka hiyo saba ya njaa, itakayokuwa katika nchi ya Misri, nchi isiharibike kwa njaa. Chakula hiki alichokusanya Yusufu kiliwasaidia ndugu zake pamoja na watu wa nchi zote waliokuja Misri kwa Yusufu ili wanunue nafaka kwa sababu njaa ilikuwa nzito katika dunia yote mfano huu unatufundisha kuwa kuweka akiba  ni jambo la kiroho na ni mpango wa Mungu.Lazima ujifunze kuomba kwa Mungu kwamba akusaidie kuweka akiba yako kwa namna ambayo hutahamisha tegemeo lako kutoka kwa Mungu na kuweka kwenye akiba yako.Kumbuka Luka 12:15 -21 kuhusu shamba la mtu mmoja tajiri lililokuwa limezaa sana,akaanza kuwaza moyoni mwake, akisema nifanyeje, akaamua kuvunja ghala zake na kujenga kubwa zaidi akaweka akiba ya mavuno yake kisha akajiambia, Ee nafsi yangu una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi, pumzika basi ule, unywe ufurahi. Lakini Mungu akamwambia, mpumbavu wewe usiku huu wa leo wanataka roho yako! na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?. Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba asijitajirishe kwa Mungu. Msiweke imani kwenye akiba ukaacha kuweka imani kwa Mungu wako.  

Kijana apate mke mwema mwenye hofu ya Mungu.

Katika maswali yanayoulizwa na wazazi lengo lake kuu ni kumsaidia kijana apate mke mwema. Neno la Mungu linasema kuwa mke mwema hutoka kwa BWANA. Mithali 19:14 Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye, bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA. Mke mwema ni yule mwenye hofu ya Mungu anayemcha, anayemheshimu kwa kuwa ni Mungu mwenye enzi, mwenye nguvu, mamlaka na utukufu. Apataye mke wa aina hii amepata kitu chema, naye ajipatia kibali kwa BWANA.

 

Mke mwenye utii na adabu namna hii huheshimiwa na watu wote. Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe. Yeye aendaye kwa unyofu wake humcha BWANA wala ugomvi haupo moyoni mwake.Maana ni afadhali kukaa katika pembe ya darini, kuliko katika nyumba pana pamoja na mwanamke mgomvi. Katika kitabu cha Mithali 31:10-31 sifa za mke mwema zimeelezwa kama ifuatavyo:-

 


Mithali 31

10 Mke mwema , ni nani awezaye

             kumwona?

     Maana kima chake chapita kima

             cha marijani.

11 Moyo wa mumewe humwamini,

      Wala hatakosa kupata mapato .

12 Humtendea mema wala si

            mabaya,

      Siku zote za maisha yake .

13 Hutafuta sufu na kitani;

      Hufanya kazi yake ya mikono

             kwa moyo.

14 Afanana na merikebu za biashara;

     Huleta chakula chake kutoka

             mbali.

15. Tena huamka kabla haujaisha

            usiku,

        Huwapa watu wa nyumbani

            mwake chakula;

        Na wajakazi wake sehemu zao.

16 Huangalia shamba akalinunua,;

      Kwa mapato ya mikono yake

            Hupanda mizabibu.

17. Hujifunga nguvu viunoni kama

            mshipi;

Hutia mikono yake nguvu .

18. Huona kama bidhaa yake ina

            faida;

        Taa yake haizimiki usiku.

19.Hutia mikono yake katika

            kusokota;

      Na mikono yake huishika pia .

20. Huwakunjulia maskini mikono

            yake;

       Naam,huwanyoshea wahitaji

            mikono yake.

21  Hawahofii theluji watu wa

            nyumbani mwake;

         Maana wote wa nyumbani

            Mwake huvikwa nguo

                        nyekundu.

22.Hujifanyia mazulia ya urembo;

    Mavazi yake ni kitani safi na

            urujuani.

23. Mume wake hujulikana

            malangoni;

       Aketipo pamoja na wazee wa

             nchi.

24.Hufanya nguo za kitani na

             kuziuza;

      Huwapa wafanyabiashara

            mishipi.

25. Nguvu na hadhi ndiyo mavazi

            yake,

       Anaucheka wakati ujao.

26. Hufumbua kinywa chake kwa

            hekima,

       Na sheria ya wema i katika ulimi

            wake.

27. Huangalia sana njia za watu wa

            nyumbani mwake;

      Wala hali chakula cha uvivu.

28. Wanawe huondoka na kumwita

            heri;

        Mumewe naye humsifu na

             kusema, 

29. Binti za watu wengi wamefanya

            mema,

      Lakini wewe umewapita wote .

30 Upendeleo hudanganya , na uzuri

            ni ubatili;

       Bali mwanamke amchaye

            BWANA, ndiye

            atakayesifiwa.

31 Mpe mapato ya mikono yake,

      Na matendo yake yamsifu

            malangoni.

 

Kijana aoe katika familia au ukoo unaomwabudu Mungu.

Mwanzo 24:1-4. Basi Ibrahimu alikuwa mzee mwenye miaka mingi na BWANA alikuwa amembariki Ibrahimu katika vitu vyote .Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu, nami nitakuapisha kwa BWANA, Mungu wa Mbingu na Mungu wa nchi, kwamba hutamtwalia mwanangu mke katika binti za wakaanani ambao nakaa kati yao; bali enenda hata nchi yangu na kwa jamaa zangu ukamtwalie mwanangu Isaka mke.  Ibrahim akamhakikishia mtumishi wake kuwa Mungu atampeleka malaika wake mbele yake. Katika mlango huu wa Mwanzo 24 Neno la Mungu linatuonyesha jinsi Mungu alivyomwongoza mtumishi yule hadi kumpata Rebeka.

Jambo ninalotaka kulisisitiza hapa ni kuwa Mungu anaagiza kuwa vijana wetu wasioane na watu wasiomwabudu na kumcha Mungu wa Mbingu na Nchi.Kutoka 34:11-17 liangalie neno hili ninalokuamuru leo, tazama mbele yako namtoa Mwamori na  Mkaanani, na Muhita na Mperizi, na Mhivi na Myebusu. Ujihadhari nafsi yako, usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi ile unayoiendea, lisiwe mtego katikati yako. Bali utabomoa madhabahu zao, na kuvunja vunja nguzo zao, na kuyakatakata maashera yao. Maana hutamwabudu Mungu mwingine kwa kuwa BWANA, ambaye jina lake ni mwenye wivu, ni Mungu mwenye wivu.Usije ukafanya agano na wenyeji wa nchi watu wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao na kuitolea sadaka miungu  yao, mtu mmoja akakuita, ukaila sadaka yake. Ukawaoza wana wako binti zao, nao binti zao wakaenda kufanya uzinzi na miungu yao, wakawavuta wana wenu wafanye uzinzi na miungu yao .Katika Kumbukumbu la Torati 7:1-5 Mungu anaendelea kuagiza kuwa, “BWANA Mungu wako atakapokutia katika Nchi uendayo kuimiliki, atakapoyang’oa mataifa mengi watoke mbele yako Mhiti na Mgirgashi,na Mwamori na Mkaanani na Mperizi, na Mhivi na Myebusi Mataifa saba makubwa yenye nguvu kukupita wewe; wakati BWANA, Mungu wako atakapowatoa mbele yako, nawe utawapiga, wakati huo ndipo utawaondoa kabisa, usifanye agano nao, wala kuwahurumia, wala usioane nao, binti yako usimpe mwanawe mume wala usimtwalie mwanao mume binti yake. Kwa kuwa atamkengeusha mwanao mume asinifuate, ili wapate kuabudu miungu mingine.

Nabii Yoshua anaendelea kuwaonya wana wa Israel wasioane na watu wa mataifa wasiomwabudu Mungu wa Israel. Yoshua 23:12 “Lakini mkirudi nyuma   kwa njia yoyote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu na kuoana nao na kuingia kwao nao, kuingia kwenu, jueni hakika ya kuwa BWANA Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii  njema, ambayo BWANA, Mungu wenu amewapa ninyi”.

Mungu anakasirika tusipotii maagizo na amri zake, hasira yake inawaka juu yetu nasi tunakuwa chukizo mbele yake.Wana wa Israeli walipowaoa wanawake wa Moabu hasira za BWANA zikawa juu ya Israel. Hesabu 25:4-9 Kisha BWANA akamwambia Musa, watwae wakuu wote wa hao watu ukamtungikie BWANA watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za BWANA ziwaondokee Israeli. Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao. Katika Kumbukumbu la Torati 7:10 “naye huwalipa wamchukiao mbele ya uso wao , kuwaangamiza.Hatakuwa mlegevu kwake yeye amchukiaye, atamlipa mbele ya uso wake. Basi zishike amri, na sheria na hukumu ninazokuamuru leo, uzitende.“ Asama BWANA, Mungu wa Israeli.

Nabii Yoshua anatufundisha kwamba tutakapovunja maagizo ya BWANA Mungu wetu aliyotupa BWANA atatufikilizia mabaya yote, hata atakapotuangamiza katika nchi hii njema aliyotupa.

1Wafalme 11:1-4 “ Mfalme Suleiman akawapenda wanawake wengi wageni pamoja na binti yake Farao, wanawake wa Wamoabi na wa Waamoni, na wa Waedomi, na wa Wasidoni na wa Wahiti na wa mataifa BWANA aliyowaambia msiingie kwao, wala wasiingie kwenu kwa kuwa hakika  wataigeuza mioyo yenu kuifuata miungu yao.

Sulemani akaambatana nao kwa kuwapenda. Akawa na wake mia saba binti za kifalme na masuria mia tatu, nao wakeze wakamgeuza moyo wake. Maana ikiwa Sulemani alipokuwa mzee wake zake wakamgeuza moyo wake afuate miungu mingine wala moyo wake haukuwa mkamilifu kwa BWANA, Mungu wake, kama moyo wa Daudi baba yake. “Basi BWANA akamghadhibikia Sulemani kwa sababu moyo wake umegeuka, naye amemwacha BWANA, Mungu wa Israeli, aliyemtokea mara mbili. Kwa hiyo BWANA akamwambia Sulemani, kwa kuwa umefanya hayo, wala huku yashika maagano yangu na sheria zangu nilizokuamuru, hakika nitaurarua ufalme usiwe wako, nami nitampa mtumishi wako.

2Wakorintho 6: 14-18 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema ya kwamba, nitakaa ndani yao na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.Kwa hiyo tokeni kati yao mkatengwe nao asema BWANA, msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribisha .Nitakuwa baba kwenu, nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, asema BWANA Mwenyezi.

Ezra 9:1-15. Na mambo hayo yalipokwisha kutendeka , wakuu wakanikaribia, wakisema , Watu wa Israel , na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, wamefanya sawasawa     na machukizo yao, yaani ya Wakaanani, na Wahiti, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi na wa Misri na Waamori. 2 Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili. 3 Nami niliposikia hayo, nikararua nguo yangu na joho yangu, nikang’oa nywele za kichwa change, na ndevu zangu, nikaketi kwa mshangao. 4 Ndipo wakanikusanyikia watu wote waliyoyatetemekea maneno ya Mungu wa Israel, kwa sababu ya lile kosa la watu wa uhamisho; nami nikaketi kwa mshangao hata wakati wa sadaka ya jioni.

5 Na wakati wa sadaka ya jioni nikainuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za BWANA, Mungu wangu; 6 nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu ; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu , na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. 7 Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi na wafalme wetu, na makuhani wetu,tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyanga’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu kama hivi  leo. 8 Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na BWANA, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu. 9 Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi,ili kutuburudisha , kuisimamisha nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka,atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu. 10 Na sasa Eeh Mungu wetu, tuseme nini baada ya hayo?Maana tumeziacha amri zako, 11ulizoziamuru kwa midomo ya watumishi wako, manabii ukisema, nchi ile mnayoiendea ili kuimiliki ni nchi ya uchafu,kwa sababu ya uchafu wa watu wa nchi zile, kwa ajili ya machukizo yao, yaliyoijaza tangu upande huu  mpaka upande huu,kwa uchafu wao.  12 Basi msiwape wana wao binti zenu, wala msitwae binti zao kuwa wake za wana zenu, wala msiwatakie amani wala kufanikiwa milele; ili mpate kuwa hodari, na kula wema wa nchi hiyo, na kuwaachia watoto wenu iwe urithi wa milele. 13 Na baada ya hayo yote yaliyotupata kwa sababu ya matendo yetu mabaya, na kwa sababu ya hatia yetu iliyo kuu, ikiwa wewe Mungu wetu hukutuadhibu kama tulivyostahili kwa maovu yetu, tena umetupa mabaki; 14 je! tuzivunje tena amri zako, tukajiunge na watu wanaotenda machukizo hayo, kwa kuoana nao? Je! Usingekasirika nasi hata kutuangamiza kabisa, pasisalie mabaki yoyote, wala mtu wa kuokoka? Ee BWANA, Mungu wa Israel, wewe ndiwe mwenye haki, maana sisi tumesalia, mabaki yaliyookoka, kama hivi leo; tazama, sisi tupo hapa wenye hatia mbele zako; maana hapana mtu awezaye kusimama mbele zako kwa sababu ya jambo hili.     

Wana wa Israeli walipotambua kosa lao walimwambia Ezra, sisi tumemkosea Mungu wetu, nasi tumeoa wanawake wageni wa watu wa nchi hizi, lakini kungaliko tumaini kwa Israel katika jambo hili. Haya basi! Natufanye agano na Mungu wetu, kuachana na wake zetu na wale waliozaliwa nao tukilifuata shauri la bwana wangu, na shauri la hao wanaoitetemekea amri ya Mungu wetu; mambo haya nayatendeke kwa kuifuata torati .Tukiziungama dhambi zetu kama walivyofanya wana wa Israeli wakati wa Nabii Ezra Mungu anatusamehe dhambi zetu na kutubarikia. Basi jueni ya kuwa BWANA ,Mungu wenu ndiye Mungu, Mungu mwaminifu, ashikaye agano lake na rehema zake kwao wampendao, na kushika amri zake, hata vizazi elfu .Kumbukumbu la Torati 7:12-15 “ Na itakuwa kwa sababu mwazisikiliza hukumu hizi na kuzishika na kuzitenda, basi BWANA Mungu wako atakutimilizia agano na rehema aliyowaapia baba zako, naye atakupenda na kukubarikia na kukuongeza tena atabariki uzao wa tumbo lako na uzao wa nchi yako nafaka zako na divai yako na mafuta yako, maongeo ya ng’ombe zako na wadogo wa kondoo zako, katika nchi aliyowaapia baba zako kuwa atawapa.Utabarikiwa kuliko mataifa yote, hakutakuwa na mtu mume wala mke aliye tasa kati yenu, wala kati ya wanyama wenu wa mifugo. Na BWANA atakuondolea ugonjwa wote, wala hatatia juu yako maradhi yoyote mabaya uyajuayo ya Misri, lakini ataweka juu yako wakuchukiao”. Mungu anasema katika Kutoka 19:5-6 “sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu, maana dunia yote pia ni mali yangu. Nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu”. Mungu wetu anawarehemu maelfu wampendao na kuzishika amri zake; ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi .BWANA ni mkuu na BWANA wetu yu juu ya miungu yote.

Basi wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.

Kijana awe na nyumba yake atakayoishi na familia yake 

Katika mila na desturi za Kipare kijana anayetaka kuoa anatakiwa kuwa na nyumba yake atakayoishi na familia yake. Kijana haruhusiwi kuoa na kuishi nyumba moja na baba yake au mama yake.Anatakiwa ajitegemee kwa kuwa na makazi yake mwenyewe .Neno la Mungu katika Waefeso 5:31 linasema hivi, “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. “ Kijana wa kiume ndiye anayetakiwa kuachana na baba yake na mama yake .Tafsiri ya kuachana inaweza kuwa na maana ya kimwili au kiroho. Katika mada hii tafsiri ninayoiongelea ni ile ya kijana kuondoka nyumbani kwa baba na mama na kuanzisha maisha ya unyumba katika nyumba yake. Kwa njia hii kijana ataweza kuambatana vyema na mkewe na kuwa mwili mmoja.Wataweza kufanya maamuzi yao ya namna ya jinsi ya kujenga familia yao bila kuingiliwa na baba wala mama .Mithali 24:27 “Tengeneza kazi yako huko nje, jifanyizie kazi yako tayari shambani, Ukiisha, jenga nyumba yako. “Katika mlango huo aya ya tatu na ya nne Neno la Mungu linasema kuwa,“Nyumba hujengwa kwa hekima na kwa ufahamu huthibitika, na kwa maarifa vyumba vyake hujazwa vitu vyote vya thamani na vya kupendeza”. Kwa kuzingatia neno hilo sio suala la kujenga nyumba tu bali ni pamoja na kuweka samani za kupendeza. Kijana atakapoweza kuzingatia maneno hayo baba yake na mama yake watashangilia na kufurahi kwa kuzaa mtoto mwenye hekima.Mungu anabariki vijana wamchao, Zaburi 128:3 “Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao, vyumbani mwa nyumba yako. Wanao kama miche ya mizeituni wakiizunguka meza yako”. Tazama atabarikiwa hivyo siku zote za maisha yake yule amchaye BWANA.

Wakati Mungu anapokubariki hivyo huna budi kutambua ya kwamba, Zaburi 127:1-5 BWANA asipoijenga nyumba waijengao wafanya kazi bure BWANA asipoulinda mji yeye aulindaye akesha bure. Kazi yenu ni bure, mnaoamka mapema, na kukawia kwenda kulala , na kula chakula cha taabu; yeye humpa mpenzi  wake usingizi .Tazama , wana ndio urithi wa BWANA, Uzao wa tumbo ni thawabu . Kama mishale mkononi mwa shujaa, ndivyo walivyo wana wa ujanani. Heri mtu yule aliyejaza podo lake hivyo Naam hataona aibu wanaposema na adui langoni. Ni vyema kijana awe na nyumba yake kwa kuwa Bwana wetu Yesu Kristo anatembelea nyumba zetu .Bwana Yesu alimwambia Zakayo katika Luka 19:5-6, “Na Yesu alipofika mahali, alitazama juu, akamwambia, Zakayo shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka akashuka, akamkaribisha kwa furaha”. Ukiwa na nyumba yako unaweza kumkaribisha Bwana Yesu kama alivyofanya Martha, Luka 38:1 “ Ikiwa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja, mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake”. Katika nyumba zetu tusisahau kuwafadhili wageni, maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.Tumfungulie Bwana Yesu milango ya nyumba zetu kwa sababu anasema, Ufunuo 3:20 “Tazama, nasimama mlangoni, nabisha, mtu akiisikia sauti yangu na kufungua mlango nitaingia kwake nami nitakuwa pamoja naye na yeye pamoja nami. “ Baada ya kujenga nyumba tukumbuke kumshukuru Mungu kwa kufanya ibada ya kubariki nyumba katika; Jina la Baba na la Mwana, na la Roho Mtakatifu. Amen.

 Hitimisho

Tuhitimishe mada hii ya kijana wa Kikristo “Kukoloka” kwa kuwakumbusha vijana wetu kuwa wanapotangaza kuwa wamekuloka wametangaza vita na shetani .Lengo la kukoloka ni kuoa kuwa na familia na kuendeleza uumbaji wa Mungu .Kwa kuwa tunajua shetani atapiga vita lengo hili vijana wetu hawana budi kusimama imara katika maombi yaliyojengwa katika Neno la Mungu. Kila kijana anayekuloka amwomba Mungu ampatie mke mwema kutoka kwake kulingana na Neno Lake. Mke atakaye mtii sawa na Neno lake. Waefeso 5:22-24 “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo”. Kila kijana amwombe Mungu ampe roho ya upendo ili ampende mke mwema aliyetoka kwa Mungu kulingana na neno lake. Waefeso 5:25-30. “ Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi  wala lolote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayechukia mwili wake popote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake”. Lakini kila mtu ampende mke wake kama nafsi yake mwenyewe; wala mke asikose kumstahi mumewe.

Wazazi wafanye maombezi kwa ajili ya kijana aliyekuloka sawasawa na Neno la Mungu.Ee Baba wa mbinguni umjalie Roho Mtakatifu wako kijana wetu aliyekuloka na anayekusudia kuoa ili siku zote awe na furaha ya upendo wako mkuu, na adumu katika upendo huo mpaka mwisho wa maisha yake.Imarisha moyo wake ili kila wakati azidi kuwa na imani kwako, akupendeze wewe katika yote, na aweze kufikia siku ya kuungana na mwenzi wake katika ndoa takatifu.

Wazazi wakumbuke kuanza kipindi cha kijana kukoloka kwa, sala na kumaliza kwa kutoa shukrani kwa Mungu. Shukrani hizo ziambatane na sadaka kwa kuwa sadaka ina nguvu ya kukuunganisha na madhabahu ya mafanikio yako.

Mungu Baba yetu tunakuomba uwasaidie vijana wetu wakue katika hekima na kimo, wsakikupendeza wewe na wanadamu. Kubali, waongoze na watawale vijana wetu kwa njia ya roho mtakatifu wako ili waweze kukua katika neema na maarifa ya Neno lako. Uwajaalie ili waweze kukutumikia wewe vyema na kwa maarifa, wakikuza vipaji vyao si kwa manufaa yao tu bali kwa utukufu wako Mungu na kwa manufaa ya watu wote. Uwalinde na kuwahifadhi katika hatari na mashaka ukiwatumia malaika wako kuwa pamoja nao, wazikimbie tamaa za ujanani, wakafuate haki, imani, upendo na amani. Kwa ajili ya Yesu Kristo, Bwana wetu.

Share This