DANIELI 12:3 “Na walio na hekima watanga’a kama mwangaza wa anga, na hao waongozao wengi kutenda haki watanga’a kama nyota milele na milele.”
Kitabu cha Danieli kinaelezea ndoto na maono aliyoyapata Daniel kuhusu siku za mwisho. Wakati wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele. Na walio na hekima watanga’a kama mwangaza wa anga, na hao waongozao wengi kutenda haki watanga’a kama nyota milele na milele. Katika somo hili tutajifunza mambo makuu mawili; moja ni kuhusu wenye hekima na jingine ni kuhusu watenda haki .Hekima ni uwezo wa kufanya maamuzi sahihi kutokana na maarifa na ufahamu ulio nao au ni uwezo wa kutumia maarifa na ufahamu vizuri. Kuna aina kuu tatu za hekima; kuna hekima ya kibinadamu au hekima ya dunia ni elimu na ufahamu unaotokana na kusoma kwingi elimu ya dunia na hekima ya Shetani ni ile inayotumia kuwadanganya watu. Yakobo 3:15 “Hekima hiyo siyo ile ishukayo kutoka juu, bali ni ya dunia ya tabia ya kibinadamu na Shetani. Katika somo hili tutajifunza kuhusu hekima ya Mungu hekima itokayo juu. Yakobo 3:17 “Lakini hekima itokayo juu, kwanza ni safi tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” Hekima hii ni karama kutoka kwa Mungu. 1 Wakorintho 12:8 -11“Maana mtu mmoja kwa roho apewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule na mwingine karama za uponyaji, imani, miujiza, unabii, kupambanua roho, aina za lugha na mwingine tafsiri za lugha. Lakini kazi hizi akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye”. Mungu alimgawia hekima hii Bwana wetu Yesu Kristo, hekima ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wake. 1 Wakorintho 1:30 “Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki na utakatifu na ukombozi.” Kwa ajili hiyo Yesu Kristo kutoka utoto wake alikua akaongezeka nguvu, amejaa hekima na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. Luka 2; 52 “Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo akimpendeza Mungu na wanadamu.” Yesu alifundisha na kutoa mifano kwa hekima kubwa. Kila aliyemsikia Yesu alishangaa juu ya hekima yake kabla hata ya kuiangalia miujiza yake. Mathayo Mtakatifu 13:53-54 “Ikawa Yesu alipomaliza mifano hiyo, alitoka akaenda zake. Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii?. Ni hekima hii ambayo tunatakiwa kumwomba Mungu atugawie kwa kuwa yuko tayari kutugawia . Yakobo 1:5-6 “Lakini mtu kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu, awapaye wote kwa ukarimu wala hakemei; naye atapewa.” Ila anaeomba kwa imani, pasipo shaka yoyote naye atapewa, awe mtakatifu, mnyenyekevu, mwenye hofu ya Mungu anaye mcha Mungu. Mithali 11:2 “Kijapo kiburi ndipo ijapo aibu; bali hekima hukaa na wanyenyekevu na Zaburi 111:10 mwimba Zaburi anasema, “Kumcha BWANA ndio mwanzo wa hekima. Wote wafanyao hayo wana akili njema sifa zake zakaa milele. Mithali 2:5-7 “Ndipo utakapofahamu kumcha BWANA na kupata kumjua Mungu. Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. Huwawekea wanyofu akiba ya hekima kamili. Yeye ni ngao kwao waendao kwa ukamilifu.” Tuangalie kwa kifupi faida au umuhimu wa kuwa na hekima ya Mungu, hekima itokayo juu.Hekima ni nguvu itokayo kwa Mungu ambayo inawapa nguvu watu wa Mungu ikiwa ni pamoja na nguvu ya kuhubiri Neno lake au habari njema.Mithali 24:5 “Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maaarifa huongeza uwezo.” Mithali 8:11-12, Maana hekima ni bora kuliko marijani; wala vyote vinavyotamanika havilingani nayo. Mimi, hekima nimefanya werevu kuwa kao langu, natafuta maarifa na busara.” Si afadhali kupata hekima kuliko dhahabu. Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko dhahabu? Naam, yafaa kuchagua ufahamu kuliko fedha.Mhubiri anatufundisha kuwa hekima ndiyo bora kupita silaha za vita kwa maana hekima ni ulinzi wa Mungu. Mhubiri 7:11-12 “Hekima ni njema, mfano wa urithi; Naam nayo ni bora kwao walionao juu. Kwa maana hekima ni ulinzi kama vile fedha ilivyo ulinzi na ubora wa maarifa ni ya kwamba hekima humhifadhi yeye aliyo nayo.” Katika Biblia Takatifu kuna mtu mmoja aliyepewa na Mungu nafasi ya kuomba atakalo na Mungu atampa naye akachagua hekima. 2 Mambo ya Nyakati 1:7-12, “Usiku ule Mungu akamtokea Sulemani akamwambia, Omba utakalonikupe. Basi sasa nipe hekima na maarifa, nijue kutoka na kuingia mbele ya watu hawa; kwa kuwa ni nani awezaye kuwahukumu watu wako hawa walio wengi? Naye Mungu akamwambia Sulemani, kwa sababu neno hili lilikuwamo moyoni mwako wala hukujitakia mali, wala utajiri wala utukufu, wala maisha za wachukiao, wala hukujitakia maisha ya siku nyingi; bali umejitakia hekima na maarifa, upate kuwahukumu watu wangu, niliokutawaza juu yao;basi hekima na maarifa umepewa; nami nitakupa mali, utajiri na utukufu, kupita walivyokuwa navyo wafalme wote waliokuwa kabla yako, wala baada yako hapatakuwa na mtu atakayekuwa navyo.” Mungu akampa Sulemani hekima na akili nyingi sana na moyo mkuu kama mchanga ulioko pwani. Hekima ya Sulemani ikapita hekima kuliko watu wote na sifa zake zikaenea katika mataifa yote yaliyomzunguka.
Tunatakiwa kulishika Neno la Mungu na mausia yake kwa kuwa Neno la Mungu ni hekima ya Mungu. Mithali 13:1 “Mwana mwenye hekima husikiliza mausia ya babaye. Bali mwenye dharau hasikilizi maono”. Waefeso 5:15. “ Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda, si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima , mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu .Kwa sababu hiyo msiwe wajinga, bali mfahamu ni nini yaliyo mapenzi ya Bwana. Hekima inatusaidia kujua wakati sahihi wa kufanya jambo, kama vile wakati wa kunyamaza na wakati wa kusema. Neno linasema tukipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kushitakiwa kwa ajili ya jina la Bwana tuwe watulivu tusipayuke payuke ovyo. Luka 21:14-15. “Basi kusudieni mioyoni mwenu ,kutofikiri –fikiri kwanza mtakavyojibu ; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga”. Katika somo hili tumeona sifa, umuhimu na faida za watu walio na hekima ya Mungu ambazo zinawafanya wanga’e kama mwangaza wa anga . Mhubiri 8:1 “Ni nani aliye kama mwenye hekima naye ni nani ajuaye kufasiri neno? Hekima ya mtu humnga’ariza uso wake na ugumu wa uso wake hubadilika”. Mtu mwenye hekima anajulikana kwa kazi zake za haki.
Katika sehemu ya pili ya somo hili tutajifunza kuhusu hao waongozao wengi kutenda haki ambao watanga’aa kama nyota milele na milele.
Tuanze kwa kuangalia haki ni nini? Kwa tafsiri rahisi haki inatumika kama uhalali wa kufanya jambo fulani au kupata jambo fulani wakati mwingine haki ni kile unachokistahili baada ya kutekeleza wajibu fulani. Haki inaambatana na hukumu inayotolewa bila ya upendeleo wowote tena haki inaambatanaa na ukweli bila udhalimu wowote. Kuna haki za kibinadamu na haki za Mungu. Haki za kibinadamu zinapatikana katika sheria, kanuni na taratibu za kimila na kiutamaduni. Kuna haki za watoto, wanawake, walemavu na haki nyingine nyingi. Haki hizi zinapatikana katika katiba za nchi na mikataba ya Kimataifa. Katika somo hili tutajifunza kuhusu haki ya Mungu. Haki ya Mungu ni uadilifu na utakatifu wake. Haki hii inapatikana katika neno lake takatifu. Neno la Mungu linatushuhudia ya kwamba Mungu ni mwenye haki. Kumbukumbu la Torati 32:4.“Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; maana njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu Yeye ndiye mwenye haki na adili.” Matendo yake yote ni kweli na njia zake ni za adili ndiye Mungu wa kweli aliye hai, Mfalme wa milele. Mungu wetu ni mwenye haki katika kazi zake zote azitendazo. BWANA ndiye afanyaye mambo ya haki, akihukumu kwa haki kila mtu pasipo upendeleo kwa kadiri ya kazi yake. Mungu huyafanya haya yote kwa kuwa yeye ni mtakatifu na haki iko ndani yake. Warumi 1:17 “Kwa maana haki ya Mungu inadhihirishwa ndani yake, toka imani hata imani, kama ilivyoandikwa mwenye haki ataishi kwa imani.”
Bwana wetu Yesu Kristo kama alivyo Baba yake naye ni mweye haki. 1Yohana 2:1-2 “Watoto wangu wadogo nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba Yesu Kristo mwenye haki naye ndio kipatanisho kwa dhambi zote, wala si kwa dhambi zetu tu, bali na kwa dhambi za ulimwengu wote.” Kwa maana nyingine tunahesabiwa haki katika damu yake ambayo inatuokoa na ghadhabu ya Mungu. Kwa mauti yake tumepatanishwa na Mungu, kadhalika kwa kutii kwake watu wengi wameingizwa katika hali ya wenye haki. Wagalatia 2:16 “Hali tukijua ya kuwa mwanadamu hahesabiwi haki kwa matendo ya sheria, bali kwa imani ya Yesu Kristo; sisi tulimwamini Kristo Yesu ili tuhesabiwe haki kwa imani ya Kristo, wala si kwa matendo ya sheria; maana kwa matendo ya sheria hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki,” Tunaokolewa kwa neema ya Mungu ipitayo akili zote za kibinadamu. Tunahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu kwa njia ya imani katika damu yake, ili aonyeshe haki yake. Ni wajibu wetu kupokea neema hii. Tito 2:11–12 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa.” Katika aya hizi tumejifunza ya kuwa tunahesabiwa haki, itokayo katika imani na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo imefunuliwa ndani yake; na furaha katika tumaini la utukufu wa Mungu.
Kama Baba wa mbinguni na Mwanae Yesu Kristo walivyo wenye haki na sisi tunatakiwa vivyo hivyo kuwa wenye haki. Tuangalie mistari michache ya Neno la Mungu inayotufundisha yatupasayo kufanya ili tuhesabiwe haki na Mungu. Mtu wa haki anapaswa kuwa mkamilifu anayekwenda pamoja na Bwana kama alivyofanya Nuhu. Mwanzo 6:9,“Hivi ndivyo vizazi vya Nuhu. Nuhu alikuwa mtu wa haki, mkamilifu katika vizazi vyake; Nuhu alikwenda pamoja na Mungu. Kwenda pamoja na Mungu ni kughairi uovu na kuacha dhambi. Kufuata amri zake kwa moyo wa unyofu na kutenda yaliyo halali na haki. Kama vile Ibrahimu baba yetu wa imani alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki. Maandiko Matakatifu yanatufundisha kuwa Mungu atawahesabia haki kwa imani (Mwanzo3:6-8). Iman inayozungumziwa hapa ni kumwamini Mungu na Mwanaye pekee Yesu Kristo Bwana wetu. Warumi 3:22 “Ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio.”Wamwaminio kwamba ni Bwana na mwokozi wa maisha yao. Hao wanakaa ndani yake na yeye anakaa ndani yao. Tusiwe na imani ya kusitasita ili tumfurahishe Bwana wetu. 1 Waebrania 10:38 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisitasita, roho yangu haina furaha naye.” Imani inaambatana na kutenda mema na kuhukumu kwa haki bila ya upendeleo wowote. 2 Petro 1:5 “Naam, kwa sababu hiyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema na katika wema wenu maarifa na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi na katika saburi yenu utauwa na katika utauwa wenu upendano wa ndugu na katika upendano wa ndugu upendo.” Ni katika upendo huu tunatakiwa tuwahukumu ndugu na majirani zetu kwa haki na upendo .Mambo ya Walalwi 19:15”. Msitende yasiyo haki katika hukumu. Usimpendelee mtu masikini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.” Neno la Mungu linatufundisha kuzitengeneza njia zetu ili tukihukumu tuhukumu kwa haki kati ya mtu na jirani yake bila ya kumwonea mgeni wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia wala kuifuata miungu mingine (Yeremia 7:5-6). Ili tuwe wenye haki na tuweze kuwaongoza wengine kutenda haki tunatakiwa tutwae silaha zote za Mungu ambazo ni Neno lake Takatifu .Waefeso 6:14-17 “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani, zaidi ya yote mkitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale ya yule mwovu. Tena ipokeeni chapeo ya wokovu na upanga wa Roho ambao ni Neno la Mungu. “Haki ni silaha muhimu sana katika vita hii ya kupigana na dhambi. Mithali 14:35 “Haki huinua taifa, bali dhambi ni aibu ya watu wote.”
Tuendelee na somo hili kwa kuangalia ahadi za Mungu kwa watu wenye haki .Neno linasema watanga’aa kama nyota milele na milele. Mathayo 13:43 “Ndipo wenye haki watakaponga’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao. Mwenye masikio na asikie.” Katika 1 Wakoritho 15:41 anasema, “Kuna fahari moja ya jua na fahari nyingine ya mwezi na fahari nyingine ya nyota, maana iko tofauti ya fahari hata kati ya nyota na nyota.” Tafsiri rahisi ya neno fahari ni kitu au jambo la kujivunia. Fahari ya jua na nyota zinaonyesha fahari ya Mungu au utukufu wa Mungu katika uumbaji wake wa mbingu na nchi.
Kwa maneno mengine wenye haki ni fahari mbele ya Mungu na macho ya BWANA huwaelekea wenye haki, wenye haki wanaona fahari katika Kristo Yesu mbele za Mungu awahesabiaye haki. Kama ilivyoandikwa yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana. Wagalatia 6:14 “Lakini mimi, hasha nisione fahari juu ya kitu chochote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulubishwa kwangu na mimi kwa ulimwengu.” Wenye haki watairithi nchi au watakula mema ya nchi na kupata baraka nyingi. Bwana huwapenda wenye haki na kuwabariki. Mithali 10:6 “Baraka humkalia mwenye haki kichwani. “Mwenye haki atalipwa mema tena upo upendeleo kwa wenye haki asema BWANA. Wenye haki wanayo ahadi ya wokovu wa Bwana na uzima wa milele.Watapata uzima wa milele na kukaa pamoja na Bwana Yesu mahali alipo lakini waovu wataadhibiwa .Mathayo 25:46 “Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.” Tunatakiwa tudumu katika kutenda haki na tuwe na juhudi katika kutenda mema ili tupate ufalme wake na haki yake.
Mungu huchukizwa mno na watu wasio haki yaani wasiotenda haki au kuwaongoza watu wengi kutenda haki. Nafsi ya Mungu humchukia asiye haki na mwenye kupenda udhalimu. Maana watenda mabaya wataharibiwa, asiye haki hatakuwepo na mikono ya wasio haki itavunjika. Isaya 10:1-4 “Ole wao wawekao amri zisizo za haki na waandishi waandikao maneno ya ushupavu, ili kumpotosha mhitaji asipate haki yake, na kuwanyang’anya masikini wa watu wangu haki yao, ili wajane wawe mateka yao, na kuwafanya yatima waliofiwa na baba zao kuwa mawindo yao! Nanyi mtafanya nini siku ya kujiliwa na wakati wa uangamivu, utakaokuja kutoka mbali sana? Je, mtamkimbilia nani mpate msaada? Na utukufu wenu mtawacha wapi? Watainama chini ya wafungwa tu, wataanguka chini waliouwawa pamoja na hayo yote hasira yake haikugeukia mbali, lakini mkono wake umenyoshwa hata sasa.” Na mkono wake ulionyoshwa ni nani atakayeugeuza nyuma?. Mtu mwovu atakapokufa taraja lake hupotea na kuangamia motoni. Natusimameni mbele ya BWANA kwa unyofu kwa kuwa wanyofu wa moyo watamwona uso wake. BWANA hutega sikio lake kwa maombi yao, nao watalishukuru jina lake na watakaa mahali alipo Yeye.
Zaburi 37:25, 39-40 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, lakini sijamwona mwenye haki ameachwa wala uzao wake akiomba chakula. Na wokovu wa wenye haki una BWANA. Yeye ni ngome yao wakati wa taabu. Naye BWANA huwasaidia na kuwaopoa; huwaoopoa na wasio haki na kuwaokoa; kwa kuwa wamemtumaini Yeye.” Kwa kuwa tumeyajua haya yote kwa neema ya Mungu natudumu katika kutenda haki, mwenye haki na azidi kufanya haki; na mtakatifu na azidi kutakaswa. Amina.