KUDHARAULIWA NA KUBEZWA
Watu wasio haki wanadharau ndugu zao na kuwabeza kwa sababu wanajiona kuwa wao ni bora zaidi ya wengine, wanajiona kuwa wana elimu zaidi, fedha zaidi na wanajiona kuwa ni maarufu zaidi.
Lengo la watu wa aina hii ni kukuaibisha, kukutia unyonge na udhaifu. Neno la Mungu linatutia nguvu katika 1 Wakorintho 15:43 "Hupandwa katika aibu, hufufuliwa katika fahari, hupandwa katika udhaifu, hufufuliwa katika nguvu". Neno la Mungu linatutaka tusidharauliane kwa kuwa sisi sote ni watoto wa Mungu, warithi wa mapenzi yake. Wala usijidharau wewe mwenyewe hata kama watu wote watachagua kukudharau na kukupuuza. Ukijipa heshima mwenyewe na ukujiamini inatosha kabisa. Kumbuka Mungu huwaheshimu wale wanaomtumikia kwa uaminifu. Usijidharau kwa kuwa Mungu atakutia nguvu kama alivyofanya kwa Gideoni. Waamuzi 6:12 “Malaika wa BWANA akamtokea, akamwambia BWANA yu pamoja nawe, Ee shujaa”. Hawataweza kukuaibisha kwa sababu utapainulia patakatifu mikono yako na kumwita BWANA akusaidie usiaibike milele wala kutahayarika. Zaburi 25:2 “ Ee Mungu wangu, nimekutumaini wewe, nisiaibike, adui zangu wasifurahi kwa kunishinda”.
Mithali 11:12 "Asiye na akili humdharau mwenziwe, bali mtu aliye na ufahamu hunyamaza." Hata Bwana wetu Yesu Kristo katika njia ya msalaba alidharauliwa, alidhihakiwa, alidhalilishwa, alitukanwa na kubezwa.
Luka 23:11 "Basi Herode akamfanya duni, pamoja na askari zake, akamdhihaki." Wakamvua nguo, wakamvika vazi jekundu. Wakapiga magoti mbele yake wakamdhihaki, wakisema, salamu, mfalme wa Wayahudi kama wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi jiokoe mwenyewe. Luka 23:39 "Na mmoja wa wale wahalifu waliotungikwa alimtukana akisema, Je! Wewe si Kristo? Jiokoe nafsi yako na sisi". Lakini yeye alinyamaza hakujibu neno. Mwishowe aliwasamehe na kuwaombea msamaha kwa Mungu. Luka 23: 34 "Yesu akasema, Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui watendalo". Na sisi pia tunaamriwa tuwasamehe na kuwaombea adui zetu.
Kwa njia hii ya msalaba sisi tukaokolewa na watu wasio haki, wabaya, maana si wote walio na imani. Ukimwamini na kumfuata Bwana wetu Yesu Kristo hakika Mungu atakuokoa katika mitego yote ya wasio haki, atakukingia mabaya yote. Atakufunika kwa mabawa yake, utapata usalama kwake, mkono wake utakulinda na kukukinga. BWANA awe kimbilio lako na ngome yako, na umtumainie yeye tu. Mabaya hayatakupata wewe kwa kuwa atakuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote. Mikononi mwao watakuchukua, usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. Kwa Jina lake lenye nguvu, uweza na mamlaka tutawaangusha na kuwashinda. Tutawashinda kwa damu ya Mwanakondoo, na kwa Neno la ushuhuda. Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zetu, Amen