AHADI ZA MUNGU KWA WATEULE WAKE
Mungu anazo ahadi nyingi sana kwa wateule wake, na hapa nitaelezea chache tu. Mungu anasema atakaa ndani yao na kati yao atatembea, atakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wake, tena maskani ya Mungu yatakuwa pamoja nao. Ezekieli 37:26-28 “Tena nitafanya agano la amani pamoja nao; nami nitawaweka na kuwazidisha na patakatifu pangu nitapaweka katikati yao milele.” Zaidi ya hapo anawaahidi wateule wake kuwa atawajalia maisha marefu. Ikiwa Mungu anatuahidi mambo mema namna hii tunangoja nini kutoka katikati ya mataifa. 2 Wakorintho 6: 17-18 “Kwa hiyo tokeni kati yao mkatengwe nao asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wakike, asema Bwana Mwenyezi”. Tokeni kwao enyi watu wangu msishiriki dhambi zao mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya BWANA. Ukishaokoka pamoja na kazi nyingi za wateule moja wapo ya kazi ni kutangaza matendo makuu na fadhili zake Yeye aliyetuita na kututoa gizani na kutuingiza katika nuru yake ya ajabu (1 Petro 2:9b). Tukatangaze kama mtumishi wa Mungu Danieli; Danieli 4:2-3 “Mimi nimeona vema kutangaza habari za ishara na maajabu aliyonitendea Mungu aliye juu. Ishara zake ni kubwa kama nini. Na maajabu yake yana uwezo kama nini. Ufalme wake ni ufalme wa milele, na mamlaka yake ni ya kizazi hata kizazi.” Sisi tunaomtolea Mungu sadaka za shukrani tunamwomba Mungu kwa neema yake kuu, autenge uzao wetu uwe mteule kwake. Huku tukijua ya kuwa Bwana, Mungu wetu ndiye Mungu, Mungu mwaminifu, mwenye upendo na rehema nyingi. Ashikaye agano lake na rehema zake kwao wapendao na kushika amri zake hata vizazi elfu. Neno la Mungu ni taa ya miguu yetu linatuongoza kila tuendapo. BWANA anasema mtu atakayemwangalia ni mtu mnyonge, mwenye roho iliyopondeka, atetemekaye asikiapo neno lake.
Tutafakari ahadi ya Mungu kuwa atawajalia wateule wake maisha marefu, na kuwa wateule wake watafurahia matunda ya jasho lao (Isaya 65: 21-25). Katika kutafakari njia zetu tunaomba Roho Mtakatifu atufundishe yote na kutukumbusha mafundisho yote ya Bwana wetu Yesu Kristro ili tuijue kweli yote. Amen