• elisheshe@yahoo.com
  • +255765837485
  • 16 Apr, 2025
  • Admin

SIFA ZA MUNGU WETU.

Mungu wetu tunayemwabudu anazo sifa nyingi sana zisizoweza kuhesabika. Matendo yake ni makuu na ya ajabu. Katika somo hili nitashuhudia na kusimulia machache yanayodhihirisha uzuri na ukuu wa Mungu wetu.

1.     Mungu wetu ni mwenye enzi yote muumbawa mbingu na nchi. Kwake vitu vyote viliumbwa vinavyoonekana na visivyoonekana, tunavyovijua na tusivyovifahamu. Mimi na wewe tu zao la uumbaji wake (Mwanzo 1:1 – 31). Mungu akaona kila kitu alichokifanya na tazama, ni chema sana.

2.     Mungu wetu ni mmoja tu hakuna Mungu mwingine tena, yeye ni Mungu wa miungu hakuna Mungu kama yeye. Ni Mungu wa kweli na wa pekee. 1 Wakorintho 8:6 “Lakini kwetu sisi Mungu ni mmoja tu, aliye Baba, ambaye vitu vyote vimetoka kwake, nasi tunaishi kwake; yuko na Bwana mmoja Yesu Kristo, ambaye kwake vitu vyote vimekuwepo, na sisi kwa yeye huyo”. Je, sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? (Malaki 2:10)

3.     Mungu wetu ni Alfa na Omega Ufunuo1:8“Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, asema Bwana Mungu, aliyeko na aliyekuwako na atakayekuja, Mwenyezi”.  Umilele ni sifa moja wapo ya Mungu. Mungu ni yuleyule jana hata leo na hata milele na milele, ni Mungu asiyebadilika yeye ni BWANA asiyekuwa na kigeugeu, akisema ndio hakuna wa kupinga wala wa kusema hapana. Nchi na vyote viijazavyo ni mali yake; vyote vyenye mwili ni mali yake kwa hiyo mimi na wewe tu mali yake.

4.     Mungu wetu ni Roho nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katikarohona kweli (Yohana 4:24). Yupo mahali pote kila wakati lakini haonekani kwa macho haya ya nyama isipokuwa katika macho ya Rohoni. Kwa njia ya roho Mtakatifu tutamwona Mungu akifanya kazi katika maisha yetu. Kwa sababu mambo yake yasiyoonekana tangu kuumbwa ulimwengu yanaonekana, na kufahamika kwa kazi zake; yaani, uweza wake wa milele na Uungu wake; hata wasiwe na udhuru (Warumi 1:20). Kila siku na kila wakati. Waefeso 1:18 “Macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo: Mtumishi wa Mungu mfalme Daudi anaonyesha kuwa Roho wa Mungu yupo kila mahali katika Zaburi 139: 7 – 8 niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama nikipanda mbinguni, Wewe uko; ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.” Macho ya Bwana  yako kila mahali; yakimchunguza mbaya na mwema (Mithali 15:3)

5.     Mungu wetu ni mwenye uweza wa mambo yote mbunguni na duniani. Hakuna jambo gumu la kumshinda BWANA wa majeshi aliyeumba mbingu na nchi. Mkononi mwake mna uweza na nguvu, asiweze mtu ye yote kusimama kinyume chake. 1 Mambo ya Nyakati 29:11 “Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza na utukufu, na kushinda, na enzi, maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee BWANA, nawe umetukuzwa u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote na mkononi mwako mna uweza na nguvu. “Mungu mwenye uweza na nguvu anajua kila kitu na ana uweza wa kufanya jambo lolote lile sawa sawa na mapenzi yake, hahitaji msaada wa aina yo yote yupo huru kutenda cho chote atakacho. Waefeso 3:20 “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu. Uweza wa Mungu hauwezi kupimwa na mwanadamu yo yote yule wala kulinganishwa kwa maana yeye ni Mungu Mkuu.

6.     Mungu wetu ni wa utukufu na utukufu wake umejaa mbinguni na duniani. Utukufu wa Mungu unajidihirisha katika heshima kuu isiyopimika kwa akili za binadamu.  Utukufu wa Mungu unaonekana katika utakatifu wake, ukamilifu, uaminifu, haki na neema yake , rehema, huruma na upendo wake, pamoja na matendo yake makuu na ya ajabu. Yuda 1:25 “Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo na nguvu, tangu milele, na sasa na hata milele”. Katika Ufunuo wa Yohana 4: 11 neno la Mungu linasema, “Umestahili wewe,Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako, navyo vikaumbwa” Mbingu zauhubiri utukufu wa  Mungu, na anga laitangaza kazi ya mikono yake (Zaburi 19:1). Duniani nako mataifa yanahubiriwa juu ya utukufu wake. 1 Mambo ya Nyakati 16:24 – 31 “wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake”. Kwa kuwa ni BWANA mkuu mwenye kusifiwa sana. Heshima na adhama ziko mbele zake, nguvu na furaha zipo mahali pake. Mpeni BWANA, enyi jamaa za watu, mpeni BWANA utukufu na nguvu. Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; leteni sadaka mje mbele zake. Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu. Tetemekeni mbele zake nchi yote. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie. Basi, mlapo au mnywapo, au mtendapo neno lolote, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.

7.     Mungu wetu ni Mtakatifu Mambo ya Walawi 11:45 “kwa kuwa mimi ni BWANA niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu”. Utakatifu huo huwezi kuupata ukiwa nje ya Kristo, kwa hiyo ni lazima uokoke. Mtumishi wa Mungu, Daudi katika Zaburi 99:5,9 “Mtukuzeni BWANA, Mungu wetu; sujuduni kwenye kiti cha miguu yake; ndiye Mtakatifu”. Na wewe U Mtakatifu, uketiye juu ya sifa za Israeli, walishukuru jina lako kuu la kuhofiwa; kwa kuwa wewe U Mtakatifu. Tunapokiri kuwa Mungu wetu ni Mtakatifu tunasema kwa maneno mengine kuwa Mungu wetu ni mkamilifu. kwa kila jambo asilimia mia (100%), hana dhambi wala dosari yoyote ile. Kazi zake ni kamilifu na njia zake ni za haki, Mungu anatutaka na sisi tuwe wakamilifu. Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”. Uwe mkamilifu mbele za BWANA, Mungu wako kwa kuwa haki yake yakaa milele. Na sisi kwa kujua ukweli huu tunaimba; Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, BWANA Mungu wa majeshi; mbingu na nchi zimejaa utukufu wako. Mungu anapendezwa na watakatifu walioko duniani.

8.     Mungu wetu ni mwenye neema nyingi. 

Neema ni kupata kitu ambacho hukukistahili. Neema ni upendeleo wa Mungu usio na sababu au kukubaliwa bila kustahili. Neema inaweza kuwa ni kuzuia uharibifu, neema ya kupewa haki, neema ya ukombozi au utakaso. Neema ya Mungu inapatikana bure. BWANA akaamua kumfutilia mbali mwanadamu na viumbe wote; lakini Nuhu akapata neema machoni kwa BWANA (Mwanzo 6:5-8). Musa naye alipata neema mbele za Mungu alipotumwa kuwatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri. Mwanzo 33:17 “Bwana akamwambia Musa, nitafanya na neno hili ulilolinena kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako”. Bwana wetu Yesu Kristo alijaa neema ya Mungu. Luka 2:40 “Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake”. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu. Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli. Kutoka kwa Bwana wetu Yesu Kristo tunapokea neema juu ya neema. Yesu Kristo ametuita kwa neema yake ili atuokoe kutoka katika dhambi; tunaokolewa kwa neema na tena neema yake yatosha. Tito 2:11 “Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa; na yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia, na utawa, katika ulimwengu huu wa sasa”. Neema ya Mungu inaambatana na huruma, wema na fadhili, hekima, haki, kweli na kumjua Mungu na Yesu Kristo Bwana wetu. Na sasa, nawasihi, ombeni fadhili za Mungu ili atupe neema kuwa kilemba chetu. Maneno yanayotoka vinywani mwetu yajae neema ya Mungu (Malaki 1:9).

9.     Mungu wetu ni mwingi wa rehema.

Kutoka 20:6 “Nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao na kuzishika amri zangu”. BWANA ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa. Hesabu 14:19 “Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa. BWANA akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa”. Mtu mbaya na aache njia yake, na mtu asiye haki aache mawazo yake na amrudie BWANA, naye atamrehemu, na arejee kwa Mungu wetu, naye atamsamehe kabisa (Isaya 55:7). Mungu ni mwingi wa rehema na kweli na kwa mapenzi yake ametuhuisha pamoja na Kristo. Rehema za Mungu hazikomi ni mpya kila asubuhi, uaminifu wake ni mkuu kwa hiyo nitamtumaini yeye.

·       Rehema za Mungu wetu huambatana na huruma, wema na fadhili; Maombolezo 3:22 “Ni huruma za BWANA kwamba hatuangamii, kwa kuwa rehema zake hazikomi”. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. BWANA ni mwema kwa watu wote, na rehema zake zi juu ya kazi zake zote (Zaburi 145:8-9). Mungu ni mwingi wa huruma, mwenye fadhili, si mwepesi wa hasira, mwingi wa rehema na kweli, mwenye kuwaonea huruma watu elfu elfu, mwenye kusamehe uovu na makosa na dhambi (Kutoka 34:6-7). Bwana ni mwingi wa rehema mwenye huruma na fadhili zake ni za milele. Mungu anatuagiza katika Waefeso 4:32 kuwa, “Tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi”. Tuseme kama mtumishi wa Mungu, Daudi Zaburi 23:6 “Hakika wema na fadhili zitanifuata siku zote za maisha yangu nami nitakaa nyumbani mwa BWANA milele. 

·       Rehema za Mungu huambatana na upendo; Mungu wetu ni mwenye upendo, upendo wa Agape au wa ki-Mungu. Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”.  Huu ndio upendo wa Agape, upendo usiokuwa na masharti yoyote, ni upendo wa hali ya juu sana. Hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake (Yohana 15:13). Upendo wa Mungu unapaswa ukuchochee kumpenda kwa moyo wako wote, kwa roho yako yote, kwa nguvu zako zote na kwa akili yako yote. Upendo wa Mungu hauna ubaguzi maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki (Mathayo 5:45). Hakuna kitu chochote chini ya jua kitakachoweza kututenga na upendo wa Mungu ulioko katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Katika somo hili tumejifunza sifa chache za Mungu wetu. Sifa zake hazipimiki wala kuhesabika, lakini jambo moja tunalijua kuwa tunatakiwa tumpende Mungu na jirani yetu. Mathayo 22:37-39 “Akamwambia Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote”. Na ya pili inayofanana nayo, nayo ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Jambo lingine tunalolijua ni kuwa Mungu anapendezwa na sifa za mioyo yetu. Anastahili sifa, enzi na utukufu. Njooni tumsifu Mungu kwa nyimbo, zaburi na tenzi tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu.

 

Share This