• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 21 Oct, 2025
  • Admin

MAOMBI YETU KWA MUNGU WETU TUNAYEMWABUDU

Wakati wa kutoa sadaka zetu za shukrani kwa Mungu wetu tunayemwabudu ni wakati mzuri pia wa kueleza haja za mioyo yetu kwa Mungu wetu. Maombi ni njia majowapo amabayo Mungu ametupa ya kuweza kuongea naye na kumpa haya za    yetu. Kila mmoja wetu amweleze Mungu haja za moyo wake kuhusu yeye mwenyewe, familia yake, uzao wa Shaidi na majirani zake. Neno la Mungu linatutaka tuombe na kushukuru kwa kila jambo. Bwana wetu Yesu Kristo anatukaribisha tumwambie haja za mioyo yetu, ili zijulikane kwa Mungu wetu. Wafilipe 4:6 “Msijisumbue kwa neno lolote, bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Kwa kuwa yeye hujishughulisha sana kwa mambo yetu. Zaburi 37:4 – 5 “Nawe utajifurahisha kwa BWANA, naye atakupa haja za moyo wako.” Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.” Katika maombi yako ni vyema kabisa uwe na mstari au mistari ya neno la Mungu kusimamia maombi yako. Mkumbushe Mungu ahadi zake kwetu tunaomwamini, tunaomtumainia na kumcha. Tunatakiwa kuomba sawasawa na mapenzi ya Mungu tukimpa Mungu nafasi mioyoni mwetu ili mapenzi yake yatimizwe kwetu kulingana na neno lake takatifu. Yohana 5: 14 – 15 “Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba.” Tumepewa njia moja tu ya kuweza kuongea na Mungu na kumpa haja za mioyo yetu. Njia hiyo ni kuomba kwa jina la Yesu Kristo tukisaidiwa na Roho Mtakatifu. Yohana 16:23(b) – 24 “Amin, amin, nawaambia mkimwomba Baba neno lolote atawapa kwa jina langu. Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu; ombeni, nanyi mtapata; furaha yenu iwe timilifu.” Naye Yesu Kristo Mwokozi wetu aliye mkono wa kuume wa Mungu ndiye anayetuombea kwa Baba. Tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki. Waebrania 7:25 “Naye, kwa sababu hii, aweza kuwaokoa kabisa wao wamjiao Mungu kwa yeye, maana yu hai siku zote ili awaombee.” Atawafanyia wamchao matakwa yao, naye atasikia kilio chao na kuwaokoa. Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa (Warumi 8:26 – 28). Sisi tuliobatizwa na tunaotoa shukrani kwa BWANA tuombe kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kutubu na kuziacha dhambi zetu. Hapo ndipo tutapokea kipawa cha Roho Mtakatifu. Ahadi hii ni kwa ajili yetu, na kwa watoto wetu, na kwa watu wote walio mbali, na kwa wote watakaoitwa na Bwana Mungu wetu wamjie (Matendo ya Mitume 2:39). Mungu tunayemwabudu ni Roho na sisi tunaomwabudu yeye imetupasa kumwabudu katika roho na kweli. Mungu alibariki neno lake lijae kwa wingi ndani ya mioyo yetu, atubariki na kuzitakabali sadaka zetu tunazomtolea kwa moyo wa unyenyekevu, unyofu na wa kupenda. Amina.

Share This