MATATIZO YANAYOWEZA KUWAPATA WATOTO KUTOKANA NA DHAMBI NA UOVU WA WAZAZI WAO
Wapendwa katika Yesu Kristo Bwana wetu. Yapo matatizo ambayo unaweza kuyapata kutokana na uovu wako wewe mwenyewe lakini yapo mengine yanayoweza kukupata kutokana na dhambi na uovu wa wazazi wako. Katika somo hili tutaangazia zaidi matatizo au madhara yanayoweza kumpata mtu kutokana na dhambi na uovu wa wazazi wake.
Ninaposema wazazi ninamaanisha baba, mama, babu na babu wa babu kwa upande wa baba na mama. Sina maana kuwa hakuna mema tunayoyapokea kutoka kwa wazazi wetu. Kutoka kwa wazazi wetu tunapokea vitu vya kimwili na kiroho. Tunapokea nyumba, mashamba, wanyama, fedha, malezi na mambo mengine mengi sana. Kiroho tunapokea imani ya Kikristo na mafundisho ya neno la Mungu kutoka kwao. Tunaamini katika Utatu Mtakatifu; Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Wala sina maana kuwa matatizo yote mtu anayoweza kuyapata yanatokana na dhambi na uovu wa wazazi wake. Hapana. Yohana 9:1-3 “Hata alipokuwa akipita alimwona mtu kipofu tangu kuzaliwa. Wanafunzi wake wakamwuliza wakisema, Rabi, ni yupi aliyetenda dhambi, mtu huyu au wazazi wake hata azaliwe kipofu? Yesu akajibu, huyu hakutenda dhambi wala wazazi wake; bali kazi za Mungu zidhihirishwe ndani yake”. Kumbe matatizo mengine tunayapata ili Mungu atukuzwe.
Ikiwa wazazi wetu watafanya au walifanya dhambi na uovu Mungu anaweza kuachilia matatizo au madhara kwao wenyewe au kwa watoto na uzao wao. Dhambi na uovu ambao haukutubiwa huleta uharibifu. Yanaweza yakatokea matatizo ya magonjwa, umasikini, ugumba, vifo vya hapa na pale, njaa, mambo ya aibu, huzuni, ukame, vita na mengine mengi. Maombolezo 5:7 “Baba zenu walitenda dhambi hata hawako; na sisi tumeyachukua maovu yao”. Mfalme Daudi mtumishi wa Mungu anasema hata mimba yake mama yake aliichukua hatiani. Zaburi 51:5 “Tazama, mimi naliumbwa katika hali ya uovu; mama yangu alinichukua mimba hatiani”. Mtumishi wa Mungu Ayubu yeye anasema; Ni nani awezaye kutoa kitu kilicho safi kitoke katika kitu kichafu? Hapana haiwezekani. Inawezakana kuwa kuna mambo mabaya yaani dhambi na uovu uliotendwa na wazazi wako na Mungu ameachilia adhabu juu ya maisha yako, ya familia na hata ya ukoo wako. Wana wa Israeli walimkasirisha Mungu kwa kuwa wamemwacha na kuabudu miungu mingine. Mungu akawaadhibu kwa kuwapeleka utumwani katika nchi ya ugenini. Yeremiah 16:10-13 “Tena itakuwa utakapowaonyesha watu hawa maneno haya yote, nao wakakuambia, mbona BWANA amenena juu yetu mabaya haya makuu? Uovu wetu ni uovu gani? Na dhambi yetu, tuliyomtenda BWANA, Mungu wetu, ni nini? Ndipo utakapowaambia, ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema BWANA, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu; na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaendelea kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi. Basi kwa sababu hio, nitawatoeni katika nchi hii na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu, na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku, kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo”.
Mungu anatuonya katika neno lake kuwa tusisujudie wala kutumikia miungu kwa kuwa yeye ni Mungu mwenye wivu. Anawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanaomchukia (Kutoka 20: 1-6).
Je, tutawezaje kupona hasira ya Mungu, juu ya dhambi na uovu?
Mungu ni mwenye huruma, mwenye fadhili nyingi si mwepesi wa hasira naye huwarehemu na kuwasamehe uovu na makosa na dhambi maelfu elfu wampendao na kuzishika amri zake. Tunatakiwa kutambua ya kuwa tunaweza kuwa na matatizo yanayotokana na dhambi na uovu wa wazazi wetu nasi tutangaze ya kuwa kuna maombi ya toba na rehema yanayoweza kutufungua katika matatizo hayo. Tukiziungama dhambi zetu, kwa kweli na kuziacha, basi Mungu ni mwaminifu na mwadilifu, naye atatusamehe dhambi zetu na kututakasa uovu wote. Tubu kwa ajili ya dhambi za wazazi wako. Yeremia 14:20 “Ee Bwana tunakiri uovu wetu na ubaya wa baba zetu, maana tumekutenda dhambi”. Ee Bwana utusikie kuomba kwetu, Ee Bwana utusamehe sisi na wazazi wetu, Ee Bwana usikilize, ukatende, usikawie kwa ajili ya utukufu wa jina lako. Pia mwombe Mungu asiwaadhibu watoto wako na kizazi chako kwa dhambi na uovu wako. Matendo ya Mitume 3:19 “Tubuni basi mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake Bwana”. Kwa upendo wake mkuu, upendo wa Agape Mungu ametupa silaha kubwa mno ya kushinda dhambi na uovu; ametupa damu ya Yesu Kristo na neno lake la uzima. Tutamshinda shetani kwa damu ya Mwanakondoo na kwa neno la ushuhuda. Mathayo 26:28 “Kwa maana hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi kwa ondoleo la dhambi”. Akiisha kufanya utakaso wa dhambi ndipo neno lile la unabii wa Ezekieli 18:20 litadhihirika kuwa, “Roho itendayo dhambi ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake”. Neno katika 2 Nyakati 25:4 na Kumbukumbu la Torati 24:16 “Mababa wasiuawe kwa ajili ya watoto wao, wala watoto wasiuawe kwa ajili ya baba zao; kila mtu na auawe kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe”. Kwa maana nyingine kila mtu atachukua msalaba wake mwenyewe. Luka 14:27 “Mtu yoyote asiyechukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”. Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata hanistahili. Mtu yeyote akitaka kumfuata Bwana Yesu Kristo ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, amfuate. Katika somo hili tumejifunza kwamba toba na rehema kwa kutumia damu ya Yesu na neno la Mungu ndivyo viletavyo ushindi dhidi ya matatizo yanayoletwa na dhambi na uovu. Roho Mtakatifu atuongoze ili tuepuke matendo ya mwili na kutembea katika njia ya haki.
Kila alitajae Jina la Bwana na auache uovu. Jina la BWANA lihimidiwe sasa na hata milele. AMEN.