NAFASI YA MWANAMUME KATIKA KUMTUMIKIA MUNGU KULINGANA NA NENO LAKE.
1. Mwanamume ni mfanyakazi katika shamba la BWANA.
Mungu alipomuumba Adamu alimpata kazi ya kulima na kuitunza bustani ya Edeni ( Mwanzo 2:15) Bustani ya Edeni au shamba la Mungu kwetu sisi ni ulimwengu Mungu aliouumba, anataka tuulime na kuutunza kimwili na kiroho. Anatuagiza twende ulimwenguni kote tukaihubiri Injili kwa watu wote na viumbe (Marko 16:15). Kimwili tunatakiwa tulime ardhi ili itupe chakula. Mungu akamwambia Adamu kwa jasho la uso wako utakula chakula tena kwa uchungu. Ili tule mazao ya ardhi lazima tufanye kazi kwa bidii hadi jasho litutoke. Ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula (2 Wathesalonike 3:10). Mungu anatutia nguvu katika Isaya 1:19 anasema “ kama mkikubali na kutii mtakula mema ya nchi.” Ndugu zangu tukubali kutii amri za Mungu ili kupata mafanikio katika maisha yetu yote. Tumtumikie BWANA, Mungu wetu, kwa furaha na moyo wa kushukuru.
2. Mungu amempa mwanamume mbegu ya uzao.
Bila mbegu hii hakuna uzao wakati agizo la Mungu la uumbaji ni kuzaa na kuijaza nchi na kuitiisha (Mwanzo 1:28). Mwanamke hawezi kuzaa bila kupokea mbegu hii katika yai lake la uzazi. Mbegu hii ndiyo inayoamua mtoto awe wa kike au wa kiume kwa kuwa ni “X and Y Chromosomes.’’ Mwanzo 4:1 “Adamu akamjua Hawa mkewe, naye akapata mimba, akamzaa Kaini, akasema, nimepata mtoto mwanaume kwa BWANA.’’ Akaongeza akamzaa ndugu yake Habil.
3. Mwanamume ni mtawala, msimamizi au kiongozi wa familia na kanisa.
Mungu ameweka wanaume ili wamtumikie katika familia na katika kanisa katika nafasi za uongozi na utawala. Baada ya Adamu na Hawa kutenda dhambi, Mungu alimteua Adamu kuwa kiongozi na mtawala. Mwanzo 3:16 (a) “tamaa yako itakuwa kwa mumeo naye atakutawala.’’ Neno la Mungu linamtaka mwanamume mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu, yaani mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje kanisa la Mungu? I Timotheo 5:17 “Wazee watawalao vema na wahesabiwe kustahili heshima maradufu, hasa wao wajitaabishao kwa kuhutubu na kufundisha.’’ Katika nafasi hii ya uongozi neno la Mungu linamtaja mwanamume kuwa ni kichwa cha mkewe. Waefeo 5: 23 “kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha kanisa naye ni mwokozi wa mwili.’’ Maneno haya yanapatikana pia katika 1 Wakorintho 11:3 ambapo Mtume Paulo anaongeza kwa kusema kuwa kichwa cha Kristo ni Mungu. Kwa kuwa baba ndiye kiongozi wa familia mke wake, watoto na watu wa nyumba yake hawana budi kumtii, kumheshimu na kumsikiliza. Kichwa cha familia ni lazima kijenge familia yenye utaratibu mzuri, familia yenye furaha na amani inayomletea Mungu utukufu.
4. Mwanamume ana wajibu wa kuihudumia familia yake kimwili na kiroho.
1 Timotheo 5:8 “lakini mtu yeyote asiyewatunza walio wake, yaani, wale wa nyumbani mwake, hasa ameikana Imani, tena ni mbaya kuliko mtu asiyeamini.’’ Tengeneza mambo ya nyumbani kwako kwa kuwa kuna baraka na kibali. Pamoja na kuhudumia watu wako kwa vitu vya mwilini, vyakula, mavazi, malazi, elimu na mengine mengi unatakiwa kuwahudumia kiroho. Ibada njema huanzia nyumbani kwa watu wa nyumba yako kumwabudu Mungu katika roho na kweli. Kwa njia hiyo utapata baraka na watu wa nyumbani mwako watakuwa na maisha ya furaha, amani na upendo, Sema kama Joshua kuwa mimi na nyumba yangu tutamtumikia BWANA. Neno la Mungu linatutaka kufundisha, kuonya kwa upole, kukirimu kwa moyo mweupe na kusimamia nyumba zetu kwa bidii katika Yesu Kristo Bwana wetu. Tukimtumikia Mungu kwa bidi tutasimama mbele ya wafalme. Mithali 22:9 “Je wamwona mtu mwenye bidii katika kazi zake? Huyo atasimama mbele ya wafalme.’’ Tukimtumikia Mungu kwa bidii na uaminifu atatuheshimu na atabariki kazi za mikono yetu sawa sawa na neno lake.
5. Mzaliwa wa kwanza mwanamume ni malimbuko kwa BWANA.
Katika kila familia mtoto wa kwanza wa kiume kuzaliwa ni malimbuko kwa BWANA kwa hiyo amepewa nafasi ya pekee kulingana na neno la Mungu. Tunatakiwa tumtolee BWANA sadaka ya malimbuko bila kukawia. Kutoka 22:29 “Usikawie kuleta malimbuko ya matunda yako na vinywaji vyako. Mzaliwa wa kwanza katika wanao wanaume utanipa mimi. Nawe utafanya hivyo katika ng’ombe zako na kondoo wako”. Mungu amewapa nafasi ya pekee wazaliwa wa kwanza, amewatenga kwa ajili yake. Wamepewa nafasi ya kubeba baraka za familia na ukoo. Mungu amewapa wazaliwa wa kwanza nguvu, uwezo, ukuu, mamlaka na uongozi katika kumtumikia au katika kutumikia kusudi lake. Mzee Yakobo alijua jambo hili akamwambia Reubeni, u mzaliwa wa kwanza, nguvu zangu na malimbuko ya uwezo wangu, umewapita wengine kwa ukuu na nguvu (Mwanzo 49:3). Mzaliwa wa kwanza kwa sheria za Bwana alitakiwa apelekwe hekaluni kwa BWANA, hivyo na Bwana wetu Yesu Kristo alipelekwa. Luka 2:22 “Kisha zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wakamweka kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana. Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana), wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana. Hua wawili au makinda ya njiwa wawili. “Je, sisi wakristo wa leo tumempa Bwana wazaliwa wetu wa kwanza? Sio kwa sheria kama kwenye Agano la kale bali kwa hiari yetu na kwa kupenda kwa kuwa tunajua ya kwamba jambo hilo linampendeza Mungu. Tuwahudhurishe wazaliwa wetu wa kwanza na kuwaweka madhabahuni kwa Bwana kwa njia ya maombi na sadaka. Tumwombe Mungu awabariki na awape nguvu, uwezo,ukuu, mamlaka na uongozi wa familia wazaliwa wetu wa kwanza sawa sawa na neno lake. Jina la BWANA lihimidiwe.
6. Baba anayo nafasi ya kubariki.
Mungu na mwanae Yesu Kristo ndio wanaotubariki na ndio wanaotupa sisi uwezo wa kubariki. Kuanzia uumbaji Mungu alibariki na kuona kuwa vyote ni vyema. Mungu anabariki wanadamu, viumbe, ardhi, sabato na vyote sawa sawa na neno lake. Waefeso 1:3 “Atukuzwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, aliyetubariki kwa baraka zote za rohoni”. Yesu Kristo ni kisima cha baraka kwetu kutoka kwa Mungu. Matendo ya Mitume 3:26 “Mungu akiisha kumfufua mtumishi wake Yesu, alimtuma kwenu ninyi kwanza, ili kuwabarikia kwa kumwepusha kila mmoja wenu na maovu yake”. Kabla ya kupaa mbinguni Bwana Yesu aliwaongoza wanafunzi wake mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki (Luka 24:50). Kutokana na kisima hiki cha Baraka za Mungu na mwanaye Yesu Kristo na sisi tumepewa uwezo wa kubariki watoto, ndugu, kanisa, taifa na ulimwengu wote. Kumbuka baraka sio zako bali ni za Mungu mwenyewe, wewe ni chombo tu cha kupitishia baraka hizo. Mtu aliyebarikiwa na BWANA ana uwezo wa kubariki na kupokea baraka. Katika Agano la kale, baba wa imani Ibrahimu, Isaka na Yakobo walibariki watoto wao. Mwanzo 49:28 kupitia kwa Ibrahimu kabila zote za dunia zimebarikiwa, kama kweli ni uzao wa Ibrahimu na uzao wa Bwana wetu Yesu Kristo. Watabarikiwa wamchao BWANA, wadogo kwa wakubwa. Yakobo alikwenda kwa hila kwa baba yake Isaka, Isaka akambariki akachukua mbaraka wa kaka yake Esau (Mwanzo 27:27-29). Yakobo nae aliwakusanya watoto wake wote kumi na mbili na kuwabariki mmoja mmoja kwa mbaraka wake aliwabariki (Mwanzo 49:28). Kuna mifano mingi ya wababa waliobariki watoto wao, ni vyema tukawaiga ili na sisis tuwabariki watoto wetu. Katika mila na desturi za Kipare ukimchichia baba yako RANDO una nafasi kubwa ya kupewa baraka. (Rando ni kama mbuzi, kondoo au ng’ombe) kama ilivyofanyika kwa Isaka. Neno la Mungu linatufundisha kuwa kuna baraka zinazotoka kwa Mungu kwa watu wenye haki, wanaomtegemea na kumtumainia. Mithali 27:7 “Mwenye haki aendaye katika unyofu wake, watoto wake wabarikiwa baada yake”. Tena amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, ambaye tumaini lake lipo kwake. Neno la Mungu linatutaka tubariki wala tusilaani. Katika ukoo wa Shaidi babu yake Shaidi mzee Mkaza alionya kuwa mtu yoyote wa uzao wake asije akathubutu kulaani mtoto wa ukoo wake. Akifanya hivyo afe yeye kabla laana hiyo haijamshika aliyelaaniwa. Onyo lake liko sawasawa na neno la Mungu kuwa tusilaani hata adui zetu au wale wanaotuudhi. Warumi 12:14 “wabarikini wanaowaudhi, barikini wala msilaani”. Kwa sababu tunao moyo uliobarikiwa hivyo neno la laana lisitoke kwetu. Bwana atufundishe kamwe kutolaani, bali kubariki. Tunatakiwa kubariki watu wengine, taifa na ulimwengu kama Mungu alivyomwagiza Musa na Haruni watakavyobarikia wana wa Israeli (Hesabu 6:22-27).
Neno la Mungu liwe taa ya miguu yetu na mwanga wa njia zetu. Amen.
ONYO:
Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani (1 Timotheo 4:1). Kazi mojawapo ya shetani katika siku hizi za mwisho ni kupinga na kuzuia uzao wa binadamu usiongezeke na kuijaza nchi. Shetani ameleta mafundisho ya ndoa za jinsia moja na binadamu kubadili maumbile yao ya asili.
Mpango huu wa kupotosha dunia unasimamiwa na nchi tajiri duniani, kinyume na neno la Mungu. I Wakorintho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike, waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala wanyang’anyi.’’ Tumpinge shetani kwa kutumia neno hili naye atatukimbia. Mkaribieni Mungu naye atawakaribieni ninyi. Uchafu wa aina hii wa ndoa za jinsia moja au wa kubadilisha maumbile usitajwe kwenu kamwe. Waefeso 5:3 “Lakini uasherati usitajwe kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu.’’ Basi msishirikiane nao hao wenye matendo yasiyozaa ya giza, bali myakemee. Wala msiketi barazani pa wenye mizaha, wala msisikilize upumbavu wao. Zaburi 14:1 “Mpumbavu amesema moyoni, hakuna Mungu, wameharibu matendo yao na kuyafanya chukizo, hakuna atendaye mema. Bali wewe uzitii amri za Mungu na maagizo yake yote kwa unyenyekevu.